Monday, May 28, 2012

Zanzibar yachafuka


KANISA la Assemblies of God liliopo Kariakoo mjini Unguja, limechomwa moto na kuharibiwa vibaya katika vurugu zilizoibuka jana asubuhi. 

Waumini wa kanisa hilo walishindwa kufanya Ibada ya Jumapili katika kanisa hilo kutokana na uharibifu mkubwa huku wakiwa na hofu.
 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Aziz Juma alithibitisha kuchomwa moto kwa kanisa hilo juzi usiku wa saa nne na gari moja aina ya Corolla kuharibiwa vibaya.

 “Ni kweli Kanisa la Assemblies of God liliopo Kariakoo limechomwa moto na watu wasiojulikana na uchunguzi zaidi kujuwa nani waliohusika unaendelea,” alisema Juma. Kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo, Dickson Kaganga alisema watu wasiojulikana, walivamia kanisa hilo saa nne za usiku juzi na kuanza kuwashambulia walinzi ambao walizidiwa na kukimbia.

 Kaganga alisema uharibifu mkubwa umefanyika ndani ya kanisa hilo na vifaa vya muziki na vipaza sauti vyote vimeharibiwa. “Kanisa limeharibiwa vibaya na linahitaji matengenezo makubwa sehemu ya ndani na nje,” alisema. Kanisa hilo lilivamiwa na kutiwa moto mara baada ya viongozi wa Jumuiya ya Kiislamu ya Uamsho kukamatwa na Polisi kwa kufanya maandamano kinyume cha sheria. Askofu Kaganga aliitaka Serikali kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo ambalo linahatarisha amani na utulivu pamoja na uhuru wa kuabudu. 

 Alisema tangu kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, amani na utulivu vimeimarika Zanzibar, lakini katika siku za hivi karibuni kumeibuka vikundi vinavyotoa mihadhara ya kidini vimeonesha kutishia amani hiyo. Polisi, CCM kwavamiwa Awali wafuasi wa jumuiya hiyo inayojishughulisha na mihadhara ya kidini pamoja na kisiasa, walivamia Kituo cha Polisi cha Madema kuwatoa viongozi wao waliokamatwa. 

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Khamis alisema Polisi ilifanikiwa kuzima jaribio la wafuasi wa jumuiya hiyo kuvamia kituo cha Polisi na kuwatoa wafuasi wao.

 “Ni kweli wapo baadhi ya viongozi tunawashikilia kwa ajili ya maelezo zaidi na wafuasi wao wakaja kundi na kuvamia kituo, lakini polisi walipambana na watu hao,” alisema Mussa. Mussa alisema Polisi inawashikilia watu saba kwa tuhuma za kuhusika na vurugu za jumuiya hiyo pamoja na viongozi wawili wa kikundi hicho.

 Alisema Polisi inaendelea na kazi za kuwatafuta zaidi viongozi wakuu wa mihadhara inayotolewa na jumuiya hiyo. Viongozi wengine wanaotafutwa na Polisi ni Amiri wa jumuiya hiyo, anayetajwa kwa jina moja la Azani pamoja na kiongozi wa Jumuiya ya Mihadhara, Farid Hadi. Aidha, Polisi imeimarisha ulinzi kwa kutumia helikopta yake ambayo ilionekana ikiruka angani mara kwa mara kwa ajili ya kuimarisha doria. 

Kamishna Mussa alithibitisha kuchomwa moto kwa gari moja jirani na Ofisi Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kisiwandui mjini hapa na uchunguzi zaidi unaendelea. Mabomu, risasi Shughuli zote za kibiashara pamoja na kijamii katika eneo la Mji Mkongwe wa Unguja zilisimama kuanzia asubuhi baada ya Polisi kufyatua risasi pamoja na mabomu ya machozi ili kutawanya vikundi vya watu walioaminika kuwa wafuasi wa jumuiya hiyo. 

“Shughuli zote za kibiashara hapa zimesita ikiwemo usambazaji wa magazeti hata wauza magazeti wote wameshindwa kufika mjini kufanya biashara,” alisema Farouk Karim ambaye ni Wakala wa Magazeti. Muuza magazeti maarufu wa Darajani Mji Mkongwe Zanzibar, aliyejitambulisha kwa jina moja la Abel alisema ameshindwa kufika mjini kutokana na fujo pamoja na mabomu ya machozi yanayopigwa na polisi. 

“Narudi nyumbani leo sikufanya kazi kwa sababu huko mjini kwenyewe hakufikiki kutokana na mabomu ya machozi,” alisema Abel. Vizuizi, doria Polisi waliweka vizuwizi katika baadhi ya sehemu za miji ikiwamo Michenzani pamoja na barabara za kwenda Ikulu ili kuhakikisha hakuna vikundi vya watu wanaofika maeneo muhimu yakiwamo ya ofisi za Serikali. Vizuizi hivyo viliwekwa katika maeneo ya kwenda vijijini katika mikoa ya Kusini Unguja na Kaskazini Unguja ili kuhakikisha hakuna vikundi vya wafuasi wa jumuiya hiyo wanaoweza kuingia mjini kuungana na wenzao waliopo mjini.

 Aidha, Polisi walikuwa wakifanya doria hadi katika maeneo ya Ng’ambo ikiwamo Mikunguni pamoja na Saateni na kurusha mabomu ya machozi kwa lengo la kusambaza vikundi vya watu. Vikundi hivyo vilikuwa wakiwasha mipira ya gari na kuweka vizuwizi katika baadhi ya maeneo ya Mji wa Unguja. 

Jumuiya hiyo kwa muda wa miezi minne sasa imekuwa ikitoa mihadhara kuhusu marekebisho ya Katiba ya Muungano kwa kuhamasisha wananchi kuukataa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kikundi hicho kilifanya mhadhara wake juzi asubuhi Lumumba na kuanza kufanya maandamano ambayo yalizuiwa na Polisi.

No comments:

Post a Comment