Friday, June 8, 2012

Wanne kuamua mwenyekiti Yanga

David Mosha
Wagombea 28 kati ya 33 wamerudisha fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mdogo wa klabu ya Yanga ambapo wanne wanawania cheo cha uenyekiti wakiwemo John Jambele, Edgar Chibula na Sarah Ramadhani.

Wanachama ambao walichukua fomu hizo lakini hadi jana saa 10:00 jioni zoezi hilo la kurudisha fomu lilipofungwa walishindwa kurejesha ni pamoja na Muhingo Rweyemamu, Eliakim Mmaswi, Muzammil Katunzi na Isack Chanja.



Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ya Yanga, Francis Kaswahili, alisema kuwa baada ya kupokea fomu hizo, kamati itakaa na kuzipitia na hatimaye kutangaza majina ya wagombea waliotimiza taratibu za kuwania nafasi kama zilivyotangazwa.


Kaswahili alisema kuwa zoezi hilo litafanywa kati ya leo na kesho na watakua chini ya usimamizi wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).


Aliwataja wagombea wengine wanne wanaowania nafasi ya Makamu Mwenyekiti iliyoachwa wazi na Davis Mosha kuwa ni Ayoub Nyenzi, Yono Kevela, Ally Mayai na Clement Sanga.


Awali juzi Mayai alichukua fomu ya kuwania nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo lakini baadae alibadili mawazo wakati Kevela anawania pia na nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji.


Wanaowania nafasi nne za ujumbe ni Lameck Nyambaya, Ramadhani Kampira Mzimba, Mohammed Mbaraka, Ramadhani Saidi, Edgar Fongo, Beda Tindwa, Ahmed Gao, Mussa Katabalo, Goerge Manyama, Aaron Nyanda, Omary Ndula, Shabani Katwila na Jumanne Mwamwenya.


Wagombea wengine ni Abdallah 'Binkleb' Mbaraka, Peter Haule, Justine Baruti, Abdallah Sheria, Jamal Kisongo, Gaudecius Ishengoma na Kevela.


Uchaguzi huo mdogo wa Yanga unatarajiwa kufanyika Julai 15 katika ukumbi utakaotangazwa hapo baadaye hapa jijini Dar es Salaam.


Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliipa maelekezo Yanga kufanya uchaguzi huo mdogo kutokana na idadi kubwa ya viongozi waliokuwa madarakani wakiongozwa na Mwenyekiti, Lloyd Nchunga, wakitangaza kujiuzulu.


Viongozi waliobakia madarakani walikuwa ni Mohammed Bhinda, Tito Osoro, Salim Rupia na Sarah ambaye sasa ameamua kuwania nafasi ya juu ya uongozi.


Wakati huo huo jana katika makao makuu ya klabu ya Yanga kulikuwa na wanachama kadhaa waliojitokeza kuwaona wagombea wao waliokuwa wanarudisha fomu ambapo walikuwa wakiwashangilia wale waliokuwa wanawakubali.


Hata hivyo wagombea wengine walituma marafiki zao kuwarejeshea fomu hizo kimya kimya kuanzia juzi hadi jana wakati zoezi hilo lilipofungwa.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment