MAWAKILI
wa Serikali jana waliwasilisha vielelezo Mahakama kuu kuthibitisha
kwamba umri wa msanii wa filamu Elizabert Michael ni zaidi ya miaka
18.Habari zilizolifikia gazeti hili na kuthibitishwa na mawakili wawili;
mmoja wa Lulu na mwingine wa Serikali ambao hawakutaka kutajwa,
zimeeleza kuwa vielelezo hivyo vimewasilishwa jana mahakamani hapo.
Habari
zimeeleza kuwa moja ya vielelezo hivyo vya Jamhuri ni Mkanda wa video
aina ya CD, yenye mahohjiano kati ya mshtakiwa huyo na mtangazaji mmoja
nchini.
"Vingine ni maelezo ya mshtakiwa huyo aliyoyatoa polisi
wakati alipohojiwa kuhusu tuhuma zinazomkabili, maombi ya hati ya
kusafiria (Passport) na maombi ya leseni ya udereva, alisema mmoja wa
mawakili hao.
Awali vielelezo hivyo walitakiwa kuviwasilishwa juzi, lakini ilishindikana na badala yake vikawasilishwa jana.
Baada
ya vielelezo kesi hiyo itasikilizwa Juni 25 mwaka huu. Lulu anakabiliwa
na kesi ya mauaji katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akituhumiwa
kumuua msanii mwenzake, Marehemu Steven Kanumba aliyefariki dunia
nyumbani kwake Sinza, April 7, 2012.
Hata hivyo umri wake
umezua utata baada ya mawakili wake wanaomtetea kudai kuwa bado ni mtoto
kwa kuwa ana umri wa miaka 17 na si 18 kama hati ya mashtaka
inavyoonyesha.
Hivyo mawakili hao walilazimika kuwasilisha
maombi mahakamani kuiomba mahakama iruhusu ufanyike uchunguzi wa umri
sahihi wa mshtakiwa huyo na ikiridhika kuwa ni mtoto basi kesi yake
iendeshwe kwa misingi ya kesi za watoto wanaokinzana na sheria ili
kulinda maslahi yake.
Juni 11, 2012 Mahakama Kuu ilikubali
yenyewe kufanya uchunguzi huo kwa lengo la kubaini usahihi wa umri wa
mshtakiwa huyo na ikaziagiza na kuzipangia tarehe pande zote katika kesi
hiyo kuwasilisha mahakamani hapo vielelezo watakavyovitumia katika hoja
zao.
Jopo la mawakili wanaomtetea Lulu likiongozwa na Kennedy
Fungamtama Juni 13 waliwasilisha mahakamani hati za viapo vya wazazi
wake na vielelezo vingine kikiwemo cheti cha kuzaliwa na cha ubatizo
vinavyoonesha kuwa bado ni mtoto.
Lakini taarifa zilizopatikana
mahakamani hapo zinaeleza kuwa vielelezo vilivyowasilishwa na Jamhuri
vinaonesha kuwa mshtakiwa huyo ni mtu mzima kwa kuwa kwa mujibu wa
vielezo hivyo ana umri zaidi ya miaka 18.
Viapo vya wazazi wa
mshtakiwa huyo vilivyowasilishwa mahakamani hapo na Makamu wa Rais wa
Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Peter Kibatala ambaye ni mmoja wa
mawakili wanaomtetea Lulu vinaeleza kuwa mshtakiwa huyo ana umri wa
miaka 17.
Viapo hivyo ambavyo Gazeti hili limefanikiwa kuviona
ni kiapo cha mama yake Lulu Lucresia Augustin Kalugila, mkazi wa Dar eS
Salaam na kiapo cha baba mzazi Michael Kimemeta, mkazi wa Moshi.
Viapo
vyote vinaeleza kuwa mshtakiwa huyo alizaliwa April 16, 1995 katika
kituo cha Afya Muhimbili na kupewa cheti cha kuzaliwa namba B.0318479
cha Julai 23, 2004.
Pia viapo hivyo vinaeleza kuwa baada ya kuzaliwa
mshtakiwa, mama yake alimpa jina la Diana Michael Kimemeta, lakini
alimpeleka mtoto huyo Moshi mkoani Kilimanjaro kwa ndugu zake, walimpa
jina la Elizabeth, jina la bibi yake Elizabeth Shikana.
Viapo
hivyo vinaendelea kueleza kuwa baada ya majadiliano wote, yeye mama,
baba na ndugu wengine walikubaliana kuwa wamuite Diana Elizabeth Michael
Kimemeta .
“ Elizabeth Michael Kimemeta alibatizwa katika
Kanisa la Katoliki Chang’ombe Septemba 28, 1997 na alichukua majina ya
ubatizo Diana Elizabeth Michael Kimemeta;” inasomeka sehemu nyingine ya
kiapo hicho cha mama wa mshtakiwa.
Utata wa umri wa mshtakiwa
huyo uliibuka Mei 7, 2012 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada
ya wakili wake Fungamtama kudai kuwa ana miaka 17 na hivyo kuomba kesi
yake isikilizwe katika mahakama ya watoto.
Hata hivyo Mahakama
ya Kisutu iliyakataa maombi hayo ikisema kuwa haina mamlaka ya
kuyashughulikia na kushauri maombi hayo yawasilishwe Mahamaka Kuu.
Ndipo
Mei 15 wakili Kibatala aliwasilisha maombi hayo mahakama kuu wakiomba
mahakama hiyo iamuru kwamba Mahakama ya Kisutu ina uwezo wa kisheria
kushughulikia maombi hayo.
Katika maombi hayo namba 46 ya mwaka
2012, pia mawakili hao waliomba Mahakama Kuu kama itaridhika kuwa
mahakama ya Kisutu haina uwezo wa kufanya wala kuagiza uchunguzi huo
ufanyike, basi Mahakama Kuu yenyewe ama iagize au ifanye uchunguzi huo.
Sambamba
na hayo pia waliomba Mahakama Kuu iamuru mwenendo wa kesi ya msingi
katika Mahakama ya Kisutu usimamishwe hadi suala la umri litakapopatiwa
ufumbuzi.
Katika uamuzi wake Jaji Dk. Fauz Twaib alisema kuwa
Mahakama ya Kisutu ina mamlaka ya kushughulikia maombi hayo na kwamba
ilikosea kukataa kuyashughulikia.
Pia Jaji Dk. Twaib
alikubaliana na hoja za pingamizi la awali la wajibu Maombi(Jamhuri)
kupitia kwa Wakili wa Serikali Shadrack Kimaro akisaidiana na Wakili
Elizabeth Kaganda, walizozitoa wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo,
Mei 28,2012.
Wakili Kimaro alidai kuwa maombi hayo
yamewasilishwa mahakamani hapo kinyume cha sheria na kwamba hata vifungu
vilivyotumika katika madai hayo haviipi Mahakama Kuu uwezo wa
kuyashughulikia.
Hata hivyo licha ya kukubali kuwa maombi hayo
yaliwasilishwa mahamakani isivyo sahihi, lakini Jaji Dk. Twaib alisema
bado Mahakama hiyo ina mamlaka ya kuyashughulikia.
Chini ya
kifungu cha 44 cha Sheria ya Mahakama za Hakimu Mkazi, Jaji Dk. Twaib
aliuagiza upande wa mwombaji(mawakili wanaomtetea mshtakiwa),
kuwasilisha mahakamani hati hizo za viapo na vielelezo vya umri wa
mshtakiwa huyo juzi. |
|
No comments:
Post a Comment