SERIKALI,
KAMATI YA BUNGE WAELEWANA, ZITTO ASEMA NI BAJETI YA KULIPA MADENI, MAMA
LISHE WATAKA MFUMUKO WA BEI USHUKE, WALIA MAISHA Waandishi Wetu LEO
ni siku ya Bajeti kwa mwaka wa fedha 2012/13. Waziri wa Fedha, Dk
William Mgimwa anatarajiwa kuanza kusoma Bajeti ya Serikali
inayosubiriwa kwa hamu na mamilioni ya Wananchi 10.00 jioni. Hotuba
ya Dk Mgimwa itatanguliwa na ile ya Mipango ya Serikali itakayosomwa
asubuhi mara baada ya kipindi cha Maswali na Majibu na Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira.
Kutwa nzima
ya jana, Dk Mgimwa na watendaji wengine wa Wizara ya Fedha walikuwa
katika pilikapilika za kukamilisha maandalizi ya bajeti hiyo ya Sh15
trilioni, ambayo inatarajiwa kuwa na vipaumbele saba.
Baada ya
kipindi cha maswali na majibu jana, Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa CCM,
ilikutana chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kufanya
maandalizi ya kuwapa taarifa ya bajeti hiyo wabunge wakewaliotarajiwa
kukutana kuanzia saa 10 jioni. Kikao hicho ambacho kiliendelea hadi
saa tisa alasiri, pia kilihudhuriwa na Dk Mgimwa na Manaibu wake, Janeth
Mbene na Saada Mkuya Salum ambao kama alivyo waziri wao, nao wote ni
wapya katika wizara hiyo.
Dk Mgimwa alisema jana kwamba
maandalizi ya bajeti yalikuwa yamekamilika na tayari Serikali ilikuwa
imefikia mwafaka na Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi inayoongozwa na
Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge.
“Hoja za
wajumbe wa Kamati ya Bunge ni kwamba Serikali iongeze Bajeti ya
Maendeleo kutoka asilimia 30 hadi 35 na Bajeti ya matumizi ya kawaida
ishuke kutoka asilimia 70 hadi 65, lakini tumejaribu kufanya mapitio ya
pamoja imeshindikana,” alisema Dk Mgimwa na kuongeza:
“Hata
hivyo, tumekubaliana kwamba kuanzia mwaka ujao wa fedha tuanze kujipanga
mapema ili tuweze kufikia lengo hilo na hata ikiwezekana tuvuke hapo.”
Kwa
upande wake, Chenge alisema: “Tumewasikiliza na mazingira ndiyo hayo
sasa katika hatua hiyo unafanyaje? Lakini hata wao (Serikali) wameanza
kuona umuhimu wa hoja yetu kwa hiyo tumeelewana nao kwamba katika bajeti
ijayo ambayo nayo haiko mbali, basi wazingatie mapendekezo ya wabunge.” Hata
hivyo, Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe alisema Bajeti hiyo ya
Serikali haitoi matumaini kwa Watanzania kwani itakuwa ni kwa ajili ya
kulipa madeni.
“Hii yaweza kuwa Bajeti ya kulipa madeni zaidi
kuliko ya kuchochea maendeleo.... yaweza pia kuwa ni Bajeti ya kukopa
maana jumla ya Sh 5.1 trilioni (Dola za Marekani 3.19 bilioni),
zitachukuliwa kama mikopo kwa Serikali. Mikopo ya kibiashara ambayo ni
mikopo ghali sana itachukuliwa kwa wingi zaidi kuliko mwaka wa fedha
uliopita.”
Hofu ya kukwama Awali, kulikuwa na hofu kwamba bajeti hiyo ingekwama kutokana na wabunge kusisitiza kuongezwa kwa fedha maendeleo.
Hata
hivyo, wabunge kupitia Kamati ya Fedha ya Uchumi walilegeza msimamo wao
kutokana na maombi ya Waziri Mgimwa na Waziri Mkuu, Pinda ambao kwa
nyakati tofauti, walinukuliwa katika vikao vya kujadili bajeti hiyo
wakiwaomba wabunge wasiwabane kwani watendaji wa wizara hiyo walikuwa ni
wapya.
Lakini kuna taarifa kwamba hata sura ya sasa ya bajeti
hiyo inatokana na Dk Mgimwa kuifumua katika baadhi ya maeneo baada ya
kuingia ofisini kutokana na mabadiliko ya Baraza la Mawaziri
yaliyofanywa mapema mwezi uliopita na Rais Jakaya Kikwete na kumweka nje
aliyekuwa akiongoza wizara hiyo, Mustafa Mkulo.
Pinda
alinukuliwa akizungumza katika kikao cha kutoa mwongozo kwa wabunge wote
(briefing) kwamba, Dk Mgimwa aliomba ridhaa ya Rais kufumua bajeti hiyo
upya ili iweze kwenda sawa na mtizamo wake kama kiongozi wa wizara,
hali iliyosababisha kuchelewa kwa vitabu vya bajeti kwani baadhi
viliandaliwa upya.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge wakiwamo wa CCM
walisema kwa nyakati tofauti kwamba wanaiona Serikali kutokuwa na
usikivu kwani mapendekezo yao kila mwaka yamekuwa hayatekelezwi. “Ni
yale yale tu, kweli Dk Mgimwa ni mpya kwenye Wizara lakini hata angekuwa
Mkulo hakuna kinachotekelezwa, kila siku wanaahidi halafu
hawatekelezi.” alihoji mmoja wa wabunge wa CCM jana. Hata hivyo,
wabunge wa CCM hawawezi kuzuia Bajeti Kuu ya Serikali kutokana na
kubanwa na kanuni za chama hicho, lakini huenda hasira zao zikaziangukia
bajeti za wizara na kuwaweka mawaziri katika wakati mgumu.
Uchambuzi wa Zitto Uchambuzi
wa Zitto unaweka wazi kwamba vitabu vya Bajeti vinaonyesha mafungu
matano ya juu kwenye Bajeti hiyo kuwa ni Deni la Taifa (Sh2.7 trilioni),
Wizara ya Ujenzi (Sh1 trilioni), Wizara ya Ulinzi (Sh920 bilioni),
Wizara ya Elimu (Sh721 bilioni) na Wizara ya Nishati na Madini (Sh641
bilioni) ambazo jumla yake ni Sh5.982 trilioni.
“Jumla ya mafungu
haya ni sawa na asilimia 40 ya Bajeti. Kwa hiyo asilimia 40 ya Bajeti
yote imepangwa kwa mafungu matano tu. Fungu lenye kiwango kikubwa zaidi
ya Bajeti kuliko vyote ni fungu 22 ambalo ni malipo kwa Deni la Taifa,”
unaeleza uchambuzi huo uliofanywa na Zitto na kuongeza: “Pia sehemu
kubwa ya fedha zilizotengwa kwa Ujenzi na Nishati ni madeni kwa
makandarasi wanaotekeleza miradi ya miaka ya nyuma. Wabunge wanapaswa
kufanya uchambuzi zaidi wa Bajeti ya mwaka huu inayopendekezwa na
Serikali.”
“Kuna haja kubwa ya kuharakisha kuanzishwa kwa Ofisi
ya Bajeti katika Bunge na Kamati ya Bunge ya Bajeti ili kuweza
kufuatilia kwa karibu, kuchunguza na kutoa taarifa kwa wabunge ili
kuwezesha kuboresha Bajeti.”
Kilio cha wafanyabiashara Wafanyabiashara
katika Soko Kuu la Kariakoo, Dar es Salaam wametaka bajeti hiyo iwe ya
kumaliza tatizo la mfumuko wa bei ya vyakula.
Akizungumza kwa
niaba ya wenzake, mmoja wa wafanyabiashara hao, Elizabeth Edward alisema
bajeti mara nyingi imekuwa haiwalengi watu wa hali ya chini, bali wenye
uwezo. Edward alitaka Bunge litumie kipindi hiki kupunguza mfumuko wa bei ya chakula ili wananchi waweze kuona unafuu wa maisha.
“Hivi
sasa mchele mzuri unauzwa kuanzia Sh2,200 hadi Sh2,500 lakini, mimi
siwezi kununua mchele wa bei kubwa. Nitanunua mchele wa Sh1,800 hadi
1,660 ambao ni mbaya una mchanga,” alisema Mama Lishe huyo na kuongeza:
“Mafuta
ya kula tunauziwa lita moja Sh3,000, sukari Sh2,400 hivyo kutokana na
vyakula kupanda, chai tunauza Sh200 na vitafunwa kuanzia Sh200 hivyo,
watu wengi hawanunui, mtu anaona bora ale muhogo wa Sh100 na maji tu.”
Mfanyabiashara
wa Soko la Mabibo, Issa Abdallah alisema bajeti hiyo haimwangalii
mfanyabiashara wa chini... “Tunataka Bunge liilegeze bajeti ili kuondoa
mfumuko wa vyakula hapa nchini.” “Kama wabunge wangekuwa na umoja,
nina imani huu mfumuko wa bei ya vyakula usingekuwapo hivyo, wabunge
wote wanatakiwa wagomee bajeti ambayo itamkandamiza mwananchi wa hali ya
chini.”
Mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu Mzumbe, Dk Prosper
Ngowi alisema kutokana na hali ya uchumi wa nchi kukabiliwa na
changamoto ya mfumuko wa bei na umaskini wa watu wake, inahitajika
bajeti inayoweza kutoa majibu kwenye matatizo ya msingi.
Dk Ngowi
aliyataja matatizo hayo kuwa ni pamoja na umeme, miundombinu ya
umwagiliaji na ile ya usafirishaji kama barabara na reli.
Hata
hivyo, alisema dalili zinaonyesha kuwa hilo haliwezi kufanikiwa, kwani
katika Sh15 trilioni zinazotarajiwa kuwasilishwa kama Bajeti ya Serikali
kwa mwaka wa fedha wa 2012/13, Sh5 trilioni pekee ndizo zinatarajiwa
kutumika kwa shughuli za maendeleo.
“Kuna tetesi kuwa kati ya
hizo Sh5.25trilioni zitakwenda kulipa madeni na zitakazobaki ndizo za
maendeleo, hali hii inaonyesha kabisa kuwa hakuna matumaini,” alisema Dk
Ngowi.
Alisema swali jingine la kujiuliza ni wapi Sh15 trilioni
za bajeti zitakakopatikana akisema ukusanyaji wa kodi wa Serikali
hauridhishi na pia nchi wahisani zinazotegemewa nazo pia hali yake ya
kiuchumi siyo nzuri.
Habari hii imeandikwa na Neville Meena, Dodoma, Pamela Chilongola, Fredy Azzah na Raymond Kamnyoge, Dar |
No comments:
Post a Comment