Monday, October 15, 2012

Rais wa Mauritania apelekwa Ufaransa

Serikali ya Mauritania imesema kuwa Rais Mohamed Ould Abdel Aziz wa nchi hiyo, amehamishiwa mjini Paris, Ufaransa kwa ajili ya matibabu zaidi na uchunguzi baada ya kujeruhiwa kwa kupigwa risasi kwa bahati mbaya.

Rais Abdel Aziz alionekana akizungumza na wananchi katika televisheni ya taifa akiwa hospitali na kuwahakikishia kwamba afya yake iko katika hali nzuri.

Amesema tukio hilo limetokea kwa bahati mbaya wakati msafara wake ulipokaribia kambi za jeshi katika barabara ambayo haikuandaliwa kwa ajili ya msafara huo kaskazini mwa Nouakchott.


Waziri wa Mawasiliano wa Mauritania, Hamdi Ould Mahjoub, alisema kuwa rais huyo amejeruhiwa mkononi, huku taarifa za vyombo vya habari nchini humo zikieleza kuwa kikosi cha usalama hakikuarifiwa kuhusu ziara ya rais.

Mauritania imekuwa haina utulivu kutokana na kundi linalojihusisha na mtandao wa kigaidi la Al-Qaida kuanzisha mashambulizi kutoka nchi jirani ya Mali.

No comments:

Post a Comment