Nida imesema katika taarifa yake iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Mkurugenzi Mkuu wake, Dickson Mwaimu, kwamba utaratibu wa ugawaji fomu utatangazwa kwa wananchi wakati utakapowadia, tena kupitia vyombo vya habari.
“Wananchi mnaombwa yeyote atakayebaini au kuwa na taarifa ya vitendo hivi, atoe taarifa kwenye kituo chochote cha Polisi kilicho karibu.
“Mamlaka inawasihi wananchi mikoani kuwa watulivu kipindi hiki, huku wakisubiri kuanza kwa usajili mikoani mwao na Nida itakuwa ikitoa taarifa za mara kwa mara kwa wananchi ili kujiandaa na usajili katika maeneo husika,” ilisema taarifa hiyo.
Zimekuwapo taarifa katika baadhi ya mikoa nchini kwamba fomu za usajili na utambuzi wa watu zenye lengo la kuchukua taarifa za wananchi na hatimaye kuwapatia kitambulisho cha Taifa, kuanza kuuzwa kinyume cha taratibu.
Kwa mujibu wa Maimu, vitendo hivyo vimebainika baada ya kupatikana taarifa kutoka kwa wasamaria walioshuhudia fomu hizo zikiuzwa kwa wananchi.
Alisema vitendo hivi vinalenga kuhadaa wananchi na hivyo kuwataka wawe waangalifu na kufichua wanaojihusisha na uuzaji huu, ambao ni kinyume cha taratibu, kanuni na sheria ya usajili.
“Nida haijaanza kutoa fomu zozote za usajili kwa wananchi wa mikoani, zaidi ya usajili kwa watumishi wa umma kwa Dar es Salaam na Zanzibar na kazi ya majaribio katika Wilaya ya Kilombero, Morogoro, lililofanyika Machi.
“Usajili rasmi wa wananchi unakusudia kuanza Juni kwa kuanzia na Mkoa wa Dar es Salaam,” ilieleza Nida.
No comments:
Post a Comment