Thursday, June 14, 2012

Wanaodaiwa kuua tembo kwa sumu wakamatwa Ngorongoro

 

watuhumiwa wakiwa wameshikilia maboga yanayodaiwa ni sumu kali kwa tembe 

Wakazi wanne wa Kijiji cha Kambi-ya-Simba, wilayani Karatu wamekamatwa wakiwa na maboga kumi yanayodaiwa kuwa na sumu kali ya kuua Tembo.

Maboga hayo yakiwa yamepangwa kando ya mto Sahata, ndani ya hifadhi ya msitu wa Nyanda za Juu Kaskazini, huku yakiwa yameunganishwa  pamoja kwa kamba, yanadaiwa kuwa na kemikali aina ya ‘Aldicarb’ yenye uwezo wa kuua Tembo kwa chini ya dakika ishirini iwapo wanyama hao wangekula hayo maboga.

“Taarifa ya mkemia mkuu wa serikali yenye namba 242/5394 inaonesha kuwa sumu hiyo ya Aldicarb inayouzwa kwa nembo ya ‘Temik,’ huathiri mfumo wa fahamu au neva na kuweza kumdondosha tembo mkubwa ndani ya dakika ishirini na kuuozesha mwili wake katika muda wa masaa machache hivyo kufanya zoezi la kutoa meno ya wanyama hao kuwa rahisi,” alisema meneja wa huduma za utalii wa hifadhi ya ngorongoro Amiyo T. Amiyo.

Waliokamtwa kuhusiana na tukio hilo ni pamoja na Romani Hamsi, akiwa na kaka yake Jonah Hamsi, Issaya Arusha na John Nindi wote wakiwa ni wakulima na wakazi wa kata ya Mbulu-Mbulu wilayani Karatu.

Hata hivyo kwa mujibu wa mmoja wao, Romani Hamsi walikamatwa wakiwa shambani wanalima ila kuhusu maboga yenye sumu, watuhumiwa hao wanadai kuwa yakitegwa na mtu mwingine aitwaye Filipo Ami ambaye ametoroka.

Mkuu wa kituo cha polisi cha Tarafa ya Ngorongoro Yohana Sinda amesema watuhumiwa hao walionekana wakiingia msituni wakiwa na maboga yaliyofungwa kwenye mashuka na baadhi ya wakajiji wa Kambi-ya-simba ambao ndio hasa waliotoa ripoti polisi.

Msemaji wa hifadhi ya Ngorongoro, Adam Akyoo amesema siku chache zilizopita tembo mkubwa alikutwa akiwa amekufa kwa sumu hiyo lakini waliwahi kabla ya maharamia kuiba pembe zake na maaafisa wa NCAA walizitoa na kumzika mnyama huyo haraka.

No comments:

Post a Comment