Mwenyekiti wa wa Chadema, Freeman Mbowe
MWENYEKITI
wa Chadema, Freeman Mbowe amesema moto uliowashwa na chama hicho katika
Operesheni Sangara utaendelea nchi nzima, lengo likiwa ni kuiondoa CCM
madarakani na iwapo itasalimika mwaka 2015, atajiuzulu siasa.
Mbowe
alitoa kauli hiyo juzi alipohutubia mamia ya wakazi wa Wilaya ya Masasi
mkoani Mtwara wakati chama hicho kilipofanya mkutano mkubwa kwenye
uwanja wa mpira wilayani humo.
Alisema CCM kimepoteza mwelekeo wa
kuongoza taifa na ndiyo sababu maisha ya Watanzania yamezidi kuwa mgumu
kadri miaka inavyozidi kusonga mbele.
“Wajibu wa Serikali kokote
duniani ni moja tu, kuwezesha watu wake kutoka katika hali ngumu za
maisha na kuwapeleka kwenye heri, leo CCM wameligawa Taifa katika
vipande, wanauza rasilimali za nchi na kuwadidimiza watu wa kipato cha
chini wengi wao wakiwa ni wakulima,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Ndugu
zangu ngojeni niwaulize swali, wakati wa utawala wa Mwinyi na Mkapa
(marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa), ni kipindi gani
maisha yalikuwa mazuri?” Wananchi wakajibu (kipindi cha Mwinyi). Miaka
10 ya uongozi wa Mkapa na miaka saba ya Kikwete, ni kipindi gani maisha
yamekuwa magumu zaidi?" Wakajibu (Kikwete); Je, 2015 wanakuja tena
kutuomba kura huyo atakayekuja si ndiyo itakuwa mbaya zaidi, Chadema
hatuwezi kukubali na moto huu tuliowasha utaendelea nchi nzima hadi
Uchaguzi Mkuu wa 2015 na kama CCM itasalimika nitajiuzulu siasa.”
Mbowe
alikishambulia CCM akidai kimepoteza mwelekeo uliowekwa na waasisi
wake, chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere wa kuzingatia usawa,
udugu huku kikijikita katika msingi wa kutetea wakulima wanyonge na
wafanyakazi lakini sasa kimewagawa wananchi katika matabaka ya walio
nacho na wasio nacho.
“CCM ya Mwalimu Nyerere ilijali wakulima na
wafanyakazi wa kipato cha chini, ilijenga mshikamano baina ya
Watanzania wote bila kujali ukabila. Tanzania ina makabila zaidi ya 120,
lakini tunaishi kama mtu na ndugu yake, leo taifa limegawanyika vipande
huku maadili ya uongozi yakiporomoka,” alisema Mbowe.
Katika
mkutano huo uliokutanisha viongozi wote wa kitaifa wa chama hicho, Mbowe
alisema kwa sasa CCM kimevuruga hata mitalaa ya elimu huku akituhumu
watunga sera kuwa wanafanya hivyo makusudi kwa kuwa watoto wao hawasomi
katika shule hizo.
“Mwalimu alijenga CCM iliyozingatia usawa,
watoto wote walisoma shule moja, mimi nilisoma na watoto wa Mwalimu
Nyerere, mawaziri na wakulima katika shule hiyo, leo watoto wa mkulima
wanasoma shule za kata ambazo hazina walimu, vitabu, maabara wala
library (maktaba), wakati watoto wa vigogo wakisoma nchi nje na wale wa
wakuu wa wilaya wakisoma shule za (academy),” alisema Mbowe.
Aliwataka
wakazi wa mikoa ya kusini, Lindi na Mtwara kuunganisha nguvu kwa lengo
la kukiondoa CCM madarakani katika chaguzi zote ukiwamo mkuu wa 2015.
“Ndugu
zangu wa Masasi, mimi Mbowe ninatimiza miaka 21 nikiongoza siasa za
upinzani zenye lengo la kuleta ukombozi wa kweli kwa Taifa hili,
nimefunguliwa kesi za uchochezi tisa hadi leo, lakini sitaacha harakati
hata wakinifunga, bado nitaendelea na harakati za ukombozi hadi
Watanzania watakapofikia kwenye uhuru wa kweli,” alisema Mbowe.
Kwa
upande wake, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa alieleza
kusikitishwa kwake na umaskini unaoukabili Mkoa wa Mtwara licha ya
kuwapo rasilimali nyingi zinazouzunguka ikiwamo gesi na korosho.
Alisema
kumekuwa na ufisadi mkubwa unaofanywa katika ununuzi wa korosho na
licha ya wananchi kukatwa Sh30 katika kila kilo wanayouza, bado mikoa
hiyo ya kusini inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji, huduma
muhimu za kijamii kama zahanati na shule.
“Taifa linaweza
kuendelea ikiwa rasilimali za nchi ambazo zinatoka kwa wananchi
zitawarudia na kutumika katika kuendeleza miradi ya maendeleo. Leo
mnakatwa Sh30 katika kila kilo moja ya korosho mnayouza, tumetafuta ni
kiasi gani cha korosho kimepatikana kwa mwaka hapa nchini lakini taarifa
hizo hatuzipati.”
“Lakini taarifa tulizopata Ulaya zinasema
Tanzania imeuza tani 157,000 kwenye soko la dunia, haya mabilioni ya
fedha mnazokatwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinatumika wapi?”
alihoji na kuongeza kuwa fedha hizo zinastahili kudaiwa. |
No comments:
Post a Comment