Sunday, May 27, 2012

Fedha bado zakwaza rufani kesi MV Bukoba


 
SIKU chache baada ya kumbukumbu ya miaka 16 tangu kuzama kwa meli ya MV Bukoba, mahakama bado haijakamilisha vitabu vya kumbukumbu za mwenendo wa mashitaka (Records) za hukumu ya kesi namba 22/1998 ya watuhumiwa wanne walioshitakiwa kwa kusababisha ajali hiyo imebainika.

Hali hiyo imeelezwa kuwa inatokana na ukata kwa idara ya Mahakama kutokana na kupokea fedha za kawaida za uendeshaji wa ofisi tu hivyo kukosa kiasi cha Sh10 milioni kwa ajili ya kutayarishia vitabu mbalimbali vya mwenendo wa mashtaka kwa kipindi cha miaka 11 hivyo serikali kushindwa kuikatia rufani kesi hiyo.

Akizungumza na Mwananchi jana, Msajili wa Mahakama wa wilaya kanda ya Mwanza, Khalfan Isaya, alisema bado mahakama haijakamilisha vitabu hivyo kutokana na kukosa fedha hatua ambayo inakwamisha uamuzi wa serikali kukata rufaani kama ilivyokusidia.

“Kwa sasa tunapokea fedha za kawaida kwa ajili ya uendeshaji wa ofisi tu, tunajitahidi hivyo hivyo kutengeneza vitabu hivyo kila tunapoweza ka fedha hivyo, lakini unajua kwa kesi ya Mv Bukoba ambayo ilikuwa na vielelezo vingi, tunatakiwa kutengeneza vitabu zaidi ya 10 vyenye Volume mbalimbali,” alieleza Msajili huyo.

Kesi ya Mv Bukoba ilihukumiwa Novemba 29 mwaka 2002 na Jaji mfawidhi wa mahakama ya kanda ya Mwanza, Juxton Mlay na washtakiwa wa kesi hiyo akiwemo nahodha wa meli hiyo Jumanne Rume Mwiru (sasa ni marehemu baada ya kufariki mwaka 2009).

Wengine walikuwa ni Mkuu wa Bandari ya Kemondo, Prosper Lugumila, Mkuu wa Bandari ya Bukoba Alfred Sambo, ambaye pia ni marehemu aliyefariki muda mfupi baada ya kesi hiyo kuanza pamoja na Mkaguzi wa Mamlaka ya Bandari (THA), Gilbert Mokiwa.

Hukumu ya kurasa 118 zilizoandikwa kwa mkono ilisomwa kwa zaidi ya dakika 160 na katika kesi hiyo upande wa mashitaka ulikuwa ukisimamia na wakili wa serikali Eliezer Feleshi (sasa Mkurugenzi wa Mashtaka - DPP) na huku upande wa utetezi ukisimamiwa na wakili Magongo.

Meli hiyo ya MV Bukoba ilipinduka na kuzama katika Ziwa Victoria, Jumanne alfajiri Mei 21, 1996 na kusababisha zaidi  ya watu 800 kupoteza maisha.

Meli hiyo ilizama ikiwa imebakisha umbali wa maili moja na nusu kabla ya kutia nanga katika bandari ya Mwanza Kaskazini, ikiwa jirani kabisa na ufukwe wa Shule ya Sekondari Bwiru, ambako sasa kumejengwa mnara wa kumbukumbu ya kumbukumbu ya waliopoteza maisha katika ajali hiyo.

Kukwama kwa rufani
Isaya alisema mahakama yake imekwisha toa nakala ya hukumu ya kesi hiyo tangu Novemba 29, 2010 lakini alieleza kuwa bado vitabu vya kumbukumbu ya kesi hiyo ambavyo vinajumuisha nyaraka za mwenendo wa Mashitaka na hukumu vilikuwa havijatengenezwa.

Kesi hiyo inaweza kuingia katika historia kwa upande wa kesi kubwa hapa nchini kutokana na kuwa na nyaraka za vielelezo vingi zaidi hivyo kugharimu kiasi kikubwa cha fedha kuviandaa.

"..ukiangalia uamuzi wa mahakama ambao katika nakala ya mkono wakati ukisomwa na Jaji ulikuwa na kurasa 118 baada ya kuchapwa una kurasa 105, sasa unapoandaa record (mwenendo wa mashitaka) unatengeneza vitabu vitakavyokuwa na kumbukumbu zote za zinazoonyesha kuanzia hati ya mashitaka ilipofunguliwa, upelelezi wake, ushahidi ulivyotolewa hadi kufikia hukumu, bado itachukua muda sana kukamilika," alisema msajili huyo.


Alieleza kuwa kulingana na kesi hiyo kuwa na washitakiwa wanne mahakama italazimika kuandaa vitabu visivyopungua 10 vya kumbukumbu za mwenendo wote wa mashitaka na hukumu huku akibainisha kuwa vitabu hivyo ni kwa ajili ya majaji 3 wa mahakama ya rufani ambao watasikiliza rufani hiyo, nakala moja kwa msajili wa mahakama, moja nyingine kwa ajili ya wakili wa serikali, na nakala nyingine kwa washitakiwa wote wanne pamoja na wakili wa utetezi.

Akifafanua kuhusu gharama hiyo alisema kazi ya kuandaa vitabu hivyo vya kumbukumbu ni vinahitaji fedha kwa vile itailazimu mahakama kuzinakilisha na kisha kuzipiga chapa nakala zote za faili la kesi hiyo, na kutoa mfano wa vitabu vya kumbukumbu vya hukumu ya kesi hiyo ya mauaji, namba 24 ya mwaka 2009.

"Ukiangalia ushahidi tu wa kesi hii, unavilelelezo vingi sana, kuna taarifa za vifo vya watu waliokufa katika ajali hiyo, picha na nyaraka mbalimbali za meli, nadhani kutakuwa na volume 4 au zaidi ya vitabu vya ushahidi, sasa kwa vile mahakama inapata mgao kidogo wa fedha toka serikalini nadhani jambo hili litachukua muda kukamilika kama litawahi labda katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2011/2012, ikiwa mapema kabla ya hapo tutashukuru maana imekuwa kero kesi hii," alieleza msajili huyo.

No comments:

Post a Comment