MBUNGE
wa jimbo la Rombo Joseph Selasini, aliyepata ajali na kupoteza
wanafamilia wanne juzi jioni, amelalamikia kukithiri kwa bidhaa feki,
akisema kuwa ndio chanzo cha ajali hiyo. Akizungumza katika Hospitali ya KCMC alikolazwa, Selasini alisema kwamba chanzo cha ajali hiyo ni kupasuka kwa tairi ya mbele, suala ambalo linamshangaza kwa kuwa alibadilisha tairi zote na kuweka mpya siku tatu kabla ya ajali hiyo na hakuwahi kufanya safari yoyote ndefu zaidi ya kiyo ya kwenda Arusha na kurejea Moshi. Aliitaka Serikali kufanya ukaguzi kupitia Shirika la Viwango nchini (TBS) kufanya uhakiki wa bidhaa zinazoingia nchini kutoka nje ya nchi kwani nyingi hazina viwango na zinasababisha madhara kwa wananchi. Hata hivyo, hali ya Selasini aliyepata ajali hiyo katika eneo la chuo cha ufundi Bomang’ombe wilayani Hai, Kilimanjaro, barabara kuu ya Moshi-Arusha imeelezwa kuwa inaendelea vizuri. Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kamanda wa polisi mkoani hapa, Absalom Mwakyoma ilieleza kuwa hali ya mbunge huyo kwa sasa inaendelea vizuri na kuwa aliteguka bega la mkono wa kulia. Hata hivyo, hali ya mke wa mbunge huyo, Digna Kavishe (43) imeelezwa kuwa ni mbaya kutokana na majeraha aliyoyapata kichwani. Kwa mujibu wa kamanda, katika ajali hiyo watu wanne walifariki dunia ambapo watatu kati yao walifariki papo hapo na mmoja alifariki wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya KCMC. Kamanda aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni Catherin Roman Selasin (80) mkazi wa Rombo, Agatha Jerome (85) mkazi wa Rombo na wanawake wawili ambao mpaka sasa hawajatambuliwa majina yao na wote walikua abiria katika gari la mbunge huyo. Kwa mujibu wa kamanda, chanzo cha ajali hiyo bado kinachunguzwa licha ya uchunguzi wa awali kuonyesha kuwa ajali hiyo ilisababishwa na kupasuka kwa tairi ya mbele upande wa kulia baada ya kuingiliwa na pikipiki mbele na hivyo kukosa mwelekeo na kupinduka. Alisema sababu nyingine inaonyesha kuwa mbunge huyo alikuwa katika mwendo kasi hali iliyomfanya ashindwe kumudu gari na hivyo kupoteza mwelekeo na kuwa miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya KCMC. |
Sunday, May 27, 2012
AJALI YA MBUNGE YAHUSISHWA NA BIDHAA FEKI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment