CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM), kina siri nzito kuhusu mapendekezo yake katika
mchakato wa mabadiliko ya Katiba, huku kikiwekeza nguvu za makada wake
katika mambo ambayo hakitaki yawe sehemu ya mjadala huo, imebainika. Siri hiyo imo katika waraka maalumu wa siri unaowapa mwongozo viongozi na wanachama wake wa jinsi ya kusimamia maslahi ya yake katika mchakato wa kupatikana kwa Katiba Mpya. Mambo ambayo hayagusi misingi mikuu ya taifa na sera za msingi za CCM, bali masuala ya uendeshaji wa Serikali hayakuwekewa msimamo wowote na chama hicho katika waraka huo na kwamba ni ruhusa kwa viongozi na wanachama wake kutoa maoni kadri watakavyoona inafaa. Muhtasari wa mwongozo huo ni ule uliopitishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM ambayo ilihitimisha kikao chake takriban wiki mbili zilizopita mjini Dodoma na kupendekeza mambo kadhaa ambayo kingependa yawemo au yasiwemo katika Katiba Mpya. Waraka huo ambao gazeti hili limefanikiwa kuuona unaweka bayana sababu za kukataliwa kwa baadhi ya mambo, kupendekezwa kwa mambo mapya na kuachwa kama yalivyo baadhi ya masuala katika katiba ya sasa. Waraka huo umeeleza kuwa mambo ya msingi lazima yaendelee kubaki kama yalivyo katika Katiba Mpya na yanatakiwa kutetewa na kila kiongozi na mwanachama wa CCM. Umeeleza kwamba CCM ni mdau katika mchakato wa uundwaji wa Katiba Mpya kwa kuwa ni chama kinachoongoza Serikali iliyoko madarakani, chenye mtandao mpana na kwamba kingependa kuona viongozi wake wanashiriki katika mchakato huo ili kulinda na kuendeleza mazuri yaliyopo katika katiba ya sasa. “Wanatakiwa kuwa na uelewa wa mambo muhimu ambayo CCM kingependa kuyawekea msimamo ili waweze kupata fursa ya kuyatetea wakati wa kutoa michango yao katika mjadala wa Katiba Mpya kwa maslahi ya nchi yetu,” ilieleza sehemu ya waraka huo. Masuala muhimu Licha ya kutoweka msimamo wowote juu ya utaratibu wa jinsi ya kupatikana kwa Rais, CCM katika waraka huo kinaonekana kuwa na msimamo wa kutaka Rais achaguliwe kwa wingi wa kura (simple majority), tofauti na mapendekezo ambayo yamekuwa yakitaka kuwapo kwa ushindi wa asilimia zaidi ya 50 ya kura halali. Chama hicho tawala kinasema si kweli kwamba mshindi anayepata kura chache anakuwa amekataliwa na wananchi kwani taratibu za kidemokrasia zinatoa fursa kwa wagombea wengine kupigiwa kura. “Ukweli ni kwamba kwa sababu wagombea walikuwa ni zaidi ya mmoja, basi wapiga kura huwa wameamua kutumia haki yao kwa kuchagua mgombea wanayemuona anafaa zaidi,” inaeleza sehemu ya waraka huo. Sababu nyingine kinasema Tanzania ni nchi maskini hivyo ikiwa kutakuwa na duru mbili za uchaguzi baada ya kushindwa kupatikana kwa mshindi katika dura ya kwanza, nchi haiwezi kumudu gharama za awamu ya pili ya uchaguzi huo. Jambo jingine ambalo limechambuliwa kwa kina ni sababu za kutaka kuendelea kuwamo kwa muundo wa Serikali mbili na kwamba uzoefu katika nchi nyingi za Afrika unathibitisha kushindwa kwa mifumo ya Serikali tatu na ule wa Serikali ya shirikisho (federation). “Muundo uliopo sasa wa Serikali mbili siyo kwamba tu umezingatia mapatano ya Muungano ya mwaka 1964, bali pia hauhitaji gharama kubwa za uendeshaji ikilinganishwa na ule wa Serikali tatu,” unasema waraka huo na kuongeza: “Ziko nchi nyingine zilizowahi kuanzisha muungano (mifano ni Sene – Gambia na Misri na Syria) lakini miungano hiyo haikufanikiwa kwanza kwa kutobuni muundo mwafaka wa Serikali.” Chama hicho pia kwa maoni yake, kinadhani kwamba iwepo fursa ya kujadiliwa kwa suala la uwezekano wa Waziri Mkuu kutoka nje ya wabunge wa kuchaguliwa tofauti na sasa ambapo lazima atoke miongoni mwa wabunge wa majimbo. Hata hivyo, CCM kinaonekana kukataa mawazo yanayolenga kuwazuia wabunge wasiwe mawaziri kwa maelezo kwamba utaratibu huo umekuwa chachu kati ya mihimili ya Bunge na Serikali. “Wapo baadhi ya watu wanaopinga utaratibu huu kwamba baadhi ya mawaziri hutumia nyadhifa zao kupendelea majimbo wanakotoka, hususan katika masuala ya maendeleo,” inasomeka sehemu ya waraka huo na kuongeza: “Madai yanayotaka utaratibu huu ubadilishwe hayana msingi kwani kwa namna yoyote ile haiwezekani kumpata waziri au naibu waziri ambaye hatakuwa na eneo anakotoka.” Hoja nyingine ni kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba changamoto zilizopo kuhusu muungano huo zinajadilika na kutatulika. Umeeleza kwamba Jamhuri hiyo ilianzishwa kwa hiari na makubaliano ya waasisi wa pande mbili na kwamba zilifuatwa taratibu zote za kisheria zilizojikita zaidi kutazama faida za kiuchumi, kibiashara na kijamii, maingiliano ya watu wa pande hizo mbili imeimarisha undugu, umoja na mshikamano. “Muungano siyo tu ulizikutanisha nchi huru, bali uliziunganisha Jamhuri ya Tanganyika na Zanzibar chini ya mapatano ya Muungano (Article of Union) yaliyotiwa saini Aprili 22, 1964 na kutambulika kwa mujibu wa sheria za kimataifa,” inaeleza sehemu ya mwongozo huo. Jinsi ya kushiriki Katika mwongozo huo licha ya kuwataka viongozi na wanachama hao kushiriki mjadala wa Katiba ikiwa ni pamoja na kuzielewa Katiba ya Jamhuri ya Muungano na ya Zanzibar, pia unalenga kuwaelimisha masuala muhimu ya kuzingatiwa ili wafahamu vizuri wajibu wao wa kutoa maoni katika tume iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete. CCM kimeweka mkakati wa kufikisha ujumbe huo kwa wanachama wake kama moja ya njia za kujenga mtandao utakaoshawishi kuzingatiwa kwa misimamo yake hiyo katika mchakato wa mabadiliko ya katiba. Mpango uliowekwa ni pamoja na kuteua baadhi ya wajumbe wa Nec kwenda mikoani ili kuufikisha ujumbe kwa viongozi wa mikoa husika na baadaye viongozi wa mikoa nao wajipange kuufikisha kwenye ngazi ya wilaya, jimbo, kata na matawi yao. Mwongozo huo wenye kurasa 22 unafafanua kwamba katika jukumu hilo, hilo wabunge, wawakilishi, madiwani na makada wengine wa CCM wawekwe mstari wa mbele katika kufanya kazi hiyo kwa kushirikiana na viongozi wa chama. |
Sunday, May 27, 2012
CCM wana siri nzito mabadiliko ya Katiba
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment