MAMLAKA
ya Kudhibiti Chakula na Dawa Nchini Marekani (FDA), imethibitisha na
kupitisha matumizi ya kifaa kipya cha kupima Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa
kutumia mate.
Kifaa hicho kilichotengenezwa na wanasayansi wa
nchini humo, kimeelezwa kuwa na uwezo wa kutoa majibu sahihi kwa zaidi
ya asilimia 90 kwa kati ya dakika 20 na 40 baada ya kupima. Imeeleza
kuwa kifaa hicho kilichopewa jina la OraQuick, kimebuniwa sio tu kwa
ajili ya matumizi ya hospitalini bali pia nyumbani na kitaanza
kupatikana katika maduka ya dawa nchini Marekani kuanzia Oktoba mwaka
huu kabla ya kusambazwa nchi mbalimbali duniani.
Serikali ya
Marekani imesema inaamini kifaa hicho kitasaidia kupunguza maambukizi ya
virusi vya ukimwi kwa kubadili tabia ya watu wanaoishi na virusi hivyo
bila kujua. Wataalamu mbalimbali wa afya wamekielezea chombo hicho
kuwa ni hatua nyingine kwa dunia katika jitihada zake za kudhibiti
maambukizi ya VVU . Kinavyotumika Kwa umbo OraQuick hakina
tofauti na vipimo vingine vya kisasa ambavyo vimebuniwa kwa ajili ya
kupima magonjwa kwa haraka kama vile malaria, Ukimwi na kisukari. Lakini
badala ya kuwa na sehemu ya kudondoshea tone la damu, kina sehemu laini
iliyojitokeza, maalumu kwa ajili ya kunyonya mate.
Mtumiaji
hapaswi kukitemea mate, bali kwa kutumia sehemu hiyo maalumu,
atakiingiza kifaa hicho mdomoni na kuchukua mate katikati ya fizi na
midomo chini au juu.
Sehemu hiyo laini italoa mate na kuyanyonya.
Hapo mpimaji atapaswa kukiondoa kifaa hicho na kukiweka sehemu kavu
kusubiri kimpatie majibu ndani ya muda huo wa kati ya dakika 20 na 40.
Gharama zake Hakuna
uhakika juu ya bei kamili ya kipimo hicho. Taarifa za awali zinaonyesha
kuwa kitauzwa kwa Dola za Marekani 17.50 sawa na Sh 27,300.
Taarifa
zinaonyesha kuwa OraQuick itaanza kuuzwa Marekani na kusambazwa maeneo
mbalimbali duniani na mtu yeyote ataweza kukiagiza kwa njia ya mtandao.
Moja ya masharti yaliyowekwa na FDA ni kwamba kipimo hicho kitauzwa kwa watu wenye umri wa miaka 17 au zaidi.
Kauli ya wataalamu Mkurugenzi
wa Taasisi ya Kupambana na Magonjwa ya Kuambukiza na Mzio (NIAID)
Profesa Anthony Fauci alisema watafiti wa magonjwa wanaendelea kupiga
hatua ya kudhibiti Ukimwi. Alisema kipimo cha OraQuick ni moja ya
hatua muhimu ambayo wanasayansi wamekuwa wakihangaika nayo usiku na
mchana katika jitihada zao za kupata vipimo rahisi na tiba.
Alisema jitihada za wanasayansi hao katika kupambana na Ukimwi zimewezesha kudhibiti maambukizi ya VVU kwa asilimia 96.
Daktari
aliyegundua Mmarekani wa kwanza mwenye VVU mwaka 1984, Dk Robert Gallox
alisema hatua ya FDA kupitisha kipimo hicho itasaidia kupunguza kasi ya
kuenea kwa virusi hivyo duniani.
|
No comments:
Post a Comment