Saturday, June 23, 2012

Walimu wajiandaa kugoma


Maandalizi ya mgomo wa walimu uliopangwa kufanyika hapa nchini yamezidi kupamba moto ambapo waraka maalum umeanza kusambazwa na Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kwa wanachama wake wote nchi nzima ili kuhamasishana.

Mgomo huo umepangwa kufanywa na walimu Julai 7, mwaka huu ili kuishinikiza serikali kuwaongeza mishahara, kuwalipa posho mbalimbali pamoja na kuwalipa malimbikizo ya madeni.

Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Dar es Salaam, Zubeda Aziz, alisema jana kuwa walimu kipindi hiki tofauti na wakati mwingine wowote hawatakuwa na uoga wala kuogopa vitisho vya serikali.


Aidha, Aziz alisema walimu wote wameanza kusamabaziwa vitabu vya sheria za kazi ili wavisome kwa ajili ya kuwasaidia kujua taratibu zinazowalinda wasifukuzwe kazi wala kutishwa na serikali watakapokuwa katika mgomo.

“Kila mwalimu ameanza kusambaziwa waraka maalum ambao unamtaka kushiriki mgomo huo na kumtaka asiwe muoga wala kuhofia vitisho vya serikali,” alisema na kuongeza:

“Madai ya walimu ni ya siku nyingi, lakini kwa bahati mbaya serikali imekuwa ikituzungusha na kutuona kama vile hatuna akiri sawa sawa ndiyo maana inashindwa kutulipa.”

Alisema walimu wanataka kulipwa nyongeza ya mshahara kwa asilimia 100,  kulipwa posho kwa ajili ya kufundisha katika mazingira magumu na posho ya kufundisha masomo ya sayansi na sanaa.

Alisema serikali imekuwa na kawaida ya kuwalazimisha walimu kugoma na kwamba kipindi kilichopita walipogoma ilitatua kidogo madai yao.

No comments:

Post a Comment