Saturday, May 19, 2012

Dawa kudhibiti VVU yaanza kutumika rasmi



MAMLAKA ya Chakula na Dawa ya Marekani (FDA), imeidhinisha dawa ya Truvada kuwa tiba ya kuzuia kuenea kwa Virusi Vya Ukimwi (VVU).Dawa hiyo ambayo awali ilikuwa katika kundi la zile zinazotumiwa kwa ajili ya Kupunguza Makali ya VVU (ARV), imepandishwa chati wakati ambapo tayari ipo sokoni ikiuzwa kama moja ya ARV za kawaida.

Kwa mujibu wa maelezo ya FDA, mwathirika anayetumia dawa hiyo anaweza kujamiiana na mwenza wake ambaye hana VVU bila kutumia kondomu na hatomuambikiza.

Matokeo ya utafiti huo yaliwahi kuchapishwa kwenye gazeti hili toleo la Februari 12, mwaka huu na sasa kilichofanyika ni FDA kuidhinisha Truvada ambayo ilionyesha kufanya kazi vizuri ikilinganishwa na ARV nyingine.

Uidhinishaji wa dawa
Jopo la wanasayansi 22 wa FDA waliokutana Jijini Washington wiki iliyopita, walipitisha Truvada baada ya kupitia ripoti ya utafiti kuhusiana na ufanyaji kazi wa dawa za ARV.

Wanasayansi hao waliisifu dawa hiyo baada ya kuonekana kufanya kazi vizuri kwa watu waliopo kwenye hatari ya kuambukizana VVU kwa kasi zaidi.

Kwa namna dawa hiyo inavyofanya kazi, mwathirika akiitumia hawezi tena kumwambukiza mtu mwingine ambaye atashiriki naye tendo la ndoa bila kutumia kondomu.

Lakini, dawa hiyo masharti yake hayatofautiani na yale ya ARV kwani mtumiaji atapaswa kuitumia maisha yake yote ili kumwekea kinga asiwaambukize wengine na yeye aishi muda mrefu.

Kulingana na ripoti ya utafiti uliofanyika Marekani, dawa hiyo ina uwezo wa kuzuia maambukizi ya VVU hadi asilimia 90.Hata hivyo, kwa watu ambao wamekuwa wakitumia dawa holela hasa za ARV, hali imekuwa tofauti kwani Truvada imeonekana ikifanya kazi kwa kiwango cha asilimia 44 tu.

"Hii ni ishara kwamba kuna kundi la watu ambao dawa hiyo haitafanya kazi kikamilifu kutokana na mazingira ya matumizi ya dawa holela,"ilisema sehemu ya ripoti.

Hata hivyo, wanasayansi wanasema  tatizo hilo linafanyiwa uchunguzi ili kupata njia bora ya kukabiliana na tatizo hilo.

Faida ya Truvada
Wataalamu wameeleza kwamba itasaidia watu ambao wana VVU lakini, hawapendi kufanya tendo la ndoa kwa kutumia kondomu."Leo ni siku ya tukio la kuwasisimua wengi katika kuzuia maambukizi ya HIV,” alisema mmoja wa wataalamu kutoka Taasisi ya kujitolea kusaidia jamii ya Fenway, Dk Kenneth Mayer ambaye alikuwa miongoni mwa wajumbe wa FDA walioipitisha dawa hiyo.

"Ingawa (Truvada) haikuweza kuonyesha uwezo wa asilimia 100 kuzuia maambukizi ya VVU, namna inavyofanya kazi itakuwa na matokeo mazuri ya kupambana na Ukimwi duniani,” alisema Dk Mayer.

Tahadhari
Hata hivyo, wataalamu hao walihimiza kuwepo kwa uchunguzi zaidi wa kitafiti ili kujua kama Truvada itafanya kazi vizuri duniani kote.Mtaalamu wa Dawa kutoka Taasisi ya Taifa ya Saratani nchini Marekani (NCI),  Dk Lauren Wood alilalamika akisema kuwa utafiti huo haukuzingatia matatizo ya figo.

Alisema matatizo ya figo yamekuwa yakijitokeza kwa waathirika wengi wa Ukimwi hasa barani Afrika."Mimi sikufurahishwa sana kwa sababu utafiti huu haukuzingatia maeneo ambayo watu wengi wako kwenye hatari ya maambukizi,” alisema Dk Wood.

Lakini, alisema utafiti uliofanyika nchini Marekani umeonyesha wazi kwamba ni dawa inayoweza kupunguza kwa kiwango kikubwa kasi ya kusambaa kwa VVU.

Wataalamu kadha nao walisema pamoja na Truvada kupitishwa na FDA, ni lazima maelezo ya kitaalamu yatolewe kwa madaktari ili wawe na uelewa wa kutosha kuhusu matumizi yake.

Mabingwa hao walipendekeza kwamba, wanaotumia kabla ya kuruhusiwa kutembea na wenzi wao bila kondomu lazima wachunguzwe kitaalamu ili wajulikane kama dawa iyo imewakubali au la.

Mwanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha Afya cha Cincinnati, Dk Judith Feinberg alikosoa ripoti ya uchunguzi akisema ilipaswa kwenda mbali zaidi katika kuchunguza madhara yanayoweza kujitokeza kwenye matumizi ya dawa hiyo.“Tusipokuwa makini katika hilo, tunaweza tukawa tumepitisha jambo ambalo litasababisha madhara zaidi kuliko faida,” alionya Dk Feinberg.


Utafiti wa ARV
Wanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha Johns Hopkins ni miongoni mwa wale ambao walifanya uchunguzi juu ya ARV, kuwa moja ya dawa zinazopunguza maambukizi ya VVU.

Watafiti hao walibainisha kuwa wale wanaotumia ARV baada ya muda fulani, huweza kushiriki tendo la ndoa bila ya kutumia kondomu na mtu ambaye hana VVU na asimwambukize kwa asilimia 95.

Mkuu wa Mtandao wa Maabara za Kuchunguza VVU katika chuo hicho, Profesa Susan Eshleman alisema kwenye ripoti ya ugunduzi huo, wamebaini dawa za kurefusha maisha kwa waathirika wa HIV, sasa zinaweza kutumika kama sehemu ya kuzuia maambukizi.

Profesa Eshleman alisema kwamba, mwathirika wa VVU anayetumia ARV kikamilifu, anaweza kujamiiana na mtu ambaye hana virusi bila kondomu na asimwambukize.

“Huu ni ugunduzi wa kustajabisha,” alisema Profesa Eshleman akifafanua: “Matokeo haya yameleta mapambazuko mapya katika sayansi ya kuzuia maambukizi na inawaweka watafiti kwenye mazingira mazuri zaidi ya kupata suluhisho la kukabiliana na maradhi haya.”

Walivyogundua
Profesa Eshleman anasema utafiti huo walioupa jina la HPTN 052, walifanya kupitia maeneo mbalimbali ya dunia.

Kwenye ripoti hiyo ambayo pia ilichapishwa kwenye jarida maarufu la kisayansi linaloitwa Science, watafiti hao walisema mtu anapotumia ARV, hufikia wakati fulani wingi wa virusi mwilini hupotea kiasi kwamba anakuwa karibu sawa na yule ambaye hajaambukizwa.

“Jambo la msingi katika utafiti huu ni kwamba dawa hizi za kurefusha maisha zinapotumiwa kikamilifu, hupunguza mzigo wa virusi mwilini kwa zaidi ya mara 200. Ni sawa na kusema inapunguza hadi kufikia karibu na sifuri,” inaeleza ripoti hiyo.

Ni katika mazingira hayo, ripoti hiyo inasema kuwa damu ya mwathirika inakuwa haina virusi na hivyo uwezekano wa kumuambukiza mpenzi wake unakuwa haupo.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa ARV inafanya kazi mbili, kwanza kurefusha maisha ya mwathirika kwa kupunguza virusi mwilini na pili ni kumkinga asiambukize wengine.

Sifa nyingine ya ARV, alisema ni kupunguza uwezekano wa waathirika kupata ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) kutokana na kiwango cha kinga za mwili kuongezeka.

No comments:

Post a Comment