Friday, June 8, 2012

Okwi kuuzwa Austria


Mshambuliaji nyota wa klabu ya Simba na timu ya taifa ya Uganda, Emmanuel Okwi
Mshambuliaji nyota wa klabu ya Simba na timu ya taifa ya Uganda, Emmanuel Okwi anatarajia kuondoka nchini wakati wowote kuanzia leo kwenda Austria kwa ajili ya kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa nchini humo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti Simba, Ismail Aden Rage, alisema kuwa mawakala watatu kutoka katika nchi za Uingereza, Serbia na Austria wamefanya mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo kwa ajili ya kumchukua Okwi kwenda kufanya majaribio katika nchi hizo.


Rage alisema kuwa kati ya mawakala waliowafuata, aliyetoka Austria ndiye aliyekamilisha taratibu zote na hivyo mchezaji huyo aliyeisaidia Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara atakwenda nchini humo.

"Hadi kufikia leo jioni (jana), uongozi utakuwa umejua Okwi anaondoka lini, lakini ni siku yoyote kuanzia kesho (leo) atakwenda Austria kuanza majaribio na baadaye anaweza pia kwenda katika nchi za Uingereza na Serbia," alisema Rage.

Alisema kuwa uongozi wake hauna pingamizi dhidi ya mpango huo kwa kuwa ni sehemu ya sera za klabu yao hivi sasa; ya kuwapa nafasi wachezaji wao kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi kila mara wanapopata nafasi hiyo.

"Hivi sasa klabu yetu inajivunia sana kwa kuona mchezaji kama Mbwana Samata akiendelea kufanya vizuri... yeye (Samatta) alipewa nafasi na ameitumia vizuri.

Hivi sasa ni mmoja wa wachezaji muhimu ndani ya klabu yake ya TP Mazembe na Simba imefaidika naye na itaendelea kufaidika kila atakapouzwa kwenda timu nyingine, hivyo na nafasi hii pia tunaitoa kwa Okwi kwenda nje," alisema Rage.

Alisema kuwa uongozi wake umeshaweka dau la kuanzia la kumuuza mchezaji huyo ambayo ni Euro 500,000 (zaidi ya Sh. Bilioni Moja).

Alisema wakala huyo wa Austria hakuwa tayari kuitaja timu anayokwenda Okwi kufanya majaribio na kuongeza kuwa hilo litajulikana baada ya  kutua nchini humo.

Mbali na kung'ara katika ligi kuu ya Bara, Okwi alionyesha kiwango cha juu pia katika mechi za Simba za michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Amekuwa aking'ara vilevile katika timu yake ya taifa ya Uganda ambapo aliisaidia kutwaa Kombe la Chalenji na wiki iliyopita aliifungia bao lililowapa sare ya 1-1 katika mechi yao ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Angola.

Wakati huohuo, Somoe Ng'itu anaripoti kuwa Simba watafanya ziara katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga kwa ajili ya kutembeza kombe lao la ubingwa wa Bara walioutwaa kwa staili ya aina yake baada ya kuwashindilia mahasimu wao wa jadi, Yanga kwa mabao 5-0.

Akizungumza jana, Rage alisema kuwa katika ziara hiyo, Simba itashuka dimbani Juni 16 kucheza  dhidi ya Toto African kwenye Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga na siku inayofuata watacheza kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza dhidi ya klabu ya nje ya nchi ambayo wataitaja baadaye.

Mechi hiyo ya Juni 17 itacheza kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba jijini Mwanza.
Rage alisema kuwa timu itaondoka jijini Dar es Salaam Juni 15 ikiwa na wachezaji wake wapya iliyowasajili pamoja na nyota wake kutoka kikosi cha vijana wenye umri chini ya miaka 20.

Aliongeza kuwa baada ya kutoka Kanda ya Ziwa, wataendelea na ziara yao katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

SIMBA DAY

Rage alisema kuwa katika sherehe ya Simba Day itakayofanyika Agosti 8, wanatarajia kukabidhiwa mabasi yao mapya kutoka kwa wadhamini wao, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na pia kutambulisha kikosi chao kipya.

Meneja wa bia ya Kilimanjaro, George Kavishe, aliipongeza Simba kwa kutwaa ubingwa wa Bara na kusema kuwa wanaamini mafanikio ya klabu hiyo yamechangiwa pia na udhamini wao.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment