Saturday, May 19, 2012

Binti- Inatosha, nisaidieni nirudi shuleni




BINTI mwenye umri wa miaka 18 mkazi wa kijiji cha Lossimingori, Kata ya Sepeko wilayani Monduli, Kilanda Melami ameiomba serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kumsaidia kuendelea na masomo, kwani licha ya kuzalishwa akiwa mwanafunzi, pia aliingia katika ndoa ya mateso kijijini kwao.

Kabla ya uamuzi wake wa kuendelea na masomo, binti huyo alisoma hadi kidato cha pili na kupata ujauzito, hivyo kumfanya asiendelee na masomo.


Na hata baada ya kurudi nyumbani, anasema baba yake alimwozesha kwa mahari ya ng’ombe wanane, hivyo kulazimika kuwa mke wa tatu wa mzee mmoja kijijini kwao.


Akisimulia, anasema baada ya kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2008, alitoroka nyumbani kwao na kwenda katika kituo kinachosaidia mabinti wa kimasai kupata elimu.


Anakumbuka kuwa, alipokelewa na baada ya masomo ya maandalizi ya kuingia kidato cha kwanza, mwaka 2009 alipelekwa Shule ya Sekondari Uroki wilayani Hai, Kilimanjaro alikoanza masomo, lakini katikati ya mwaka 2010, akiwa kidato cha pili aligundulika mjamzito hivyo kurudishwa nyumbani.


Hata hivyo, akiwa anasubiri kujifungua anasema baba yake mzazi aliyemtaja kuwa ni Melami Martin alimwozesha kwa mzee wa kijijini hapo baada ya kutoa mahari ya ng’ombe wanane.


“Mateso na manyanyaso yalianza baada ya kujifungua, nilipigwa sana hasa ikizingatiwa mtoto hakuwa wake, nikarudi nyumbani lakini baadaye alinifuata nirudi kwake, nilirudi nikiamini mambo yatabadilika, lakini yakawa yale yale…nikashindwa.


“Ninaomba wasamaria wema wanisaidie kuendelea na shule, kwani sitaki kurudi tena kwa yule mwanaume alininyanyasa mno, sasa nimeshaona umuhimu wa elimu na nitasoma kwa bidii,” alisema Kilanda.

 
     

No comments:

Post a Comment