KITUO
cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimezindua Ripoti yake ya Haki
za Binadamu ya mwaka 2011 inayoonyesha pamoja na mambo mengine, wanawake
visiwani Zanzibar na katika Mkoa wa Dar es Salaam, wanaongoza kuwapiga
waume zao. Mbali na ukatili huo kwa wanandoa, ripoti hiyo imeonyesha pia kuwa vitendo vya rushwa nchini vimeendelea kuwa sugu na kugusa maeneo muhimu kwa ustawi wa jamii, ikiwamo bungeni ambako imedai kuwa baadhi ya wabunge wanahongwa ili kupitisha bajeti za wizara. Akisoma ripoti hiyo kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa LHRC, Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema asilimia 7.3 ya wanawake wa Unguja Kusini huwapiga waume zao wakifuatiwa na Mikoa ya Dar es Salaam, Mjini Magharibi na Lindi ambako asilimia 5.3 ya wanawake huwapiga waume zao. “Hata hivyo, Dar es Salaam inashika nafasi ya pili kwa kuwa ina watu wengi ikilinganishwa na mikoa mingine. Mkoa wa mwisho ni Iringa ambako tatizo hilo liko kwa asilimia 4.7,” alisema. Dk Bisimba alisema ripoti hiyo ni ya 10 kuzinduliwa na LHRC na ya mwaka huu imegusa maeneo mbalimbali na kuanisha yale ambayo haki za binadamu zinakiukwa kwa kiwango kikubwa. Alisema kulingana na tafiti zilizofanywa na waandishi wa ripoti hiyo, vitendo vya wanawake kuwapiga waume zao ni moja ya tatizo la ukatili kwa haki za binadamu. Dk Bisimba alisema mbali na ukatili wa wanawake kuwapiga waume zao, ripoti hiyo pia inaonyesha kwamba Mkoa wa Dodoma unaongoza kwa vitendo vya ukatili kwa kina mama ukifuatiwa na Mikoa ya Mara, Ruvuma, Morogoro na Kagera. “Ukatili wa kijinsia kwa kina mama na kina baba umeshamiri. Takwimu zinaonyesha kuwa Mkoa wa Dodoma unaongoza kwa asilimia 70.5 katika matukio ya wanaume kuwapiga wake zao, Mkoa wa Mara kwa asilimia 66.4 na Ruvuma kwa asilimia 50.8.” Rushwa Dk Bisimba alisema ripoti hiyo pia imeonyesha kuwa rushwa imekuwa bado tatizo nchini na sasa imeanza kuingia bungeni ambako baadhi ya wabunge wanahongwa ili kupitisha bajeti za wizara. “Ripoti yetu inaonyesha kwamba kumekuwa na vitendo vya rushwa hadi ndani ya Bunge jambo ambalo linachangia kuwanyima haki Watanzania hasa watu wa kipato cha chini kwani watu wachache wanafanya uamuzi kwa maslahi yao binafsi,” alidai Dk, Bisimba na kuongeza: “Miongoni mwa mambo ambayo yanaonyesha wazi kwamba rushwa imeingia mpaka ndani ya Bunge ni pale tuliposikia suala ya (David) Jairo (aliyekuwa Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, na tuhuma za baadhi ya wabunge kuomba rushwa kwa wakurugenzi wa halmashauri,” alisema. Bisimba alisema ripoti hiyo imeeleza kuwa licha ya kuwepo vitendo vya rushwa ndani ya Bunge, vimekuwa pia vikionekana katika maeneo mengine kadhaa ikiwamo usafirishaji wa wanyama kupitia viwanja vya ndege, kwenye chaguzi pamoja na vyombo vya usalama. “Ripoti inaonyesha kwamba suala la usafirishaji wanyamapori kupitia viwanja vya ndege mfano, Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro (Kia) ndege 120 wanaojulikana kama species walipelekwa ughaibuni mwaka 2010. Hii yote inatokana na kusahau misingi ya haki za binadamu,” alisema. Adhabu ya Kifo Kuhusu adhabu ya kifo, Dk Bisimba alisema bado kuna changamoto kubwa ya kuhakikisha adhabu hiyo inaondolewa kwani ni moja ya kitendo kinachowanyima wananchi haki ya kuishi. Alisema kila Mtanzania ana haki ya kuishi, na kwamba adhabu ya kifo ni inakiuka misingi ya haki za binadamu ya kuishi. “Mpaka sasa, asilimia 74 ya watu 600 walioshtakiwa na kuhukumiwa kifo, wanasubiri kunyongwa,” alisema. Aidha, ripoti hiyo inaonyesha uwepo wa watumishi wachache katika vyombo vya kutolea uamuzi kuwa ni miongoni mwa mambo ambayo yanachangia kuwanyima haki wananchi. Dk Bisimba alisema mpaka sasa, kuna mahakama 760 kati ya 1,000 zinazohitajika na mahakama za mwanzo 500 ambazo hazina mahakimu Ripoti hiyo pia imeonyesha kuwepo kwa upungufu wa watumishi wa sekta ya afya kwa asilimia 68 ikisema watumishi waliopo ni asilimia 32. Akizindua ripoti hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alisema Serikali inapaswa kuweka wazi matumizi ya rasilimali za taifa na kodi za wananchi ili wapate fursa ya kujua uhalali wa matumizi hayo na moyo wa kuendelea kuchangia maendeleo yao. “Ni vyema wanaohusika katika ufujaji wa fedha za Serikali wakachukuliwa hatua kwani hiyo ni mojawapo ya kuwanyima haki wananchi kwa kukosa maendeleo kutokana na kodi zao kutumiwa na viongozi wasio waadilifu,” alisema Profesa Lipumba. |
Tuesday, May 29, 2012
Wanawake wanaongoza kuwapiga waume zao Dar
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment