Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando
Meneja Mawasiliano wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) inayodhamini tuzo hizo, Imani Lwinga aliwaambia wanahabari jana kuwa uamuzi wa kutoa fedha unalenga kumpa uhuru mshindi atumie fedha hizo vile atakavyo.
“Nia ya kutoa zawadi ni kumfanya mshindi aone ana kitu fulani amepata, hivyo safari hii tumeona tutoe kiasi hicho cha fedha ambacho tunaamini kitakuwa changamoto kubwa kwa mshindi,” alisema Lwinga.
Aliongeza kuwa pendekezo la zawadi ya mshindi kuwa pesa badala ya gari kama iliyotolewa kwa mshindi wa kwanza wa mwaka jana lilitoka kwa TASWA. Mshindi huyo wa jumla atapewa pia cheti na kombe.
Lwinga alisema pia Serengti itatoa zawadi ya Sh. milioni moja kwa kila mshindi wa michezo mbalimbali ambayo itazawadiwa katika sherehe hizo zitakazofanyika Juni 14 mwaka huu kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.
Naye Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando alisema wanatarajia wanamichezo mbalimbali watapewa tuzo siku hiyo na kutaja michezo ambayo itapewa tuzo kuwa ni riadha, wavu, netiboli, kuogelea, tenisi, judo, kikapu, soka, ngumi za kulipwa, ngumi za ridhaa, gofu (ridhaa), gofu (wa kulipwa), baiskeli na kriketi.
Michezo mingine ni mpira wa mikono, olimpiki maalum, Mchezaji Bora wa Nje anayecheza Tanzania, Mchezaji Bora wa Tanzania anayecheza Nje, Mchezaji Bora Chipukizi, Karate, Mwanamichezo Bora wa Tanzania mwaka 2011 na Tuzo ya Heshima.
Mhando ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Tuzo hizo alisema Ijumaa watatangaza majina ya wanamichezo wote watakaowania tuzo hiyo na kuipongeza Serengeti kwa udhamini wao wa kila mwaka.
Mwanamichezo Bora wa Tanzania 2006 alikuwa Samson Ramadhan aliyezawadiwa Sh. 500,000, wakati mwaka uliofuata mshindi Martine Sulle alizawadiwa Sh.500,000, huku mwaka 2008 mshindi akiwa ni Mary Naali ambaye alizawadiwa Sh.750,000. Wote hao ni wanariadha.
Mshindi wa mwaka 2009 alikuwa mchezaji wa netiboli Mwanaid Hassan aliyezawadiwa Sh. Milioni moja na mwaka 2010 pia alikuwa Mwanaid aliyezawadiwa gari aina ya Toyota Cresta GX 100 .
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto aliwashukuru Serengeti na kusema kuwa ana matumaini zawadi hizo itakuwa kichocheo cha wanamichezo kufanya vizuri zaidi.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment