|
WATOTO
mapacha walioungana waliozaliwa juzi katika hospitali ya Muhimbili
wamefariki dunia usiku wa kuamkia jana katika hospitali ya Taifa
Muhimbili.
Watoto hao walioungana kuanzia kifuani walikuwa na
jinsi moja ya kike na miguu miwili, lakini katika eneo la juu walikuwa
na vichwa viwili na mikono minne.
Mtoto mwenye vichwa viwili
Akizungumza ofisini kwake,
Daktari bingwa wa watoto, Augustine Massawe alisema watoto hao
wamefariki kabla ya kufanyiwa vipimo ambavyo vingeeleza uhusiano mzima
wa kimaumbile.
“Hawa ni mapacha walioungana, ni watoto wawili
ambao sehemu ya tumbo na kifua havikutengana wakati wa ukuaji akiwa
kwenye mfuko wa uzazi, na mara nyingi watoto kama hawa huzaliwa kwa
upasuaji,” alisema.
Alieleza kwamba kitaalamu watoto hao huitwa
‘Conjoined twins’ ambao hutengenezwa kwenye mfuko mmja na hutumia kondo
moja kwa kila kitu katika kupata mahitaji kutoka mama, pia iwapo
wangeendelea kuwa hai pengine wangekuwa na matatizo ya ubongo.
Dk
Massawe alisema kuzaliwa kwa watoto wa aina hiyo hakuhusishwi na imani
yoyote na si mara kwanza Tanzania kutokea uzao wa aina hiyo kwani kila
baada ya mwaka mmoja Hospitali ya Muhimbili hupokea uzazi wa aina hiyo.
Alisema
kuwa madaktari walishangazwa na namna mama huyo alivyoweza kujifungua
watoto hao kwa njia ya kawaida bila kufanyiwa upasuaji, kitendo ambacho
ni nadra sana kutokea.
Alieleza kwamba awali walijua kuwa ni
mtoto mmoja kwa mujibu wa vipimo vilivyowasilishwa, lakini wakati wa
kujifungua ndipo walipobaini kuwa ni watoto wawili walioungana.
Mama
wa watoto hao, Kidawa Mbonde (25) alisema anamshukuru Mungu kwani yote
ni mapenzi yake na kwamba kwa sasa anajisikia maumivu makali ya nyonga
kuliko kawaida, suala ambalo madaktari wamesema linatokana na kulazimika
kujifungua mapacha hao kwa njia ya kawaida.
|
No comments:
Post a Comment