Thursday, March 29, 2012

VIONGOZI WA NCHI ZA KIARABU WAKUTANA NCHINI IRAQ



Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa pamoja na viongozi kadhaa wa Mataifa ya Kiarabu wamewasili nchini Iraq kwa mkutano wa kilele wa Jumuia ya nchi za Kiarabu.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu 9,000 wameuawa nchini Syria katika kipindi cha mwaka mmoja wa ghasia na kumekuwepo miito kutoka katika Mataifa ya Kiarabu yakitaka hatua za moja kwa moja dhidi ya serikali ya nchi hiyo.

Viongozi wengine wakiwemo wa nchi jirani na Syria, kama Lebanon na Iraq wana wasiwasi juu ya nini kitafuata ikiwa utawala wa Bashar al Assad utapinduliwa. Kwa hiyo wameomba tahadhari ifanywe na kusema kuwa pasiwepo uingiliaji wa Mataifa ya kigeni nchini Syria.

Suala hili huenda lisipatiwe ufumbuzi mjini Baghdad, hususan wakati viongozi kadhaa kutoka Mataifa ya Ghuba na wa Wasunni wakiwa hawapo.Wasiwasi umetanda katika eneo zima. Iraq eneo ambalo bado linajikwamua kutoka katika muongo mzima wa mgogoro huku kukiwa na hali ya tahadhari mjini Bagdad.

Wakati Mkutano wa viongozi wa Kiarabu ukianza majira ya adhuhuri zilitoka taarifa za milipuko miwili karibu na eneo moja la mji linalojulikana kama la kimataifa ambalo haliko mbali na majengo ambako Mkutano unaffanyika.

No comments:

Post a Comment