Saturday, May 19, 2012

Mtoto ateleza na kufia kisimani



MWANAFUNZI wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Jitihada, katika Manispaa ya Ilala, Shomari Kimara (8), Mkazi wa Kitunda Matembele amekufa baada ya kutumbukia kisimani wakati akicheza na wenzake.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile alisema mwanafunzi huyo alikufa juzi saa 11:00 jioni wakati mtoto huyo akiwa na wenzake wakicheza karibu na maeneo ya kisima hicho lakini ghafla aliteleza na kutumbukia kwenye kisima hicho.

Alisema maji hayo yalimzidi mwanafunzi huyo na hatimaye kunywa maji mengi na kufa papo hapo.

Shilogile alisema mwili wa mtoto huyo uliopolewa na wananchi wa maeneo hayo na umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, huku upelelezi wa polisi ukiendelea zaidi.

Katika tukio jingine, moto ulizuka ghafla katika nyumba ya Zanuba Rajabu (42) na kuteketeza chumba kimoja na mali zilizokuwemo.

Kamanda Shilogile alisema moto huo ulizuka juzi saa 4:00 asubuhi katika nyumba hiyo ambayo iko katika mtaa wa Muheza ghorofa ya tatu .

Alisema moto huo uliteketeza chumba cha kulala watoto na mali zote zilizokuwemo. Chanzo na thamani ya moto huo bado hakijajulikana na moto huo ulizimwa na wananchi wa eneo hilo, hakuna madhara yaliyojitokeza kwa binadamu, upelezi bado unaendelea.

Katika tukio jingine, Watu watano wamekamatwa wakiwa na dawa za kulevya aina ya bango puli 5 na misokoto 15.

Watuhumiwa hao walikamatwa katika maeneo ya Msongola, Wilaya ya Ilala na askari waliokuwa wakifanya msako katika maeneo hayo. Watuhumiwa hao ni Mohamed Mussa (19), Issah Juma (22), Rajabu Athumani (25), Daud Ismail (18) na Mohamed Rashid (21).

No comments:

Post a Comment