Tuesday, May 22, 2012

HALI YAENDELEA KUWA TETE RUFIJI



Mkazi wa Mtaa wa Chemchem Kata ya Igawilo ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Oscar Mbalamwezi (47) akiwa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya baada ya kujeruhiwa kwa kupigwa na nondo juzi majira ya saa 7 usiku wakati akitoka kuangalia mpira.
Vurugu kubwa zinazodaiwa kusababisha vifo vya watu wawili, wengine kujeruhiwa kwa risasi, maduka na nyumba kadhaa, ikiwamo inayotumiwa na Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) na Mkuu wa Kituo cha Polisi (OCS) kuchomwa moto, zimetokea mjini Ikwiriri, Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani, baada ya mkulima kuuawa na watu wa jamii ya wafugaji kwa kipigo. 
Kati ya wanaodaiwa kuuawa katika vurugu hizo, ni pamoja na daktari wa mifugo wa mjini humo, ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ernest Mangu, na Mkuu wa Mkoa huo, Mwantumu Mahiza, kwa nyakati tofauti jana walisema hakuna vifo vipya katika vurugu hizo mbali ya mkulima mmoja ambaye aliuawa juzi.
Kamanda Mangu alisema mtu aliyethibitika kuuawa ni mkulima wa kijiji cha Nyambere, ambaye alikufa kutokana na kushambuliwa na wafugaji Jumamosi kufuatia ugomvi uliosababishwa na wafugaji kulisha mifugo katika shamba lake.
Mangu alisema wanalichukulia tukio hilo kama la kawaida na siyo mapigano baina ya wakulima na wafugaji kama inavyodaiwa. Kauli kama hiyo pia ilitolewa na Mahiza akizungumza na NIPASHE kwa simu akiwa Ikwiriri jana saa 11 jioni.
“Hakuna mapigano ya wafugaji na wakulima, bali ni vijana wa Ikwiriri ndio waliofunga barabara mabasi yasipite. Subirini tutatoa taarifa baada ya kuelezwa na Kamanda wa Polisi,” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Wakati viongozi hao wakitoa msimamo huo, askari polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), walifanya kazi ya ziada kwa zaidi ya saa nne kutumia mabomu ya machozi kutawanya makundi ya wananchi wenye hasira walioungana na baadhi ya wakulima wilayani humo kupambana na wafugaji mjini Ikwiriri.
Askari hao waliingia mtaani kupambana na makundi hayo baada ya nyumba kadhaa kuchomwa moto, ikiwamo ya OCD na OCS Ikwiriri, pamoja na mfanyabiashara mmoja wa mjini Ikwiriri anayedaiwa kushirikiana na wafugaji.
Nyumba hiyo ya biashara ni kituo cha kukusanya maziwa mjini humo iliyokuwa ikiendelea kujengwa.
Awali, NIPASHE ilizungumza na baadhi ya mashuhuda wa kadhia hiyo na ambao walidai kuwa kuna watu wawili, akiwamo daktari wa mifugo, waliuawa na mmoja wa viongozi wa watu wa jamii ya wafugaji katika vurugu hizo.

Pia kuna taarifa za kujeruhiwa kwa risasi mwananchi mmoja. Mkuu wa Mkoa amekanusha kuwapo kwa matukio hayo, akisema: “Hatujaona maiti yoyote.”
Habari zaidi zinasema kumekuwapo na mfululizo wa mauaji ya wakulima yanayofanywa na wafugaji huku polisi wakituhumiwa kuwalinda kwa sababu wanapewa kitu kidogo.
Raia mmoja aliyezungumza na NIPASHE alidai kuwa wafugaji hao wamekuwa wakichanga fedha kila mwezi na kuwapa polisi ili kufumbia macho udhalimu wanaowafanyia wakulima.
Kamanda  Mangu alipoulizwa juu ya tuhuma hizo, alikanusha akisema hazina ukweli.
Alisema wakulima wanapokwenda kituoni kuwalalamikia wafugaji, baadaye huwa wa kwanza kurudi kituoni kwenda kufuta kesi wakidai kwamba, tayari wamekwishalipwa fidia.
Mangu alisema kama tuhuma hizo zingekuwa za kweli, zingekuwa zimekwishafikishwa kwa viongozi wa juu wa polisi, kama OCD, Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC), lakini hakuna hata siku moja tuhuma hizo zilifikishwa kwa viongozi hao.
Alisema watu wanaotoa tuhuma hizo, wana ajenda zao, kwani mpaka sasa ni mara tatu kwa mwaka huu vijana hao wamefanya matukio hayo, mojawapo likiwa lile la kuwakataa walimu wa Shule za Sekondari za Ikwiriri na Muhoro.

Hata hivyo, alisema wanafanyia kazi suala hilo kujua sababu za wananchi hao kuwakataa watumishi hao wa umma.
“Ugomvi uliopo ni polisi wanapowazuia kufanya matakwa yao,” alisema Kamanda Mangu.
Alisema katika vurugu za jana, nyumba kadhaa, ikiwamo ya OCD na ofisa mmoja wa polisi ambaye hakutaja cheo chake, pamoja na za wafanyabishara zilichomwa moto.

Baadhi ya watu walioshuhudia, waliliambia NIPASHE kwa njia ya simu kutoka mjini Ikwiriri jana kuwa vurugu hizo zilianzishwa na wananchi hao, wengi wao wakiwa ni vijana kwa lengo la kulipiza kisasi cha kuuawa mkulima huyo juzi.
Aliyeuawa juzi, amefahamika kwa jina moja la Mtowangala, ambaye ni mkulima wa Kijiji cha Nyambere, wilayani humo.
Hadi tunakwenda mitamboni jana jioni, vurugu zilikuwa zikiendelea na karibu mji wote wa Ikwiriri uliripotiwa kuwa ulikuwa umetawaliwa na milindimo ya risasi   na mabomu ya machozi na kusababisha hofu na tafrani kubwa miongoni mwa wakazi mjini humo.
Risasi na mabomu hayo yalikuwa yakirushwa na askari wa FFU kutoka mjini Kibaha, mkoani Pwani na Ukonga jijini Dar es Salaam kutuliza vurugu hizo.
Kwa mujibu wa mashuhuda hao, vurugu hizo zilisababisha karibu shughuli zote, zikiwamo za biashara, usafiri na usafirishaji kusimama kwa zaidi ya saa nne baada ya vijana hao kufunga barabara.
Aidha, mkutano wa hadhara uliokuwa umeandaliwa na Mbunge wa Rufiji (CCM), ambaye pia ni Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Suleiman Rashid, ulishindikana kufanyika jana kutokana na vurugu hizo.
Shuhuda mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Rwanda Ali Rwanda, alisema kufuatia mauaji ya mkulima huyo, baadhi ya wananchi walitoa taarifa kituo cha polisi na askari polisi walikwenda kijijini humo na kuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka mjini Ikwiriri.
Rwanda alisema vurugu hizo zilianza saa 7 mchana jana wakati wa shughuli za mazishi ya marehemu zikifanyika.
Alisema wananchi hao walianza kuvamia maduka na nyumba za wafugaji pamoja na za viongozi hao wa polisi na kuzichoma moto.
Rwanda alisema kabla ya wananchi hao kuchoma moto maduka na nyumba hizo, walikwenda katika kituo cha polisi mjini Ikwiri kulalamikia vitendo vya wafugaji kuendelea kuua wakulima, huku wauaji wakiachwa bila kuchukuliwa hatua zozote.
Alisema wananchi hao walidai kuwa mkulima aliyeuawa juzi alikuwa anatimiza idadi ya wakulima wanne waliokwishauawa na wafugaji tangu mwaka jana.
Alisema kutokana na matukio hayo, wananchi hao walidai kuwa wameshindwa kuvumilia kuona hali hiyo ikiendelea.
Mmoja wa wakulima waliouawa mwaka jana alitajwa kuwa ni Abdulrahmani Mtibo na kudaiwa kuwa hali hiyo imekuwa ikichangiwa na baadhi ya wafugaji.
“Baadhi ya askari polisi wamekuwa wakipelekewa Sh. milioni 6 kila mwezi na wafugaji,” alidai mmoja wa wananchi aliyezungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana.
Awali, akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu akiwa njiani kwenda mjini Ikwiriri jana, Kamanda Mangu alisema taarifa za awali alizokuwa nazo muda huo, zinaeleza kuwa vurugu hizo zilitokea baada ya wafugaji kuingiza mifugo yao kwenye shamba la mkulima huyo.
Alisema kutokana na kitendo hicho, ulizuka mzozo kati ya mkulima huyo na wafugaji hao ambao haukuwafikisha katika maelewano.
“Ndipo purukushani ikatokea na mkulima kufariki,” alisema Kamanda Mangu.
Alisema kutokana na kifo hicho, wakulima hawakukubali na hivyo, wakaamua kufunga barabara na kuanzisha vurugu hizo.

Hata hivyo, baada ya kufika Ikwiriri, Kamanda Mangu aliliambia NIPASHE kwa njia ya simu kuwa kufikia jana saa 11 jioni barabara iliyokuwa imefungwa na vijana hao ilikuwa imefunguliwa na hivyo kuruhusu magari kuendelea na safari zake.
Hata hivyo, alisema pamoja na barabara hiyo kufunguliwa, vijana hao waliendelea kubaki kwenye makundi wakijadili matukio yaliyotokea.


 

No comments:

Post a Comment