Friday, June 8, 2012

Takukuru yaihoji kamati ya Mrema

Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema  

Kauli ya Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, kwamba Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imekithiri kwa rushwa, imezua mambo, baada ya baadhi ya wajumbe wake kuanza kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhusiana na tuhuma hizo.

Hatua hiyo inadaiwa kuchukuliwa siku tano tangu mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ambaye ni Mbunge wa Bahi (CCM), Omary Badwel, kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kupokea rushwa ya Sh. milioni 1.


Habari za kuaminika kutoka Takukuru na ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam, zinaeleza kuwa, wajumbe hao wa LAAC walianza kuhojiwa na taasisi hiyo jana, huku wengine wakitarajiwa kuendelea kuhojiwa baadaye.

Kwa mujibu wa habari hizo, wa kwanza kuitwa na Takukuru na kuhojiwa ni mmoja wa maofisa waandamizi wa LAAC mwenye jukumu la kuwezesha shughuli za kamati hiyo.

WAJUMBE WATHIBITISHA

Baadhi ya wajumbe wa LAAC waliozungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti, walithibitisha kuhojiwa kwa wenzao na Takukuru.

“Na mimi ninayo barua ya kuitwa kwenda Takukuru kuhojiwa, nimetakiwa niende kesho (leo),” alisema mmoja wa wajumbe wa LAAC akithibitisha kuwapo kwa mahojiano hayo kati yao na Takukuru.

Mjumbe huyo alisema taarifa za kuaminika alizonazo ni kwamba, mahojiano yanafanywa na Takukuru kwa kuwahoji wajumbe kadhaa wa kamati hiyo kama si wote.

GODFREY ZAMBI

Mbunge wa Mbozi Mashariki (CCM), Godfrey Zambi, ambaye ni mjumbe wa LAAC, akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, alisema taarifa sahihi alizonazo ni kwamba, kuna baadhi ya wajumbe wenzake wa kamati hiyo walioitwa na wengine waliokwenda Takukuru kuhojiwa.

“Najua kuna watu wameitwa na wengine wamekwenda, lakini mimi simo, lakini kama ikitokea tutawaambia,” alisema Zambi.

ABDUL MTEKETA

Mbunge wa Kilombero (CCM), Abdul Mteketa, naye aliliambia NIPASHE kwa njia ya simu jana kuwa alimuuliza Makamu Mwenyekiti wa LAAC, Iddi Azzan, ambaye alimthibitishia kuhojiwa kwa baadhi ya wajumbe.

Aliwataja wajumbe hao kuwa ni pamoja na Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Suzan Kiwanga na Katibu wa LAAC, Mswige Bisile.

“(Makamu Mwenyekiti, Azzan), ameniambia pia kuwa hana uhakika, lakini huenda kamati nzima (LAAC) watakwenda (Takukuru kuhojiwa),” alisema Mteketa.

Hata hivyo, Mteketa alisema haogopi kuhojiwa na Takukuru kwa sababu wezi wanajulikana na kwamba, hana tamaa ya Sh. milioni moja.

Awali, Mteketa, alipoulizwa na NIPASHE kama naye alihojiwa na Takukuru au la, alisema hayumo katika orodha ya wajumbe wa LAAC waliohojiwa, hajawahi wala hajaitwa kwenda kuhojiwa na kwamba, hana taarifa zozote kama kuna wajumbe wa kamati hiyo wameitwa kuhojiwa na taasisi hiyo.

SUZAN KIWANGA

Kiwanga alipoulizwa na NIPASHE kwa njia ya simu, alisema bado hajajua kama atahojiwa au la na kusema: “Labda nitaitwa.”

SPIKA MAKINDA

Spika wa Bunge, Anne Makinda, alipotafutwa jana kwa njia ya simu kuzungumzia suala hilo, hakuwa tayari kuzungumza, badala yake alimwambia mwandishi: “Nipigie (simu) kesho.”

KAULI YA TAKUKURU

Awali, NIPASHE iliwasiliana na Ofisa Uhusiano wa Takukuru, Doreen Kapwani, ambaye alimshauri mwandishi kuwasiliana na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Taasisi hiyo, Alex Mfungo.

Mfungo alipoulizwa na NIPASHE, alikana Takukuru kuwahoji wajumbe hao wa kamati ya Bunge kwa maelezo kwamba hawana kitu cha kuwahoji.

“Hatuna mpango wa kuwahoji (wajumbe hao wa kamati ya Bunge). Tunawahoji kwa kitu gani?,” alihoji Mfungo na kuongeza:

“Kama unazo taarifa za tuhuma za rushwa kwa wajumbe hao tuletee, mimi sina taarifa hizo, ndio kwanza nazisikia kutoka kwako.”

NAIBU SPIKA

NIPASHE pia ilimtafuta Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai. Alisema hana taarifa zozote za kuhojiwa kwa wajumbe hao wa LAAC na Takukuru.

Pamoja na kukana kuwa na taarifa hizo, Ndugai alizungumzia uhalali wa Badwel kushiriki shughuli za kamati ya Bunge na Bunge licha ya mahakama kumuachia kwa dhamana.

Alisema mbunge huyo bado ana uhalali wa kushiriki shughuli zote za Bunge kwa kuwa bado mahakama haijamuona kuwa na hatia.

“Kwa kawaida kama mbunge hajahukumiwa na mahakama, anaruhusiwa kushiriki shughuli zote za Bunge, kwa kuwa anaonekana kuwa bado hajawa na hatia,” alisema Ndugai.

MAKAMU MWENYEKITI LAAC

Makamu Mwenyekiti wa LAAC, Iddi Azzan, ambaye pia ni Mbunge wa Kinondoni (CCM), alipoulizwa na NIPASHE jana, alisema hana taarifa za mjumbe yoyote wa kamati hiyo kuhojiwa na Takukuru.

Alisema pia hakuna kifungu chochote cha sheria kinachoeleza kwamba kama mjumbe akikutwa na tatizo, basi kamati yote itakuwa haifai.

“Hilo ni tatizo la mtu mmoja mmoja, lisihusishwe na kamati. Laiti kama ingekamatwa kamati yote inapokea rushwa. Hata hivyo, kukamatwa pia bado ni tuhuma mpaka ithibitishwe na mahakama,” alisema Azzan.

Jumapili wiki iliyopita, Kafulila akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, aliituhumu LAAC kuwa imekithiri kwa rushwa.

Kutokana na tuhuma hizo, alimtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuivunja kamati hiyo, vinginevyo yeye atajiondoa.

Pia aliitaka Kamati ya Maadili kulitumia Bunge kumvua ubunge, Badwel, kutokana na tuhuma za kupokea rushwa zinazomkabili kwa madai kwamba wananchi hawatakuwa na imani tena na kamati hiyo.

“Ikumbukwe Juni 13, 2011 nilieleza bungeni namna wabunge wa Kamati ya LAAC wanavyoomba rushwa kwa watumishi wa serikali, huku nikimtaja kwa jina Mbunge wa Bahi, Omary Badwel kuwa ni miongoni mwao,” alisema Kafulila ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo.

Kafulila alisema licha ya kutoa taarifa hiyo bungeni na kumwandikia Spika kuhusu vitendo vya rushwa vya baadhi ya wajumbe, hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa.

“Nilijitoa mhanga kwa kutaja majina ya wabunge wanaoomba rushwa kwa watumishi wa Serikali, lakini hatua hazikuchukuliwa, sasa leo Takukuru wamemtia mbaroni mmoja wao, bado hamuamini,” alisema Kafulila. 

“Sasa naomba niweke wazi kwamba kama Spika hataivunja kamati hii na kuunda nyingine nitajiondoa kwenye kamati kwa sababu itakuwa imepoteza imani kwa wananchi,” alisema Kafulila.

Alisema kamati hiyo imepoteza uhalali na sifa za kuendelea kuzikagua hesabu za serikali za mitaa kwa sababu wajumbe wake wanatuhumiwa kwa rushwa.

Kafulila alisema ni wajibu wa Spika kutafakari upya kuhusu hadhi ya kamati hiyo na kuipanga upya kwa kuzingatia maslahi ya umma.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema, ndiyo yenye jukumu la kusimamia hesabu za serikali za mitaa.

“Serikali legelege ni matokeo ya Bunge legelege kwa kuwa ni kazi ya Bunge kusimamia na kuidhibiti serikali kikatiba,” alisema Kafulila.

Mbunge huyo wa Kigoma Kusini aliitaka Bunge kuweka azimio la kumvua ubunge Badwel kwa tuhuma za rushwa zinazomkabili.

“ Kamati ya Maadili ya Bunge ifanye hivyo ikiwa ni hatua za kinidhamu kuchukuliwa kwa mbunge huyo kwa tukio hilo la aibu,” alisema.

Kafulila alisema hata mabunge ya Jumuiya za Madola ambalo Tanzania ni miongoni mwao, huchukua hatua za kinidhamu za kuwavua wabunge wanaotuhumiwa kwa makosa ya aibu kabla ya mahakama hazijatoa uamuzi.

Kwa mujibu wa Kafulila, Bunge la Uingereza limeshachukua hatua za kuwavua ubunge watuhumiwa zaidi ya 59 ili kujenga imani ya wananchi kwa Bunge lao.

“Kwa hiyo nafahamu kwa kutumia azimio, Bunge lina uwezo wa kumvua madaraka mbunge yeyote ambaye amefanya vitendo vya aibu vya kuliaibisha Bunge,” alisema. 

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 71(1) (d) Mbunge anaweza kupoteza nafasi yake ikiwa itathibitishwa kwamba amevunja masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Badwel na Mbunge wa Mbozi Mashariki (CCM), Godfrey Zambi, ni miongoni mwa wabunge waliotajwa na Kafulila katika Bunge la bajeti la mwaka jana kwamba, aliwaona wakichukua rushwa kwa viongozi wa halmashauri ambayo hakuitaja.

Badwel, ambaye alikamatwa na Takukuru akidaiwa kupokea rushwa kutoka kwa watumishi wa serikali katika hoteli moja jijini Dar es Salaam, alifikishwa mahakamani Juni 4, mwaka huu, kujibu tuhuma hizo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment