Saturday, July 7, 2012

Waasi Mali wawaingiza watoto vitani


Wapiganaji wa kundi la Ansar Dine kaskazini mwa Mali

Umoja wa Mataifa umesema watoto nchini Mali wamekuwa kidhalilishwa kingono na wengine kuchukuliwa na waasi na kuingizwa kwenye mapigano.
Mfuko wa watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF, umesema wanamgambo wa Kiislam kaskazini ya nchi hiyo wamewalazimisha na kuajiri wavulana karibu 175 wenye umri wa miaka 12 hadi 18.

UNICEF imesema inao ushahidi ambao pia wasichana wadogo nao wamekuwa wakibakwa na kudhalilishwa kijinsia.
Mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika nchini Mali mwezi Machi 2012, yametoa mwanya kwa wapiganaji wa Kiislam kuchukua udhibiti wa kaskazini mwa nchi hiyo.


Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limesema alhamisi kuwa haikuwa tayari kuunga mkono Umoja wa nchi za Afrika Magharibi kutumia nguvu kuingilia mzozo kaskazini mwa Mali, lakini badala yake lilipitisha azimio la vikwazo dhidi ya makundi hayo ya wapiganaji.
UNICEF imesema pamoja na unyanyasaji na matumizi ya watoto kama wapiganaji, watoto pia wameuawa kwa mabomu ya mikono.
UNICEF limezidi kusema kiasi cha watoto 300,000 wameathirika na shule zimefungwa katika maeneo yenye mapigano.
Tangu waasi walipoteka na kuudhibiti eneo la kaskazini ya Mali, watoto wengi wamekuwa wakiishi katika makambi ambapo wanakabiliwa na uhaba wa chakula, UNICEF limesema.
Umoja wa Mataifa umesema taarifa walizowasilisha zinaonyesha picha ndogo tu ya mambo yalivyo kwa vile ilikuwa ni hatari kwa kufanya utafiti wa kina kaskazini mwa Mali.
UNICEF imesema ilikuwa ikifanya kazi na washirika katika baadhi ya maeneo ya nchi kujaribu kusaidia jamii kuwalinda watoto.
"Watoto katika eneo la kaskazini wameshuhudia na wamekuwa waathirika wa unyanyasaji ni lazima walindwe" alisema Theophane Nikyema, Mwakilishi wa UNICEF nchini Mali.
Mgogoro unaoendelea nchini Mali umeshuhudia mashambulizi kwenye misikiti na makaburi katika mji wa kihistoria wa Timbuktu uliofanywa na wapiganaji kiislamu la Ansar Dine.
Ansar Dine kundi ambalo linasema lina uhusiano na al-Qaeda limesema lengo lao ni kuharibu makumbusho yote yanayokwenda kinyume na sharia za Kiislamu.
Kundi hilo la Ansar Dine waliliuteka na kuudhibiti mji wa Timbuktu mwezi Aprili mwaka huu.

No comments:

Post a Comment