Thursday, June 14, 2012

MAJAMBAZI WANNE WAKAMATWA MANYARA

JESHI la polisi Mkoani Manyara linawashikilia watu wanne wanaodaiwa kuwa ni majambazi waliotumia silaha na kuwateka watu wawili na gari aina ya Fusso lililobeba magunia 100 ya zao la alizeti lililotokea wilayani Kiteto wakielekea kuuza mjini Arusha.
 
Watu hao walikamatwa  saa 11 jioni kwenye eneo la Majengo mjini Arusha na askari watano wa kituo cha polisi Mirerani Wilayani Simanjiro wakiongozwa na Mkuu wa kituo hicho,Ally Mohamed Mkalipa.
 
Akithibitisha tukio hilo,Kamanda wa polisi mkoani Manyara,Akili Mpwapwa alisema watu hao wanadaiwa kuteka gari hilo aina ya Fusso kwenye eneo la Hoi hoi wilayani Simanjiro kwenye barabara kuu ya Orkesumet-Kibaya.
 
Kamanda Mpwapwa alisema watu hao walifanya tukio hilo la utekaji mnamo Juni 9 mwaka huu saa 12 jioni kwenye eneo la Hoihoi kata ya Shambarai wilayani Simanjiro wakati gari hilo mali ya mwarabu mmoja wa Moshi likiwa barabarani.
 
Aliwataja watu hao kuwa ni Gilbert Bernad (34) mkazi wa Himo mjini Moshi Julius John (40) mkazi wa Kibaya Wilayani Kiteto,Hamis Seif (33) na Juma Hussein (28) wote wakazi wa Kiteto mkoani Manyara.
 
Alisema wakati dereva akiendesha gari hilo aina ya Fusso walipofika eneo la Hoi hoi walikuta kizuizi kimewekwa barabarani na ghafla wakajitokeza watu wanne waliokuwa na silaha na kuanza kupiga risasi hewani. 
 
“Baada ya kupiga risasi hewani dereva na utingo walipata hofu na kuteremka kwenye gari hilo wakaanza kuongozwa kuelekea eneo la Shambarai na wakahifadhi mzigo kwa kiongozi mmoja wa Serikali,” alisema Kamanda Mpwapwa.
 
Alisema baada ya kuweka mzigo huo kwa kiongozi huyo walirudi porini kwa kutumia pikipiki wakiwa na watu hao kisha wakawaachia na wakaurudia mzigo huo na kuupeleka kuuza mjini Arusha.
 
Alisema polisi walipopata taarifa ya tukio hilo walianza uchunguzi wao na kufanikiwa kupata tetesi kuwa mzigo huo upo mjini Arusha ndipo askari wetu wakafanikiwa kupata magunia hayo 100 ya alizeti.
 
“Tumefanikiwa kukamata magari mawili aina ya Canter yenye namba za usajili T 978 ASS na T 999 AMA yote aina ya Canter ambayo yalikuwa yamepakiwa magunia hayo 100 ya alizeti hizo,” alisema Kamanda Mpwapwa.
 
Alisema kwamba askari wake bado wanaendelea na upelelezi wa tukio hilo kabla ya kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hao pindi uchunguzi wake utakapokuwa umekamilika.

No comments:

Post a Comment