MVUVI
wa samaki katika kijiji cha Butata kata ya Bukima Wilayani Msoma
Vijijini mkoani Mara, Stephano Mboyi amenusurika kutafunwa na mnyama
aina ya kiboko, baada ya kupambana naye ana kwa ana na kumshinda
maarifa.
Tukio hilo ambalo kwa kadri Mboyi mwenyewe
alivyolisimulia lilionekana kama ni filamu ya kusisimua ya mpambano
baina yake na mnyama huyo hatari lilitokea Jumatatu majira ya saa moja
za usiku ziwani.
Akiongea na Mwananchi kwa njia ya simu kutokea
katika Hospitali ya Murangi alikolazwa kwa matibabu baada ya kujeruhiwa
na mnyama huyo wakati wa pambano hilo, Mboyi alisema alikumbana na tukio
hilo wakati akifanya shughuli zake za uvuvi.
“Nilikuwa
nimekwenda kutega mtego (nyavu) wangu wa kwa ajili ya samaki aina ya
furu. Baada ya kumaliza kuuzungusha, nilianza kuwafukuza samaki kuelekea
kwenye mgeto;
“Ghafla nikasikia maji yakifoka kunifuata, nikajua
huyo ni kiboko nimeshapatikana. Hivyo ilinibidi nizame ndani ya maji
ili nikimbie kando lakini kiboko akataka kunikanyaga, bahati nzuri
nikawahi kupita miguuni mwake na nikaenda mbele,” alisema Mboyi.
Aliongeza
kuwa wakati anatapatapa akitafuta namna ya kukimbia kutoka ndani ya
maji mara kiboko huyo akamsukuma akaanguka na akataka kumkamata mgongoni
lakini akakwepa na kuamua kukimbilia kwenye maji marefu.
Aliendelea
kusimulia kuwa kiboko huyo alimfuata tena na katika harakati za
kupambana naye mara kiiboko akaudaka mkono wake wa kushoto na kuingiza
mdomoni mwake.
“Baada ya mkono kuingia mdomoni aliachama zaidi ili
anikamate kichwani na kisha anitafune lakini nikamshika kidevu
nikamsukuma nikauchomoa haraka mkono wangu kisha nikazama majini,”
alieleza Mboyi.
Alisema hatua ya kuzama majini ndiyo iliyokuwa
ikimsaidia hivyo aliendelea kuhangaishana na kiboko huyo hata baada ya
kuweza kuudaka mkono wake katika kinywa chake kama mara tatu hivi lakini
alifanikiwa kujinasua kabla hajatafunwa.
Mboyi alisema kuwa wakati akiendelea kupambana na kiboko huyo watu wakafika ziwani hapo wakiwa na tochi baada ya kusikia kelele.
Alisema
yule kiboko alipoona ule mwanga wa tochi, alimwacha yeye kisha
akawatisha kuwafukuza wale watu waliokuwa na tochi nao wakakimbia na
kisha akamrudia tena na kuanza kusumbuana.Hata hivyo wale watu walirudi
tena na kutumia mwanga mkali kummulika kiboko huyo ambapo mara hiyo sasa
yule kiboko alimuacha, akasogea nyuma kidogo kisha likawatisha tena
kuwafukuza.
Alieleza kuwa hapo ndipo alipopata nafasi ya kukimbia
hadi ufukweni upande mwingine, ambapo alikimbia na kiboko huyo kuanza
kumfukuzatena, ambapo baada ya mwendo mfupi alianguka ndipo alipobaini
kuwa alikuwa amesharudi kwenye maji.
Aliongeza kuwa baada ya hapo ndipo wale watu waliokuwa na tochi walipomfuata na kumchukua na kisha kumpeleka hospitali.
Hata
hivyo alisema kuwa katika pambano hilo aliweza kupata majeraha katika
mkono wake wa kushoto tu ambao kiboko huyo alikuwa akiudaoa na kuuingiza
kinywani mwake, wakati wa harakati za kujinasua kuutoa mdomoni mwake. |
|
No comments:
Post a Comment