Friday, June 8, 2012

Chadema yatikisa CCM, CUF Lindi


Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk.Willibrod Slaa akiwahutubia kwenye Uwanja wa Ilulu Lindi jana.
Operesheni Okoa Kusini imevitikisa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Wananchi (CUF) mkoani Lindi.

Abdallah Madebe, aliyekuwa Meneja wa Kampeni za Mbunge wa Lindi Mjini, Salum Khalfan Barwan (CUF), alijiondoa katika chama hicho na kujiunga Chadema.
Pia Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Mbanja kupitia CCM, Issa Shahame, pia alitangaza ‘kujivua gamba’ na ‘kuvaa gwanda’ la Chadema.
Wote wawili walirejesha kadi za vyama vyao kwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, na kukabidhiwa kadi za chama hicho kilichofanya mkutano wake wa hadhara kwenye uwanja wa Ilulu mjini Lindi.
Mbali na viongozi hao, wanachama kwa maelfu walijipanga mistari mirefu kununua kadi za Chadema baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe,alisema Chadema imeamua kuikosoa CUF kutokana hatua ya chama hicho kikuu cha upinzani visiwani Zanzibar, kuisaidia CCM ibaki madarakani.

Alisema matatizo yanayoukabili umma hayahitaji kuwepo chama chenye muelekeo wa kuisaidia serikali iendelee kutawala, bali kukiondoa madarakani kwa vile kinaendeleza mfumo unaoathiri usawa kwa watu kunufaika na rasilimali za umma.
Aliwashukuru wananchi wa majimbo ya Lindi Mjini na Kilwa Kusini, kwa kuwachagua wabunge kupitia Chama Cha Wananchi (CUF), Salum Khafan Barwan na Seleman Bungala maarufu kama Bwege.

Mbowe alisema pamoja na mafanikio hayo, tatizo linalowakabili wabunge huo ni kuwemo ndani ya chama kinachoshirikiana na CCM kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

“Tatizo sio Bwege, tatizo sio Barwan, tatizo ni kwamba hatujui msimamo wa CUF, kwa maana ukienda Zanzibar wanakuwa watawala, ukija Bara wanakuwa wapinzani…inawezekana,” alihoji na watu wakaitikia “haiwezekani.”

Mbowe alisema kinachohitajika sasa ni kuunganisha nguvu ya umma pasipo kuwekeza kwenye itikadi za vyama vya siasa kwa vile hali hiyo itachochea mgawanyiko wa watu na kushindwa kuyajadili masuala yenye maslahi kwa umma.

“Cha msingi si chama gani, cha msingi ni sera gani na jinsi zinavyomsaidia mwananchi wa kawaida kuondokana na umasikini, ili tufikie ustawi wa nchi yetu,” alisema.

Mbowe alisema Chadema imekusudia kuendelea msimamo wake wa kuutetea umma na ikiwa kitashindwa, wananchi wasisite kutowachagua katika nafasi za uongozi.

“Tukishindwa kufikia matarajio ya umma msituchague, tuacheni na muendelee kupiga hatua, muendeleze safari ya kulikomboa taifa,” alisema.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment