Monday, October 16, 2017

DKT TIZEBA AFUNGA MAADHIMISHO YA SIKU YA CHAKULA DUNIANI


Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya kitaifa ya siku ya chakula Duniani, yaliyofanyika katika Uwanja wa CCM Kalangalala Mkoani Geita.
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba alipotembelea banda la Kampuni ya POLYTECH MACHINERY inayojishughulisha na uuzaji wa mashine mbalimbali ikiwemo za kukamua mafuta ya alizeti wakati wa maadhimisho ya siku ya kitaifa ya siku ya chakula Duniani, yaliyofanyika katika Uwanja wa CCM Kalangalala Mkoani Geita. Mwingine ni Mhe Dkt Mary Mwanjelwa Naibu waziri wa Kilimo (Kulia).
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya kitaifa ya siku ya chakula Duniani, yaliyofanyika katika Uwanja wa CCM Kalangalala Mkoani Geita.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Mary Mwanjelwa akizungumza jambo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Methew Mtigumwe wakati wa maadhimisho ya siku ya kitaifa ya siku ya chakula Duniani, yaliyofanyika katika Uwanja wa CCM Kalangalala Mkoani Geita.



Na Mathias Canal, Geita

Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba leo Octoba 16, 2017 amefunga rasmi maadhimisho ya siku ya kitaifa ya siku ya chakula Duniani, yaliyofanyika katika Uwanja wa CCM Kalangalala Mkoani Geita kuanzia Octoba 10 mpaka Octoba 16, mwaka 2017.

Akizungumza katika Kilele cha Maadhimisho hayo waziri Tizeba alisema kuwa Kuanzia msimu huu wa kilimo Wakulima wa korosho watapata bure pembejeo aina ya salfa zilizokuwa zikiuzwa kwa bei ya ruzuku.

Alisema Hatua hiyo ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuhakikisha vikwazo vyote vilivyokuwa, vikiwakabili Wakulima wa zao la korosho vinaondolewa ili kuwawezesha kuongeza uzalisha na tija zaidi kutokana na zao hilo.

Mhe Tizeba alisema Madhumuni ya Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani ni kutoa nafasi ya kutafakari, namna Jamii katika ngazi ya Kaya, Kijiji, Kata, Tarafa, Wilaya, Mkoa, Taifa na Kimataifa zinavyoweza kuhakikisha ongezeko la uzalishaji na upatikanaji wa chakula cha kutosha na chenye lishe bora kwa watu wote na kwa wakati wote. 

Alisema kuwa Kila mwaka Shirika la Chakula Duniani (FAO) baada ya kufanya tathmini ya hali ya Chakula hutoa Kaulimbiu ambayo huwa ni dira ya maandalizi na maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani. 

Kaulimbiu ya mwaka huu 2017 inasema “Badili mwelekeo wa uhamaji; Wekeza katika usalama wa chakula na maendeleo Vijijini”. Kaulimbiu hii inaweka umuhimu katika kuweka Mipango na Programu zinazolenga kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo Vijijini; kupuza utegemezi na kuongeza usawa katika Jamii, sambamba na uhifadhi mazingira ambayo ndiyo muhimu katika maendeleo ya kilimo na hifadhi ya Jamii ili yachochee jitihada za kuondoa umaskini.

Alisema kuwa maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kwa mwaka huu ni ya kujivunia kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika uongozi wa Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli, kwa kipindi chote nchi yetu imejitosheleza kwa chakula kwa zaidi ya asilimia 100 na hivyo kuwa na ziada ya chakula. 

Uzalishaji wa mazao ya chakula kwa mwaka 2016/2017 umefikia Tani 15,900,864 za chakula kwa mlinganisho wa nafaka. Kati ya kiasi hicho, tani 9,388,772 ni za mazao ya nafaka na tani 6,512,092 ni za mazao yasiyo nafaka. 

Hata hivyo Mahitaji ya chakula kwa mwaka 2017/2018 yatakuwa Tani 13,300,034 ambapo Tani 8,457,558 ni kwa mazao ya nafaka na Tani 4,842,476 ni mazao yasiyo nafaka. 

Dkt Tizeba aliongeza kuwa Kutokana na uzalishaji huu, nchi itakuwa na kiwango cha utoshelevu wa asilimia 120 ambapo kiwango hiki kinaonyesha kuwa nchi itakuwa na ziada ya chakula ya Tani 2,600,831 ambapo mazao ya nafaka kutakuwa na ziada ya Tani 931,214 na mazao yasiyo nafaka ni Tani 1,669,617 kwa viwango vya utoshelevu vya asilimia 111 na 134 mtawalia. Alisema Ziada hii inatosha kwa matumizi ya chakula hapa nchini na kuwa na ziada ya kuuza.

Katika hatua nyingine Mhe waziri wa kilimo ametumia fursa hiyo kuwaasa wananchi wote kuwa na hifadhi ya chakula katika kaya zao na kutumia chakula kilichopo kwa uangalifu hadi msimu mwingine wa mavuno. 

‘‘Wahenga walisema usione vyaelea vimeundwa; hivyo mafanikio tuliyoyapata ni matokeo ya jitihada za Serikali, Wadau, Wabia wa Maendeleo na Wananchi wote kwa ujumla wao kwa kuendelea kushiriki katika shughuli za maendeleo hususani kilimo, ufugaji, uvuvi na huduma mbalimbali zinazotolewa, Aidha zipo changamoto mbalimbali zikiwemo, mabadiliko ya tabianchi, ambayo kwa kiasi kikubwa yanachangia kupungua kwa uzalishaji na tija ya mazao, uhaba wa malisho ya mifugo na rasilimali maji lakini Tumejipanga kuendelea, kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni pamoja na kuzalisha mbegu bora zinazovumilia ukame, magonjwa na kutoa mavuno mengi” Alisema Mhe Dkt Tizeba 

Sambamba na hilo, alisema kuwa serikali imejipanga kuendelea kuwaelimisha na kuwasaidia Wafugaji wa Tanzania, kufuga kitaalamu zaidi ili kuepuka ile hali ya kuhamahama kwa ajili ya kutafuta malisho na maji. 

Kilele cha maadhimisho ya siku ya Chakula Dunia ilihudhuriwa na Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala, Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Mwakilishi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, Miji na Majiji, Viongozi wa Vyama vya Siasa, na Viongozi wa Dini. 

No comments:

Post a Comment