MKUU
wa Shule ya Sheria Dk Gerald Ndika, amesema ‘umbumbu’ kwenye suala la
mikataba ya kimataifa, linachangangia kuliingiza taifa kwenye wimbi la
mikataba mibovu. Dk Ndika aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, katika ufunguzi wa mafunzo ya mikataba yanayofanywa na wataalam kutoka kampuni ya kimataifa ya sheria ya DLA Piper na General Electric (GE). “Mikataba kama ya kukodisha ndege, inahitaji mtu ambaye amebobea katika eneo hilo siyo kila mtu tu anaweza kufanya kila kitu,” alisema Dk Ndika na kuongeza: “Kwa hiyo siyo rushwa tu inasababisha sisi kuwa na mikataba mibovu, hata kutokuwa na ujuzi wa kutosha katika kuandika na kujadiliana juu ya mikataba ya kimataifa ni tatizo.” Akisisitiza kuhusu suala hilo, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Angela Kairuki, alisema mbali na uandishi wa mikataba, suala la kuweza kujadiliana kwenye mikataba ya kimataifa ni muhimu zaidi. “Watu wanaweza kukuzidi ujanja tu kwenye kujadili na mkataba ukawa mbovu, kwa hiyo eneo hili pia lazima tulitazame kwa makini zaidi,” alisema Kairuki. Alisema kuwa ni vyema wafunzi hao wakapewa mafunzo zaidi juu ya mikataba ya mafuta na gesi, sekta ambayo inatarajiwa kuwa moja eneo muhimu la uchumi nchini. Mafunzo hayo yanatarajiwa kulenga zaidi katika kujenga uwezo na mbinu za kuandika maandiko ya kisheria katika uandikaji wa mijadala ikiwa ni pamoja na majadiliano na vipengele vya kutengeneza upatanishi na mizozo. Mwendelezo wa kesi mahakamani, mikataba ya kuuza na kununua, mikataba ya mikopo ni maeneo mengine ambayo wataalam hao kutoka nchi mbalimbali za Ulaya na Afrika watawafunza wanafunzi hao. Mkuu wa mradi huo Simon Boon kutoka DLA Piper ya London, alisema ni jambo zuru kuwa nchini kwa mara ya tatu kutoa mafunzo hayo, tangu mpango huo ulipoanza mwaka 2010. “Tunafurahi kupindukia kurudi kwa mara ya tatu mfululizo kufundisha uandishi wa sheria katika chuo cha sheria Tanzania,” alisema Boon. |
Tuesday, May 29, 2012
Umbumbumbu unaliumiza taifa kwenye mikataba
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment