Tuesday, May 29, 2012

MKURUGENZI JIJINI MWANZA APANDISHWA KIZIMBANI ARUSHA

MKURUGENZI wa jiji la Mwanza,Willson Kabwe juzi alipanda kizimbani katika mahakama ya mwanzo Maromboso jijini Arusha,kutoa utetezi juu ya madai ya kutaka kupora mali za marehemu mdogo wake,John Mkenga aliyefariki hivi karibuni kwa ajali ya gari na kuacha mke na watoto wanane.

Kesi hiyo ya mirathi namba 42 ya 2012 inasikilizwa na hakimu Mwanaidi Lemmy wa  mahakama ya mwanzo,ambapo Kabwe anapinga mke wa marehemu,Blandina Mkenga kuwa msimamizi wa mali za marehemu mumewe na kudai kuwa hana sifa za kisheria .
Akitoa utetezi huo mbele ya hakimu Lemmy,Kabwe alidai kuwa kikao cha ukoo kilichofanyika februari 14 mwaka huu kilimpitisha kama msimamizi mkuu wa mali za marehemu.

Upande wa mjibu maombi ambaye ni mke wa marehemu, Blandina Mkenga anadai kuwa hoja ya Kabwe haina msingi kwani kikao kilichofanyika  kumteua Kabwe kuwa msimamizi wa mirathi  ni cha kimila na kililenga kumkandamiza mwanamke kusimamia mali za marehemu mumewe.

''kama wewe unauchungu na familia ya marehemu mdogo wako umewahi kufika mara ngapi hapa nyumbani kuijulia hali familia na unajua tunaishije,ivi unahabari kwamba hadi sasa watoto hawaendi shule kwa kukosa ada''alisema na kuongeza.

''kwanini unathamini zaidi mali za marehemu kuliko familia na watoto wameachwa bila msaada huku wewe ukidai umeteuliwa kusimamia mali za marehemu''alisema Blandina baada ya hakimu Lermmy kumpa idhini ya  kumuuliza swali  Kabwe ambaye ni shemeji yake

Alizidi kuieleza mahakama kwamba ,Kabwe na wenzeke akiwemo kaka yao mkubwa,Jacob Mkenga wanalengo la kupora mali za marehemu kwa kutumia mgongo wa kimila ,hivyo aliiomba mahakama itengue maamuzi hayo na kumpitisha yeye kuwa ndiye msimamizi halali wa mali za Mumewe.

Shahidi wa upande wa mjibu maombi,Elitabu Mkenga ambaye ni mdogo wa marehemu alimtaka kaka yake, Kabwe kuacha ubinafsi na kudai kwamba analengo la kutaka kupora mali za mdogo wake kwani alishazoea kufanya ufisadi kwenye halmashauri.

‘’ivi wewe hujatosheka na ufisadi unaoufanya huko Mwanza unataka pia kufanya ufisadi kwenye mali za marehemu mbona mimi ni mdogo wa marehemu sipiganii mali hiyo kwani mimi sihitaji mali, najua ni mali za watoto sasa wewe unachotaka nini’’alimuuliza swali Kabwe

Hatua hiyo ilichafua hali ya hewa mahakamani hapo ambapo wanandugu hao walianza kushambuliana kwa maneno makali huku kabwe akimweleza mdogo wake kwamba anampango wa kumridhi mke wa marehemu kwani amehama nyumbani kwake na kuhamia kwenye familia ya marehemu.

Malumbano hayo yalizimwa na hakimu Lemmy baada ya kuwataka wasizungumzia masuala ya nyumbani kwao  mahakamani hapo kwani hayana msaada wowote katika kesi hiyo.

‘’unajua mimi nawashangaa sana mnapoleta malumbano ya masuala ya nyumbani kwenu  hapa mahakamani , hayo mambo ya familia yenu hatuyahitaji katika kesi hii,tafadhili nendeni kwenye kesi ya msingi iliyotuileta hapa’’alisisitiza hakimu Lemmy.

Akisisitiza mahakamani hapo Kabwe aliieleza mahakama kwamba anataka imwidhinishe kuwa msimamizi halali wa mali za marehemu ili aweze kudhibiti mali hizo  zisiporwe kwani tayari anaoushahidi wa wazi kwamba siku chache baada ya marehemu kufariki ndugu wa upande wa mke wa marehemu walimiminika kwenye mgodi wa marehemu na kupora madini ya Tanzanite yenye thamani kubwa.

‘’mheshimiwa hakimu ninao ushahidi wa wazi kabisa kwamba siku chache tu baada ya marehemu kufariki ndugu wa upande wa mke wa marehemu walivamia mgodi wa madini uliopo Mererani na kupora kiasi kikubwa cha madini’’alisema Kabwe
Hata hivyo hakimu Lemmy alimtaka Kabwe kuleta hoja hiyo baada ya kumalizika kwa kesi ya msingi iliyofunguliwa kwani hoja hiyo haihusiani katika kesi hiyo ya msingi inayoendelea hapo mahakamani.
Hakimu Lemmy alimtaka Kabwe kuzitaja mali zilizoachwa na marehemu mdogo wake kwa ujumla  ,ambapo Kabwe alizitaja kuwa ni pamoja na mgodi wa madini ya Tanzanite,Kiwanda cha kutengeneza nafaka ya binadamu na mifugo.

Mali zingine ni Godauni makubwa 7 yaliyopo Kisongo jijini Arusha,migodi ya madini ya dhahabu iliyopo mkoani Tanga,Nyumba za kuishi zilizopo maeneo tofauti nje ,viwanja vya kuendeleza ,magari ,Fedha zilizopo Benki tofauti na mali zingine alizodai hazifahamu.

Mara baada ya utetezi wa pande zote wakiwemo mashahidi ,hakimu Lemmy aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 22 mwaka huu, itakapotole hukumu na kuzitaka pande zote kuhakikisha zinafika mahakamani hapo.

Awali  Kabwe akishirikiana na ndugu wengine walileta pingamizi mahakamani la kutaka mahakama isitishe taratibu za mirathi  kwa madai kuwa mke wa marehemu hana mamlaka ya kusimamia mirathi.

Baada ya hatua hiyo,Kabwe alipeleka barua ya pingamizi kwa hakimu wa mahakama hiyo,Mwanaidi Lemmy ya tarehe 12/4/2012 ya kutaka shauri la mirathi namba 42/2012 lililofunguliwa na mke wa marehemu,kusitishwa mchakato wote wa kuendelea kusikiliza shauri hilo.

Katika barua hiyo Kabwe alitoa sababu sita na moja ya sababu ni kuitaka mahakama hiyo isitishe kuwasikiliza kwani yeye hakuwa na taarifa rasmi kwani yeye ndiye mwenye mamlaka aliyeteuliwa kusimamia mirathi ya mdogo wake,kama ilivyoamuliwa na kikao cha ukoo kilichoketi Februal 14 mwaka huu na kwamba mke wa merehem,u hajawahi kuteuliwa kusimamia mirathi na ukoo.

No comments:

Post a Comment