Saturday, June 23, 2012

Wanafunzi DUCE wavamia Bodi ya Mikopo

Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE)
 
Wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE), jijini Dar es Salaam, jana walivamia ofisi za Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), wakidai kupewa pesa zao za mazoezi kwa vitendo.
NIPASHE, ambayo ilifika katika ofisi hizo, iliwashuhudia wanafunzi hao zaidi ya 100 wakiwa nje wakilalamikia kutopewa pesa hizo, huku wakitarajia kuripoti katika vituo vyao vya kazi Juni 25, mwaka huu.

Wanafunzi hao wa mwaka wa kwanza na wa pili katika chuo hicho, walichukua uamuzi huo baada ya majina yao kutoonekana katika orodha ya wanafunzi wanaotarajiwa kupewa pesa za mazoezi hayo.
Witness Kyando, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili anayesomea masomo ya sayansi katika chuo hicho, alisema zaidi ya wanafunzi 200 hawajapewa pesa zao, huku siku ya kuripoti vituo vyao vya kazi imekaribia.
Alisema walifika katika ofisini hizo jana asubuhi na kuonana na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, ambaye aliwataka wasubiri kwa madai kwamba, tatizo lao linashughulikiwa.
Afisa Habari wa HESLB, Veneranda Malima, alisema alithibitisha wanafunzi hao kuvamia ofisi za bodi hiyo na kusema taratibu za kulipatia ufumbuzi tatizo hilo zinaendelea.

No comments:

Post a Comment