Wednesday, October 18, 2017

SERIKALI YA IRELAND YAPONGEZA TASAF KWA KUTEKELEZA MPANGO WA KUNUSURU KAYA MASIKINI KWA MAFANIKIO.



 Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Ladislaus Mwamanga akitoa maelezo kwa waziri wa Mambo ya nje wa Ireland namna shughuli za kuhawilisha fedha zinavyotekelezwa kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini.
 Waziri wa Mambo ya Nje wa Ireland akizungumza na Mkurugenzi wa TASAF,Ladislaus Mwamanga  wakati waliposhuhudia zoezi la kulipa ruzuku kwa baadhi ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya masikini katika wilaya ya  Misungwi,mkoani Mwanza.
 Waziri wa Mambo ya Nje wa Ireland Ciaran akipata maelezo kutoka kwa baadhi ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani Misungwi unaotekelezwa na TASAF namna walivyonufaika na huduma za Mpango huo.
 Mkuu wa mkoa wa Mwanza,John Mongela akihutubia wananchi (hawapo pichani ) katika ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ireland( aliyeketi kushoto )
 Waziri wa Mambo ya nje wa Ireland aliyeshika kipaza sauti akiwahutubia baadhi ya walengwa wa TASAF (hawapo pichani) katika wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongela (aliyevaa kofia) akiwa na mgeni wake waziri wa Mambo ya Nje wa Ireland wakiwa na baadhi ya walengwa wa TASAF wakiwa na vyeti vya bima ya afya ya jamii waliyopata baada ya kujiunga na bima hiyo kwa kutumia  sehemu ya ruzuku ya  TASAF.



NA ESTOM SANGA- MISUNGWI

Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa kimataifa wa Ireland bwana Ciar`an Cannon T.D amepongeza jitihada za serikali ya Tanzania katika kuboresha huduma za jamii na kuwajengea uwezo wa kiuchumi wananchi hususani wanaokabiliwa na umaskini .

Bwana Ciar`an ametoa pongezi hizo alipofanya ziara katika wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza ambako amekutana na Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF na kupata ushuhuda wa namna walivyonufaika na Mpango huo.

Baadhi ya Wananchi wanaonufaika na huduma za TASAF wamemweleza waziri huyo kuwa tangu waorodheshwe kwenye Mpango wameboresha maisha yao kwa huku wakijengewa misingi ya kujitegemea kwa kuanzisha miradi midogo midogo ya kiuchumi,kuboresha na makazi yao .

Aidha baadhi ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini wameeleza kuwa wamepata mafanikio makubwa katika sekta ya elimu na afya katika kaya zao baada ya kujiunga na Mfuko wa Afya Jamii kwa kutumia fedha walizozipata kutoka TASAF na hivyo kuwapungizia mzigo mkubwa wa matibabu katika kipindi cha mwaka mzima,jambo ambalo wamesema limeboresha afya zao.

Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Ireland amesema serikali yake imevutiwa na utekelezaji wa shughuli za TASAF na ili kuunga mkono juhudi hizo imepanga kuchangia kiasi cha shilingi bilioni 7.3 katika kipindi cha mwaka huu ili kufanikisha shughuli za Mpango huo ambao ni miongoni mwa mipango mikubwa ya huduma za kijamii inayotekelezwa barani Afrika.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Mwanza Bwana John Mongela amewataka walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kuendelea kuzitumia vizuri fedha na huduma nyingine wanazopata kupitia TASAF ili kupambana na umaskini.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bwana Ladislaus Mwamanga ameishukuru serikali ya Ireland kwa kutambua jitihada za kupambana na umaskini na kuahidi kuwa Mfuko huo utaendelea kuzingatia maelekezo ya serikali ya Tanzania katika kuboresha huduma kwa kaya za walengwa wa Mpango huo zipatazo milioni 1.1 nchini kote.

No comments:

Post a Comment