Tatu anadaiwa kufanya kitendo hicho kwa madai kwamba mtoto huyo amekuwa akimsumbua kutokana na kujisaidia haja kubwa mara kwa mara na hivyo siku ya tukio alichoka na kuamua kumnyonga mtoto huyo ili kukomesha tabia yake.
Inadaiwa kuwa mara baada ya baba wa mtoto James Lushingo ambaye anafanya kazi ya kinyozi kuwasili nyumbani hakumuona mwanawe na alipomuuliza mkewe alimjibu kuwa mtoto huyo alikuwa amelala chumbani na shangazi yake ambaye ana ulemavu wa kutosikia (kiziwi).
Kwa mujibu wa majirani, James aliamua kwenda moja kwa moja katika nyumba aliyoambiwa amelala mwanae na kumkuta shangazi wa marehemu akiwa amelala peke yake bila mtoto hivyo alirudi tena kwa mkewe na kumhoji ambapo alitoa majibu ya kusita sita.
Hatua hiyo ilimfanya James kwenda kwa Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho kutoa taarifa na pia kuwafahamisha wanakijiji wengine ambao walianza kumsaka mtoto huyo hadi walipofanikiwa kukuta shimo katika kichaka eneo la jirani likiwa na dalili za kufukiwa kitu muda mfupi uliopita.
“Hivyo wanakijiji hao waliamua kulifukua shimo hilo lenye urefu wa futi mbili na nusu na kuona miguu na mikono ya mtoto huyo ikichomoza katika shimo hilo na kisha kumfukua mwili mzima na kumueleza baba mzazi wa merehemu kuwa akatoe taarifa katika Kituo cha Polisi,” alisema jirani ambaye hakuwa tayari kutajwa jina.
Alisema baadaye James alikwenda katika Kituo cha Polisi na kutoa taarifa huku akieleza kumshuku mkewe Tatu kutokana na maelezo yake ya awali ya kuwa na wasiwasi na kudanganya kuwa mtoto huyo alikuwa amelala na shangazi yake kwenye nyumba jirani na wanapoishi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Onesmo Lyanga jana alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwaeleza waandishi wa habari kuwa mtoto huyo alinyongwa na kufukiwa katika shimo la urefu wa futi mbili na nusu.
Alisema mtuhumiwa anashikiliwa na jeshi hilo kwa uchunguzi zaidi na kwamba upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani. Naye Fadhili Abdallah anaripoti kutoka Kigoma kuwa, jeshi la Polisi mkoani Kigoma linamtafuta mwanafunzi wa Shule ya sekondari Rwiche katika Halmashauri ya Wilaya Kigoma, Rehema Issa (22) ambaye alijifungua mtoto na kumtupa chooni jambo lililosababisha kifo cha mtoto huyo.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa Kigoma, Francis Mwakabana amesema hayo wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusiana na matukio mbalimbali yaliyotokea mjini Kigoma katika wiki hii. Mwakabana alisema mwanafunzi huyo alijifungua mtoto huyo na kumtupa katika choo cha shimo cha Shule ya Msingi Nyangwe akiwa hai na baadaye kuokolewa na wanafunzi wa shule hiyo.
Kamanda huyo alisema baada ya kuokolewa kutoka katika choo hicho cha shule kichanga hicho kilifariki muda mfupi baadaye na sasa mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa Kigoma ya Maweni.
Kufuatia hali hiyo Kamanda huyo wa polisi amesema kuwa hivi sasa Jeshi hilo la Polisi mkoani Kigoma liko katika jitihada za kumtafuta mwanafunzi huyo ili aweze kukabiliana na tuhuma zinazomkabili za kutupa kichanga na kusababisha mauaji.
No comments:
Post a Comment