KATIBU
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dk Wilbrod Slaa
amesema vitendo vya ufisadi, ubinafsi, kutowajibika na kukosa uzalendo
vimekuwa ni kielelezo cha taifa machoni pa watanzania na wageni
wanaokuja kutembelea nchini. Slaa alisema kuwa inashangaza kuona mashirika muhimu ya umma katika taifa yenye dhamana ya kutoa huduma kwa jamii yakiwa katika hali mbaya kiutendaji na kushindwa kutoa huduma hizo kwa ufanisi jambo ambalo hutoa sifa mbaya kwa taifa. Alieleza hayo akichangia mada kwenye mtandao wa Twitter juzi iliyosema kuwa ‘Utajuaje kama upo Tanzania’ iliyolenga kuwapa fursa watu mbalimbali kubainisha vielelezo vizuri kwa maana ya mafanikio na vibaya kwa maana ya kasoro vinavyomfanya mtu ajue yupo Tanzania. Akitolea mfano vielelezo cha madudu nchini Slaa alisema kuwa “kielelezo cha kuwa upo Tanzania ni pale unapoona Shirika la Mawasiliano, TTCL likiwa katika hali mbaya na kushindwa kuonyesha ufanisi wake, huwezi kujua limekufa, linaumwa au liko hai”. Slaa alisema mbali na TTCL, kielelezo cha madudu nchini pia ni kuona wanasiasa wakichochea udini na ukabila majukwaani wakati misingi ya nchi inahimiza watu kuishi kwa amani na upendo bila kuulizana wala kubaguana kidini, kikabila wala rangi. Katika maoni yake alishangaa kuona Rais wa nchi anashindwa kujua kwanini nchi yake ni masikini huku akisikitishwa na kuona wanafunzi wasiojua kusoma wala kuandika wakifaulu kuingia sekondari. Aliwaponda watu wanaotumia muda mwingi kushangilia na kutamba mitaani baada ya timu za ligi za ulaya kushinda katika mechi zake wakishindwa kushangilia timu za nyumbani na hata kujali maendeleo ya nchi yao. “Utajua kuwa upo Tanzania endapo utaona Serikali inawaita wezi ‘wajanja wachache’ wanaoliibia taifa au wanasiasa wachache wakitumia muda mwingi mahakamani badala ya kuwatumikia wapiga kura wao,” alisema Slaa. Alisema mbali na changamoto hizo pia hapendezwi na askari wa usalama barabarani wanaoongea na simu katika vituo vyao vya kazi huku magari yakiwa yamekwama kwenye foleni jambo ambalo ni kielelezo tosha kinachoweza kumfanya mtu yeyote hata kama ni mgeni atambue kuwa yupo Tanzania aliyoiita ya ‘wajanja’. Mada hiyo ilichangiwa na watu wengi wakiwemo wanamuziki, wananchi na watu maarufu ambao kila mmoja alitoa dukuduku lake moyoni juu ya vielelezo vya Tanzania machoni pa watanzania wenyewe na wageni. |
Sunday, May 27, 2012
UFISADI KIELEZO CHA TAIFA LETU
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment