Tuesday, July 11, 2017

Masauni aliagiza Jeshi la Polisi kufungua kituo makazi ya kabila la Wahazabe


 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akiwafafanulia jambo Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, Flatei Massay (kulia) na Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mjini, Zakaria Isaay mara baada ya Naibu waziri huyo kukagua Jengo la Mifugo (nyuma yao) ambalo linatarajiwa kufunguliwa Kituo cha Polisi ili kuwasaidia wananchi wa kabila la Wahazabe na wengineo wanaoishi katika Bonde la Yueda Chini, Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara kuleta ulinzi wa raia hao pamoja na mali zao.
Na Felix Mwagara (MOHA)
 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amelitaka Jeshi la Polisi mkoani Manyara kufungua Kituo cha Polisi katika Makazi ya Kabila la Wahazabe wanaoishi katika Bonde la Yueda Chini, wilayani Mbulu. 
Masauni alisema hayo jana wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa kabila  hilo mara baada ya kukagua jengo la mifugo katika eneo la bonde hilo ambalo jamii hiyo ilijitenga kwa kuweka makazi pembezoni mwa Mji wa Mbulu. 
“Hivi karibuni Kituo cha Polisi kitafunguliwa hapa ili kulinda usalama wenu katika eneo hili ambalo lilikua halina kituo cha Polisi kwa miaka mingi. Serikali ya Rais Magufuli ni sikivu ndio mana nimekuja hapa kuwasikiliza matatizo yenu na kuwatekelezea.” Alisema Masauni huku akishangiliwa na wananchi hao. 
Aliongeza kuwa, mchakato wa kujenga kituo hicho umeanza na tayari ametoa maelekezo kwa Kamanda wa Jeshi la Polisi wa Mkoa huo, kwa kushirikiana na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Wabunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini na Mbulu Mjini. 
Pia aliongeza kuwa, uhalifu katika eneo hilo sasa umepata tiba kwa maana Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi watahakikisha hali ya usalama unaimarishwa zaidi katika eneo hilo ambalo lipo. 
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, Flatei Massay alisema wananchi wa jimbo lake wanavamiwa, wanaporwa mali zao ikiwemo mifugo, wanajeruhiwa na wanaingizwa katika umaskini zaidi kutokana na waalifu kuwa wengi kutokana na ukosefu wa Kituo cha Polisi. 
“Nilimuomba na nilimsumbua sana Naibu Waziri kule Bungeni ili aweze kufika katika eneo hili, ninamshukuru sana kwa kufika na kutoa maelekezo ya kufunguliwa kituo cha polisi, sasa wakazi wa eneo hili tunatarajia kupata ulinzi wa kutosha baada ya kituo hicho kufunguliwa hivi karibuni,”alisema Massay. 
Mkuu wa Jeshi la Polisi mkoani humo, Francis Massawe alisema amepokea maelekezo kutoka kwa Naibu Waziri na mchakato utaanza rasmi na hatimaye kituo cha Polisi kitakuwepo katika eneo hilo na wananchi wataendelea na shughuli zako za kutafuta mahitaji yao kwa usalama zaidi.

MONDAY, JULY 10, 2017

WAVAMIZI WA MAENEO YA HIFADHI ZA RELI WAPEWA MIEZI SITA

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngoyani ametoa Miezi sita kwa wakazi wa Mpanda Mkoani Katavi kuondoka katika maeneo ya hifadhi za Reli ili kupisha maboresho yanayoendelea kufanywa na Shirika la Reli Tanzania (TRL) kwenye miundombinu yake.
Ametoa agizo hilo wakati akiongea na wafanyakazi wa taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo Mkoani Mpanda na kusema ni wakati sasa kwa wananchi kufuata sheria kwa kutovamia miundombinu hiyo.
“Ninatoa miezi sita kuanzia sasa, itakapofika Mwezi Januari mwakani wananchi wote watakaokuwa ndani ya hifadhi ya reli watabomolewa nyumba zao kwa kuzingatia sheria zinazolinda miundombinu,” alisisitiza Eng. Ngonyani.
Naibu Waziri Eng. Ngonyani ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Mpanda kusimamia zoezi la wananchi kuhama na kuhakikisha kila aliyevamia miundombinu hiyo anabomoa nyumba yake kabla ya sheria kufata mkondo wake.
Aidha, Eng. Ngonyani amewatahadharisha wafanyakazi wa Wakala wa barabara nchini (TANROADS) kuzingatia maslahi mapana ya Taifa wakati wa kutafuta zabuni kwa kufanya hivyo watakuwa wanamuunga Mkono Mhe. Rais Dkt. John Magufuli.
Katika hatua nyingine Eng. Ngonyani amekagua barabara ya Kanazi-Kizi-Kibaoni (76.6KM), Sumbawanga-Kanazi (75KM) ambapo ameiagiza TANROADS Mkoa wa Rukwa kuweka mizani katika barabara zinazojengwa ili kudhibiti magari makubwa yanayozidisha uzito na kusababisha uharibifu kwa barabara katika Mkoa huo.
“Ni wakati sasa wanaotoa huduma za usafirishaji wa mizigo kufuata  sheria na kubeba mzigo wa uzito unaostahili sababu madereva hao hao wakienda nchi za jirani wanafuata sheria kwa umakini, SUMATRA simamieni utoaji wa leseni kwa magari ya abiria na mizigo kwa kuzingatia uzito wa magari ili kuziweshesha barabara zetu zidumu,” alisisitiza Eng. Ngonyani.
Kwa upande wa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Rukwa, Eng. Msuka Mkina amemuhakikishia Naibu Waziri kuwa Wakala utahakikisha Mizani inawekwa sehemu za barabara  ili kubaini Magari yanayozidisha uzito na kuyachukulia hatua za kisheria.
Naibu Waziri Eng. Ngonyani yupo katika Ziara ya kukagua Miundombinu ya barabara, Viwanja vya Ndege, Ujenzi wa Nyumba za viongozi, huduma za mawasiliano ya simu   na Madaraja katika Mkoa wa Katavi na Rukwa.
 Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani akitoa maelekezo kwa Meneja wa Kampuni ya Simu (TTCL) mkoa wa Rukwa na Katavi Bw. Peter Kuguru wakati alipokagua eneo ambalo Mkongo wa Taifa umeharibika kwa kuliwa na panya Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa.
 Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani (Katikati) akiangalia ramani ya Mkongo wa Taifa wakati alipokagua eneo ambalo Mkongo wa Taifa umeharibika kwa kuliwa na panya Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa.
 Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani (Kulia) akitoa maelekezo kwa Mkandarasi anayejenga barabara ya Kanazi-Kizi-Kibaoni (76.6KM) Wakati alipokagua ujenzi wa barabara hiyo kwa  kiwango cha lami.
 Meneja wa Kampuni ya Simu (TTCL) mkoa wa Rukwa na Katavi Bw. Bw. Peter Kuguru (aliyenyoosha kidole) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani wakati alipokagua eneo ambalo Mkongo wa Taifa umeharibika kwa kumegwa na panya Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa.
 Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani (Kulia) akipokea maelezo ya kifaa maalumu cha kugundua sehemu ambayo mkongo wa Taifa una tatizo kutoka kwa Bw. Juma Ngimba (Kulia), wakati alipokagua eneo ambalo Mkongo wa Taifa umeharibika kwa kuliwa na panya Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa.
Muonekano wa barabara ya Kanazi-Kizi-Kibaoni (76.6KM), ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami umekamilika.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, 
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments:

Post a Comment