Wednesday, October 18, 2017

UKARABATI UWANJA WA NDEGE KIA KUKAMILIKA DESEMBA.


Serikali imesema ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu ambapo kwa sasa umefika zaidi ya asilimia Tisini. 

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mheshimiwa Elius Kwandikwa, mara baada ya kukagua ukarabati wa jengo la kupumzikia abiria na upanuzi wa maegesho ya ndege katika uwanja huo leo mkoani Kilimanjaro.

"Nimeridhishwa na ukarabati unaoendelea katika uwanja huu na nafikiri mmejionea wenyewe kazi inaendelea vizuri, hivyo naamini kutokana na hali hii kazi itakamilika hivi karibuni, amesema Naibu Waziri Kwandikwa.

Aidha, Naibu Waziri huyo amefafanua kuwa ukarabati huo ambao pia umehusisha maboresho ya mfumo wa maji taka unalenga kuleta tija kwa mkoa huo na Taifa kwa ujumla kutokana na kuwepo ongezeko la abiria, huduma za kijamii na kibiashara.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kukarabati na kujenga viwanja vya ndege nchini ili kurahisisha huduma za usafiri wa anga kwa wananchi wake lengo likiwa ni kuchochea fursa za kiuchumi ambazo zitasaidia kulipeleka Taifa katika uchumi wa kati.

Kwa upande wake, Meneja Miradi wa KIA, Mhandisi Mathew Ndossi, amesema kuwa maegesho yatakapokamilika yatakuwa na uwezo wa kuegesha jumla ya ndege kubwa 11 kwa wakati mmoja badala ya 6 zinazoegeshwa sasa.

Ameongeza kuwa abiria wanatarajiwa kuongezeka kutoka laki nane kwa mwaka hadi kufikia milioni moja na laki mbili mara baada ya kukamilika kwa uwanja huo.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kwandikwa amekagua barabara ya Sakina - Tengeru (km 14.1) na barabara ya mchepuko ya Arusha (Arusha Bypass km 42.4) ambapo amesema kuwa kukamilika kwa barabara ya Sakina - Tengeru ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa mkoa wa Arusha na wageni wanaoingia katika mkoa huo kwani kumepelekea kupungua kwa ajali na msongamano wa magari katika eneo hilo.

Ametoa wito kwa wananchi kuzitunza barabara na kutunza mazingira yanayozunguka barabara hizo ili ziweze kudumu kwa muda mrefu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Arusha Mhandisi, Johny Kalupale, amemhakikishia Naibu Waziri huyo kufanya kazi kwa ubora na kwa weledi ili kutimiza malengo ya Serikali ya kuwajengea wananchi miundombinu bora na ya kisasa.

Awamu ya pili ya mradi huo sehemu ya barabara ya mchepuo ya Arusha (Arusha Bypass), inayofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), inatarajiwa kukamilika mwakani na kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 67.

Naibu Waziri Kwandikwa amemaliza ziara ya kikazi katika mkoa wa Kilimanjaro na Arusha ambapo amekagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara yake.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. 
Meneja Miradi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Mhandisi Mathew Ndossi, akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mheshimiwa Elius Kwandikwa (Mb), (Kushoto), upanuzi wa maegesho ya ndege uliofanyika uwanjani hapo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mheshimiwa Elius Kwandikwa (Mb), akikagua maboresho ya mfumo wa majitaka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), alipofika uwanjani hapo kujionea hatua zilizofikiwa za ukarabati wa uwanja huo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mheshimiwa Elius Kwandikwa (Kulia), akitoa maelekezo kwa Meneja Miradi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Mhandisi Mathew Ndossi (Katikati), alipofika uwanjani hapo kujionea hatua zilizofikiwa za ukarabati wa uwanja huo.
Mafundi wakiendelea na ukarabati katika jengo la abiria la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA). Ukarabati huo umefika zaidi ya asilimia Tisini na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mheshimiwa Elius Kwandikwa,akifafanua jambo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoani Arusha, Mhandisi Johny Kalupale, alipokagua barabara ya Sakina – Tengeru (KM 14.1) na Barabara ya Mchepuko ya Arusha (Arusha Bypass KM 42.4) mkoani Arusha.
Muonekano wa Barabara ya Sakina – Tengeru (KM 14.1), mkoani Arusha,ambayo imekamilika kwa kiwango cha lami. Kukamilika kwake kumesaidia kupunguza ajali na msongamano katika eneo hilo.
Muonekano wa Daraja la Nduruma lililopo katika barabara ya Sakina – Tengeru (KM 14.1), mkoani Arusha.

No comments:

Post a Comment