Jeshi la Syria limeanzisha mashambulizi ya anga dhidi ya waasi kaskazini mwa nchi hiyo hii leo, katika harakati za kurejesha udhibiti wa maeneo yaliyotwaliwa na waasi katika siku za hivi karibuni.
Shirika la Uangalizi wa Haki za Binaadamu nchini Syria, limesema katika jimbo la kaskazini-magharibi la Idlib, ambalo kwa kiasi kikubwa liko chini ya waasi baada ya kulitwaa mwanzoni mwa juma hili, jeshi lilitumia ndege za kivita kushambulia Maaret al-Numan.
Mashariki mwa Maaret al-Numan, majeshi yalijaribu kuzuia shambulio jipya la waasi katika ngome ya kijeshi ya Wadi Dief, ambayo ni kubwa katika Jimbo la Idlib na ambako mafuta mengi na vifaru vimehifadhiwa.
Kwa mujibu wa shirika hilo la haki za binaadamu la Uingereza, mapambano yalizuka Maarshurin na Hish karibu na kambi hiyo, huku ndege za kivita zikishambulia eneo hilo. Mashambulio hayo ya anga yanafanyika baada ya waasi kuwateka maafisa watatu wa jeshi huko Idlib. Wiki iliyopita waasi waliripotiwa kuwateka wanajeshi 256 katika mapigano karibu na mpaka na Uturuki.
No comments:
Post a Comment