Friday, June 8, 2012

Harambee ya Lowassa yazoa milioni 400



WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu wadhifa huo Edward Lowassa amechangisha kiasi cha Sh.400milioni kutoka kwa wadau mbalimbali wa Maendeleo ya Elimu kwa ajili ya kuboresha miundombinu  ya Elimu katika Kata ya Kipawa jijini Dar es Salaam.

Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli aliwezesha kuchangwa kwa kiasi hicho cha pesa wakati wa harambee iliyoandaliwa na diwani wa Kata ya Kipawa Bonnah Kaluwa iliyofanyika juzi usiku Dar es Salaam, ambapo yeye alikuwa mgeni rasmi.

Kabla ya kuendesha haramabee hiyo Lowassa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama alisema kuwa kuchangia uboreshaji wa elimu nchini ni jambo la heshima na linawezekana kuondoa changamoto zinazozikabili shule mbalimbali.

Lowassa alisema mjini ambako maisha ni nafuu kulinganisha vijijini shule zinakabiliwa na matatizo makubwa ya miundombinu, kwa vijijini shule nyingi ziko katika hali mbya zaidi.

“Kila kata sekondari zilizoanzishwa na serikali baadhi hazina vyumba vya madarasa vya kutosha, maabara wala nyumba za walimu. Watanzania tukiamua na tukiongozwa vizuri tunaweza kuzichangia’ alisema.

Aliongeza kuwa Wakuu wa Mikoa, Wakurugenzi wa Manispaa, Maofisa Elimu wa mikoa wanaweza kufanya haya, na kwamba Kipawa wameonesha njia.

“Tuhimizane kwa hili. Madiwani na wabunge wote Tanzania tuige hili,” alisisitiza Lowassa.
Awali Meya wa Manispaa ya Ilala Jerry Slaa alisema ili kukabiliana na matatizo ya miundombinu  katika Manispaa hiyo iliyomo kata ya Kipawa zinahitajika zaidi ya Sh.300bilioni.
Meya Slaa ambaye Manispaa yake ilichangia Sh.10milioni, alitoa wito kwa serikali kuangalia namna ya kugharimia elimu nchini.

Katika harambee hiyo  Lowassa alichangia kiasi cha Sh.10miloni huku Benki ya Uwekezaji (TIB) ikivunja rekodi kwa kuchangia madawati 50 yenye thamani ya zaidi ya  Sh.300milioni, wakati kampuni ya Maersk Sealine ilichangia Sh.90milioni  ikifuatiwa na Lions Club iliyochangia Sh.70milioni.

Baadhi ya makampuni mengine na watu binafsi waliochangia katika harambee hiyo ni pamoja na Home Shopping Centre iliyochangia Sh.22milioni, mfanyabiashara Yusufu Manji Sh.15milioni, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini kabla ya kuondolewa katika wadhifa huo hivi karibuni William Ngeleja Sh.10milioni.

Pia Chama cha Mapinduzi (CCM) kilichangia Sh.20milioni sawa na kampuni ya Simon Group, wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) kikichangia Sh.10milioni huku  kampuni ya madini ya Barrick Gold Mine ilichangia dola za Marekeni 10,000.

Akitoa shukrani mbunge wa jimbo la Segerea ambapo imo kata ya Kipawa ambaye pia Naibu Waziri Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana Dk. Milton Makongoro alisema mbali na michango hiyo kuna watu wengine ambao wamechukua fomu za kuchangia ambazo bado wanaendelea kuzikusanya.

No comments:

Post a Comment