Wednesday, May 18, 2016

TRA YABAKIZA SH TRILIONI 2.363 KUFIKIA LENGO


Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Kodi Prof. Isaya Jairo akisisitiza jambo wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya mpango wa mafunzo ya kuhitimu kwa wafanyakazi waliopo kwenye fursa za ajira Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katikati Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kushoto ni Bw. Alphayo Kidata  Kaimu Mkurugugenzi Rasilimali Watu na Utawala Bw. Victor Kimaro. (Picha zote na Eliphace Marwa-Maelezo)
Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Alphayo Kidata (katikati) akionesha kitabu cha mtaala mpya wa mafunzo kwa wafanyakazi (TRA) watakaopata fursa za kusoma katika Chuo cha Usimamizi wa Kodi (ITA), kulia ni Mkuu wa Chuo hicho Prof. Isaya Jairo na kushoto na kushoto ni Kaimu Mkurugugenzi Rasilimali Watu na Utawala Bw. Victor Kimaro. 
Baadhi ya washiriki  waliohudhuria katika uzinduzi wa awamu ya pili ya mpango wa mafunzo ya kuhitimu kwa wafanyakazi waliopo kwenye fursa za ajira Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) uliofanyikia jijini Dar es Salaam. 
Baadhi ya washiriki wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni Rasmi  Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Alphayo Kidata. 

Na Ally Daud- Maelezo.
MAMLAKA ya mapato Tanzania (TRA) imebakiza Tsh. Trilioni 2.363 ili kufikia lengo  waliojiwekea la kukusanya mapato ya trilioni 12.363 katika  mwaka wa fedha 2015/16, ambapo hadi sasa imekusanya kiasi cha Tsh. Trilioni 10.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi  wa awamu ya pili ya mpango wa mafunzo kwa wafanyakazi waliopo kwenye fursa ya ajira za taasisi hiyo  Kamishina Mkuu wa TRA Bw. Alphayo Kidata alisema taasisi yake imefanikiwa kukusanya kiasi cha  sh trilioni 10 katika muda waliojiwekea na kuahidi kumalizia kiasi cha shilingi trilioni 2.363 kabla ya mwaka mpya wa fedha wa Serikali unaoanza mwezi Julai mwaka huu.

“Tumejiwekea malengo ya kukusanya kiasi cha fedha cha shilingi trilioni 12.363 kwa mwaka huu wa fedha na tumefanikiwa kukusanya shilingi trilioni 10 mpaka mda huu ila tunaendelea na kutimiza lengo letu hadi kufikia July mwaka huu na tutajipanga upya mwaka ujao wa fedha kufikia malengo mapema” alisema Bw. Kidata.

Aidha Bw. Kidata amesema kuwa kwa mpango huo wa mafunzo ulioanzishwa kwa  kushirikiana na Chuo cha Usimamizi wa Kodi (ITA) ni mafunzo ya mwaka mmoja yanayoendana na usaili mpya kwa wahitimu ili  kufanya Mamlaka hiyo kuwa na wafanyakazi waadilifu na wachapa kazi ili kupaisha uchumi nchi.

Kwa upande wake Mkuu wa chuo cha cha Usimamizi wa Kodi (ITA) Prof. Isaya Jairo alisema kuwa wameamua kuanzisha mpango huo kwa kushirikiana na Mamlaka ya mapato  ili kufundisha wafanyakazi wa TRA maadili na nyenzo za utendaji kazini  pamoja na kuendesha mafunzo ya dini ili kuwafanya wafanyakazi wawe wacha mungu katika kazi zao.

Aidha Kaimu Mkurugenzi Rasilimali Watu na Utawala wa TRA Bw. Victor Kimaro aliwataka wafanyakazi wote wanatakiwa wafanye kazi kwa maadili hususani upande wa ukusanyaji kodi na Chuo hicho kimewafundisha wafanyakazi hao kufanya kazi kwa ushindani katika maeneo ya kazi ili kuliletea taifa maendeleo yaliyokusudiwa.

No comments:

Post a Comment