Thursday, June 28, 2012

Mgomo: MOI huduma zasimama


Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Namala Mkopi
Mgomo wa madaktari katika hospitali za serikali nchini umeingia siku ya tano huku Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi ikimwamuru Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Namala Mkopi, awatangazie madaktari hao wasitishe mara moja mgomo huo.

Jaji wa Mahakama hiyo, Lusekela Moshi, ametoa amri hiyo jana na kueleza kuwa Rais wa MAT anatakiwa kuwatangizia madaktari kupitia vyombo vya habari wasitishe mgomo huo hadi Julai 24, mwaka huu siku ambayo kesi ya madaktari itakaposikilizwa na kutolewa maamuzi.


Alisema jalada linalowataka madaktari kusitisha mgomo tayari limekwisha kupelekwa kwa Rais wa MAT Jumatatu wiki hii na kwamba kinachosubiri ni rais huyo kuwajulisha wananchama hao wasikaidi amri ya mahakama.

Jaji Moshi alisema mahakama inamtambua Rais wa MAT kuhusika katika mgomo huo kwa sababu awali alisikika akizungumza na vyombo vya habari kwamba madaktari watagoma.

Rais wa MAT, Mkopi alipotafutwa na NIPASHE kutoa maelezo kuhusiana na utata huo aliahidi kuzungumza na vyombo vya habari leo kulitolea ufafanuzi.

Hata hivyo, Mkopi hivi karibuni alikaririwa na vyombo vya habari kuwa chama chake hakihusiki kuitisha mgomo huo na kwamba wanaohusika ni Jumuiya ya Madaktari Tanzania.

Wakati mahakama ikitoa amri hiyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka, juzi alipozungumza na gazeti hili alisema madaktari wataendelea na mgomo bila kikomo kwa sababu hawajapokea hati ya zuio la mgomo huo kutoka mahakamani.

Dk. Ulimboka alisema madaktari hawawezi kupuuza amri ya mahakama, lakini kwa kuwa zuio hilo halijapelekwa rasmi kwao wataendelea na mgomo kama kawaida.

Siku mbili baada ya madaktari kutangaza kuanza mgomo, serikali ilikimbilia Mahakama Kuu kitengo cha Kazi na kufanikiwa kuweka zuio la mgomo.

Wakati malumbano hayo yakiendelea, hali ya utoaji wa huduma katika hospitali mbalimbali za serikali nchini imeendelea kuwa tete na hivyo kusababisha kero kubwa kwa wagonjwa.

MOI YAFUNGWA

Katika Taasisi ya Mifupa (MOI) huduma za matibabu zimesitishwa rasmi kutokana na madaktari kugoma kuingia kazini.

Maeneo ambayo utoaji wa huduma umesitishwa ni kitengo cha upasuaji na wodi maalumu ya wagonjwa binafsi (private).

Ofisa Habari wa MOI, Jumaa Almasi, akizungumza na waandishi wa habari jana alisema huduma katika maeneo hayo zimesitishwa kutokana na madaktari kutofika kazini.

Alisema hata hivyo kitengo cha dharura na huduma za maabara kinaendelea kupokea wagonjwa ambako madaktari viongozi wanaendelea kuwahudumia wagonjwa kama kawaida.

“Kwa kawaida tunakuwa na madaktari 73 lakini kwa siku hizi nne zilizopita mpaka leo mahudhurio yamepungua, siwezi kusema wamefikia wangapi, lakini idadi ya madaktari ni ndogo,” alisema Almasi.

Wagonjwa waliolazwa katika taasisi hiyo wakisubiri matibabu walisema hawajapata huduma kabisa tangu juzi na kwamba wauguzi wamekuwa wakiwaeleza kuwa madaktari hawapo.

Robert Mrope, mmoja wagonjwa anayesumbuliwa na mguu alisema alitakiwa kupigwa X-RAY Juni 21, mwaka huu lakini kila akifika hospitalini hapo anaambiwa daktari hayupo.

MUHIMBILI 

Katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) idadi kubwa ya madaktari hawajafika kazini na kusababisha wagonjwa kukosa huduma.

Johari Mkonde mgonjwa aliyelazwa katika wodi ya Kibasila alisema tangu asubuhi hakuna daktari aliyepita kutoa matibabu ila wauguzi ndio wanaowahudumia kwa kuwapa huduma ya kwanza.

Mkonde aliiomba serikali kumaliza mgogoro uliopo baina yao na madaktari kwani wanaoumia ni wagonjwa na siyo madaktari.

Baadhi ya ndugu za wagonjwa walionekana wakiwachukua wagonjwa wao na kuwarudisha nyumbani, huku wakitoa maneno makali wakisema “Ni heri kuishi bila viongozi  kuliko serikali isiyowajali wananchi wake.”

Ofisa Habari wa Muhimbili, Aminieli Aligaesha, ambaye tangu mgomo huo uanze Juni 23 mwaka huu amekuwa nadra kupatikana kuelezea tatizo hilo amekuwa hapatikani na hata simu yake akipigiwa inaita tu bila kupokewa.

AMANA, MWANANYAMALA, TEMEKE 

Hali ya utoaji wa huduma za matibabu katika Hospitali ya Manispaa ya Ilala ya Amana, jijini Dar es Salaam imezidi kuwa mbaya kutokana na madaktari kutokuwepo kazini.

Kutokana na tatizo hilo NIPASHE ilishuhudia msururu wa wagonjwa wakisubiri matibabu bila mafanikio katika mabenchi ya kusubiria kwenye vyumba vitatu vilivyokuwa na madaktari huku vyumba vingine vikiwa havina madaktari.

Cecilia Christian mmoja wagonjwa aliyekutwa hospitalini hapo, alisema kitendo cha kuingia kwa daktari na kuandikiwa dawa bila ya kuulizwa anaumwa nini na kisha kuambiwa akanunue hakifai kabisa na kutaka serikali iingie kati suala hilo.

“Mwandishi, tiba sijui unaweza ukasema nimepewa au nimepewa nusu, kwa sababu nilipoingia kwa daktari, alichofanya alinyosha mkono na kuchukua kadi yangu na kisha akaniandikia dawa bila hata ya kuniuliza ninachoumwa wala bila ya kunifanyia vipimo vyovyote,” alisema.

Mgonjwa mwingine jina tunalihifadhi alikataliwa kutibiwa na daktari mwanamke aliyekuwa chumba cha matibabu namba 21 kwa maelezo kuwa alikuwa na mambo ya kifamilia ya kuyashughulikia nyumbani kwake.

Hali hii iliwafanya ndugu zake waliokuwa wameongozana naye walie na huku wakisaidiana na muuguzi mmoja aliyekuwa amempokea kwenye kitanda cha hospitali, walimutoa na kumpeleka chumba cha matibabu namba 22 kilichokuwa na daktari mwanaume ambaye alikubali kumhudumia.

Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. Shani Mwaluka, alisema asilimia 50 ya madaktari katika hospitali hiyo wamegoma na kusababisha huduma ya wagonjwa wa nje ambao siyo wa kulazwa kusimamishwa na kuendelea kutoa huduma ya dharua.

“Unajua kuwa siyo siri, madakatari wamegoma na inapaswa waandishi kuandika hali halisi na siyo kuweka chumvi wakati hali hiyo inafahamika kwa wananchi wote,” alisema Mwaluka.

Katika hospitali ya Mwananyamala pamoja na huduma kuendeela, hata hivyo baadhi ya madaktari walikiri kuzidiwa na kazi baada ya wale  wa mafunzo ya vitendo na wa kawaida kuingia kwenye mgomo.

Daktari bingwa wa upasuaji ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema wao wanaendelea na huduma kama kawaida kwa madaktari wachache wanaoendelea na kazi.

Regina Richard, mkazi wa Musoma ambaye alifanyiwa upasuaji kutokana na mimba kutungwa nje ya mfuko wa uzazi, alisema tangu alazwe hapo wiki mbili zilizopita amekuwa akipatiwa matibabu na afya yake iliendelea kuimarika hadi siku hiyo aliporuhusiwa kurudi nyumbani.

MBEYA MADAKTARI WAPIGWA MEMO

Serikali mkoani Mbeya imetishia kusitisha mikataba ya madaktari waliogoma katika hospitali za serikali za mkoa huo hasa wale ambao wako kwenye mafunzo ya vitendo kama hawatarejea kazini.

Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Norman Sigalla, alisema jana kuwa bodi imefikia hatua hiyo baada ya kuona madaktari hao wamevunja mkataba wao ambao unawataka kufanya kazi bila kugoma.

“Bodi imekaa na kugundua kuwa mkataba umevunjwa, hivyo tumewaandikia barua kila mmoja ili ajieleze kwa nini asichukuliwe hatua kwa kuvunja mkataba tuliokubaliana naye,” alisema Dk. Sigalla.

Dk. Sigalla ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, alisema kabla ya kuwaandikia barua hiyo, juzi bodi ya Hospitali ilikutana na kuwawaita madaktari wote kwa barua ili wakae nao na kuwasikiliza, lakini hakuna daktari hata mmoja aliyejitokeza kwenye kikao.

Alisema kwa mujibu wa sheria za kazi mtumishi asipofika kazini kwa muda wa siku tatu mfululizo anakuwa amejifuta kazi mwenyewe, hivyo kama madaktari hao hawataripoti kazini kufikia leo, watalazmika kuwaondoa na kuwarejesha kwa Katibu Mkuu wa Wizara ambaye ndiye aliwatuma kwenda kufanya mazoezi ya vitendo hospitalini hapo.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Mbeya, Dk. Eliuter Samky, alisema kimsingi mgomo huo umeathiri utoaji wa huduma katika hospitali hiyo.

Dk. Samky alisema Jumamosi ambayo ilikuwa siku ya kwanza ya mgomo huo, hospitali ilipokea wagonjwa 42 waliostahili kulazwa, Jumapili wagonjwa 53 na juzi Jumatatu ilipokea wagonjwa wa nje (OPD) 283 ambao wote waliathirika kwa kupata huduma za kiwango cha chini.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Seif Mhina, alisema baada ya huduma kusuasua katika Hospitali ya Rufaa ya wazazi Meta, kina mama wanaohitaji kujfungua wote wamekuwa wakielekea kwenye hospitali ya mkoa, jambo ambalo limeifanya kuelemewa na wagonjwa.

KCMC
Hali ya utoaji wa huduma za afya katika hospitali ya Rufaa ya KCMC imezorota baada ya madaktari walio kwenye mafunzo kwa vitendo kugoma na kuondoka kabisa katika eneo la hospitali hiyo.

Jumatatu hali haikuonekana mbaya sana kwa kuwa madaktari walikubali kuendelea na baadhi ya kazi kwa kuangalia wagonjwa wa nje wenye hali mbaya zaidi, huku wakiisikilizia serikali kuwa inachukua hatua gani, lakini baada ya kuona hakuna hatua yoyote hadi sasa wameamua kugoma kabisa.

Taarifa kutoka kwa mmoja wa madaktari ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini, alisema wameamua kuendelea kuwahudumia wagonjwa waliozidiwa na dharura nyingine kama majeruhi wa ajali na wajawazito.

“Jana ilionekana tunaendelea na kazi, kutokana na kwamba tuliamua kuangalia waliozidiwa na ambao wangeachwa wangekufa tuliwapa huduma, wale ambao ukiwaangalia wana maumivu ila hawawezi kufa bali watateseka tu, tuliwarudisha, ili tusikilizie serikali yetu inasemaje, tumeona haijali nasi tumeamua kuachia kabisa,” alisema daktari huyo.

Alisema kwa siku ya jana (leo), kliniki zote hazifanyi kazi huku madaktari walio kwenye mfunzo ya vitendo (Interns), wakiwa wameacha kufanyakazi kabisa.

Alisema lengo ni kuishinikiza serikali kutimiza madai yao ambayo ni vifaa tiba, dawa na huduma kwenye hospitali, ikiwa ni pamoja na viongozi kuacha kwenda kutibiwa nje ya nchi baada ya kuboresha huduma nchini.

“Tumegundua tunayegombana naye hana huruma na wananchi wake na anayeteseka ni mwananchi, hivyo kwa KCMC tutaendelea kuwahudumia wagonjwa waliolazwa na waliozidiwa tu," alisema.

Alipoulizwa na NIPASHE juu ya mgomo huo, Mwenyekiti wa Interns, Dk. Petro Arasumin, alisema ni kweli wapo kati ya 70 na 80, na wamekubaliana kutoendelea na kazi baada ya kukaa katika kikao maalum cha pamoja juzi jioni.

KIGOMA WACHAPA KAZI

Madaktari wa Mkoa wa Kigoma ya Maweni jana hawakugoma badala yake walikuwa wakiendelea kutoa huduma kwa wagonjwa.

Akizungumza na NIPASHE jana ofisini kwake Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Leonard Sudi alisema kuwa: “Sisi katika mkoa wetu hatuna mgomo, madaktari na wauguzi wanaendelea na  kazi kama kawaida.”

Sudi alisema Mkoa wao haujawahi kukumbwa na mgomo wa madakatari kama ilivyo kwa mingine nchini.

Aliwataka wananchi kama hawatapatiwa huduma zinazostahili kutoa taarifa ili hatua kali zichukuliwe.

Imeandikwa na Thobias Mwanakatwe, Gwamaka Alipipi, Raphael Kibiriti, Isaya Kisimbilu, Nebart Msokwa, Leonce Zimbandu, Hadija Kitwana, Jacqueline Yeuda, Dar; Salome Kitomari, Moshi; Emmanuel Lengwa, Mbeya na Joctan Ngelly, Kigoma.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment