Tuesday, August 5, 2014

ASKARI POLISI FEKI WA USALAMA BARABARANI ALIYEKUWA ANATAPELI WANANCHI AKAMATWA JIJINI DAR ES SALAAM

Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam linamshikilia na kumhoji mtu mmoja aitwaye ROBSON S/O SEIF MWAKYUSA EMMANUEL, miaka 30, Mkazi wa Kijitonyama jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kujifanya afisa wa Polisi kikosi cha Usalama barabarani akiendelea na kazi za ukaguzi wa makosa ya usalama barabarani. Mtuhumiwa huyu alikamatwa tarehe 02/08/2014 huko Kata ya Chamazi, Mbagala Majimatitu Mkoa wa Kipolisi Temeke akiwa amevalia sare za Polisi na cheo cha Stesheni Sajenti.

Baada ya kukamatwa alikutwa na gari namba T723 BAK T/Cresta rangi nyeupe analilotumia kuzunguka maeneo mbalimbali ya jiji kutapeli watu akiwadanganya yeye ni askari polisi. Gari hilo lilipopekuliwa lilikutwa na
  • Radio Call 1yenye namba GP380 aina ya Motorola
  • Leseni za udereva zipatazo 40 za watu mbalimbali
  • Stakabadhi 02 za Serikali zenye nambari A0531562 na A1672464
  • Police Loss Report mbalimbali.
  • Nakala 03 za Notification zilizojazwa.
  • Kofia moja ya (Uhuru Cape) ya Usalama barabarani,
  • Beji 01 yenye jina la E.R. MWAKYUSA ya kuweka kifuani.
  • Ratiba ya mabasi yaendayo Mikoani ya SUMATRA
Pia mtuhumiwa alipekuliwa nyumbani kwake alikutwa na vitu vifuatavyo:
  • Pea 04 za sare ya Polisi ya KAKI.
  • Pea 03 za sare ya Polisi ya Usalama Barabarani
  • Koti 01 ya mvua ya Usalama Barabarani
  • Reflector 08 za Usalama Barabarani
  • Kofia 01 (Uhuru Cape) ya Usalama Barabarani
  • Kofia 02 (Barret) nyeusi za Polisi
  • Mikanda 02 ya Bendera mali ya Jeshi la Polisi
  • Mikanda 02 ya Polisi (Tunic Cross Belt) mweusi.
  • Mikanda 02 ya Filimbi.
  • Cheo 01 cha Sajenti
  • Vyeo 03 vya Stesheni Sajenti.
  • Vifungi 08 vya chuma mali ya Jeshi la Polisi.
  • Cheo 01 cha Stesheni Sajenti cha JWTZ
  • Notification Form zilizojazwa zipatazo 62.
  • PF3 Forms zipatazo 04
  • Notification Forms ambazo hazijajazwa zipatazo 08
Mtuhumiwa huyu aliwahi kuwa askari polisi aliyejiunga na Jeshi hilo Mwaka 2000 akiwa mwenye namba F2460 lakini alifukuzwa kazi kwa fedheha mnamo tarehe 21/03/2014 huko Kibaha Mkoani Pwani akiwa na cheo cha Stesheni Sajenti. 

Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mtuhumiwa huyu amekuwa akijitambulisha kuwa ni askari hivyo kufanikiwa kuwatapeli wananchi mbalimbali na kujipatia kiasi kikubwa fedha kwa njia za udanganyifu. Wananchi waliotapeliwa wanatakiwa kuja kutambua leseni zao ili sheria iweze kuchukua mkondo wake

S. H. KOVA,
KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM

No comments:

Post a Comment