Tuesday, June 12, 2012

Afya ya Mubarak yazidi kuwa mbaya

Hali ya afya ya Rais wa zamani wa Misri Hosni Mubarak imezidi kuwa mbaya leo, akipoteza fahamu na na kulishwa chakula cha maji maji kwa kutumia mpira.

Kwa mujibu wa maafisa katika hospitali ya gereza la Torah anakotumikia kifungo cha maisha , madaktari walilazimika kutumia chombo cha kumrejeshea fahamu mara mbili kiongozi huyo wa zamani.


 Madaktari hao hawakusema kama  moyo wa  Mubarak mwenye umri wa miaka 84 ulikuwa umesita kufanya kazi, lakini walieleza kwamba alipoteza fahamu mara tatu kuanzia jana hadi leo.

 Habari zinasema watoto wake wa  kiume Gamal na Alaa walikuwa karibu naye.   Kwa mujibu wa maafisa wa Misri, afya ya Mubarak imezorota  mno tangu alipohukumiwa  kifungo cha maisha  mapema mwezi huu kwa kushindwa kuzuwia mauaji ya waandamanaji, wakati wa vuguvugu la umma lililomn´goa madarakani  mwaka uliopita.

 Wanawe  Gamal na Alaa hawakupatikana na hatia kuhusiana na mashtaka ya rushwa, lakini wamebakia gerezani kusubiri kesi nyengine inayowakabili kuhusu biashara .

No comments:

Post a Comment