Saturday, June 23, 2012

Mshirika wa Al-Shabaab arejeshwa Ujerumani

Raia wa Ujerumani, Emrah Erdogan (24)
 
Raia wa Ujerumani, Emrah Erdogan (24), aliyekamatwa jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za ugaidi amerejeshwa nchini Ujerumani baada ya kuhojiwa na Jeshi la Polisi Nchini.

Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Naibu Kamishina wa Polisi, Issaya Mngulu, aliliambia NIPASHE jana kuwa Erdogan au kwa jina lingine Abdulrahman Othuman, alirejeshwa nchini humo Jumatatu wiki hii.

Hata hivyo, hakufafanua kama jeshi hilo litahusika katika kumchukulia hatua au la, badala yake, alisema amerejeshwa Ujerumani ili kuchukuliwa hatua zaidi za kisheria kuhusiana na tuhuma za ugaidi zinazomkabili nchini humo.

Alisema mtuhumiwa huyo alipelekwa Ujerumani bila masharti yoyote na kwamba, Tanzania imeamua kufanya hivyo kwa sababu ni mtu, ambaye hatakiwi nchini.

Juni 13, mwaka huu, Mngulu alikaririwa akisema makachero wa jeshi hilo kwa kushirikiana na wenzao wa Ujerumani, Kenya na Uganda walikuwa wakiendelea kumhoji mtuhumiwa huyo.
Alisema mtuhumiwa huyo, ambaye ni mzaliwa wa Uturuki, makazi yake yapo Ujerumani.
Alisema taarifa walizozipata ni kwamba, mtuhumiwa huyo ni mpiganaji wa kikundi cha kigaidi cha Al-Qaeda, aliyeshiriki mapambano kadhaa nchini Afghanistan.

Mngulu alisema taarifa za awali zinaonesha kwamba hivi karibuni alikuwa nchini Somalia ambako alikuwa akishirikiana na kikundi cha Al-Shabaab.

No comments:

Post a Comment