Monday, May 28, 2012

Basi lililozama laopolewa



BASI dogo la abiria lililotumbukia katika Ziwa Victoria kwenye kivuko cha Kigongo wilayani Sengerema likiwa na abiria 40, limeopolewa huku abiria wake wakilalamika kupoteza vitu
mbalimbali vya thamani.

Akizungumza kwa simu, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema ilihusisha basi dogo la abiria aina ya Toyota

Coaster lenye namba za usajili T720 BDY lililokuwa likisafiri kutoka wilayani Geita kwenda jijini Mwanza.

Kamanda Barlow alisema ajali hiyo ilitokea Ijumaa jioni na kwamba gari hilo lilikuwa likiendeshwa na dereva ambaye hajajulikana jina lake kwani alitoroka mara baada ya

kuokolewa. Basi hilo liliondolewa ndani ya ziwa saa 2 usiku.

“Gari liligonga uzio wa kivuko na kushindwa kusimama na hatimaye kutumbukia ziwani, hakuna abiria aliyepata majeraha makubwa wala aliyefariki dunia kutokana na tukio hilo,” alisema na kuongeza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni kukatika kwa breki kwa basi hilo na kumfanya dereva kushindwa kulimudu ambapo lilitumbukia kwa kulalia ubavu ndani ya maji likiwa na abiria hao.

No comments:

Post a Comment