Tuesday, June 5, 2012

Mengi atangaza neema kwa wafanyakazi IPP


Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi
Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, ametangaza neema kwa wafanyakazi wake ambapo wataweza kumiliki hisa za baadhi ya kampuni tanzu zilizopo chini ya IPP baada ya kuziorodhesha katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Aidha, ametangaza kuwa kima cha chini cha mishahara kwa wafanyakazi wa makampuni hayo kitakuwa Sh. 450,000 kwa mwezi.



Dk. Mengi alitangaza neema hiyo juzi usiku jijini Dar es Salaam wakati wa chakula cha usiku alichowaandalia wafanyakazi zaidi ya 850 kutoka makampuni yote yaliyoko chini ya IPP.


Dk. Mengi alisema kwa kuanzia ataanza kusajili kampuni mbili na kwamba hivi sasa wataalamu wanafanyia kazi jambo hilo ili kuhakikisha kuwa linatakelezwa mapema iwezekanavyo.


Alisema katika azma hiyo, zitatengwa hisa zitakazotolewa kwa wafanyakazi bila malipo kama motisha kwa kutambua mchango wao kwa kampuni hizo.


“Kwa kuanzia tunatarajia kusajili kampuni zetu mbili kwenye soko la hisa na kutakuwa na hisa kwa ajili ya wafanyakazi wa IPP, nia ni kutufanya sote kuwa sehemu ya IPP,” alisema.


Akizungumzia kuhusu kupanda kwa kima cha chini cha mishahara, Dk. Mengi alisema nia kuwawezesha wafanyakazi kuweza kukabiliana na kupanda kwa gharama za maisha.


“Kiwango hicho ni cha chini, lakini kampuni husika inaweza kupanga kiwango cha juu zaidi kutokana na uzalishaji wake,” alisema.


Dk. Mengi pia alifafanua kuhusu misaada anayoitoa kwa jamii hususan watu wasio na uwezo.

Alisema wanaosaidiwa wana maisha magumu na kwamba anafanya hivyo kwa niaba yao, kwa vile anachokitoa ni sehemu ya pato ambalo wafanyakazi wa IPP wanachangia katika kulizalisha.

Alisema uamuzi wa kuwasaidia wenye mahitaji haumsaidii yeye binafsi na kwamba ni kwa manufaa ya wafanyakazi wote. “Sisi sote tunawasaidia wenye mahitaji kwa kuwa tunachotoa ni sehemu ya jasho lenu. Tunapata baraka sote kwa kusaidia wenye mahitaji zaidi,” alisema.


Wakati huo huo, Dk. Mengi alizungumzia kampuni za IPP kuingia kwenye uwekezaji wa sekta ya madini nchini kwa kuanzia hatua ya utafiti wa madini kwa kuwa Watanzania wengi bado wana uelewa mdogo kuhusu sekta hiyo bila kutambua kwamba utafutaji wa madini huweza kuwapatia pato kubwa.


“Nimeamua kuanzisha kampuni ya madini na sasa hivi tupo kwenye utafiti wa madini ya aina mbalimbali hapa nchini…tuna leseni nyingi tu …Watanzania wengi bado wana uelewa mdogo kuhusu sekta hii na ndiyo maana tumewaachia wageni wakiiendeleza,” alisema.


Aliongeza: “Watu wanadhani kwamba kuwekeza kwenye madini ni hatari. Kwa miaka sasa wengi wanadhani kazi ya madini inaanza na uchimbaji, napenda kuwahakikishia kwamba ni utafiti kwanza na kuna fedha nyingi huko.”


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ITV/ Radio One, Joyce Mhavile, alimpongeza Dk. Mengi kwa kuandaa chakula cha pamoja na wafanyakazi wake pamoja na kupewa tuzo kadhaa za heshima za kimataifa hivi karibuni.


Mhavile pia alitangaza kuwa Mengi ameanzisha tuzo ya mfanyakazi bora wa mwezi na wa mwaka ambapo kila mwezi mfanyakazi bora wa kila kampuni tanzu ya IPP atazawadiwa Sh. 500,000 na wa mwaka atazawadiwa Sh. 1,000,000 ambazo zitatolewa na Dk. Mengi.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment