Monday, June 11, 2012

Siku tatu za maombolezi ya Saitoti


Kenya imetangaza siku tatu za maombolezi baada ya kifo cha Waziri wa Usalama wa Kenya, Profesa George Saitoti, na naibu wake, Orwa Ojode, kwenye ajali ya helikopta ya polisi katika eneo la Ngong, nje ya Nairobi.
Profesa George Saitoti
Rais Mwai Kibaki alisema kifo cha Bwana Saitoti ni msiba mkubwa kwa taifa, na serikali imetangaza kuwa baraza la mawaziri litakutana Jumatatu, kujadili tukio hilo.

Idara ya polisi imesema uchunguzi utafanywa kujua sababu ya ajali hiyo, na balozi wa Marekani mjini Nairobi, amesema Marekani iko tayari kusaidia kwenye uchunguzi huo, ikiwa itatakiwa kufanya hivo.
Msemaji wa polisi alieleza kwamba inavoelekea kuanguka kwa helikopta hiyo lilikuwa tukio la ajali.
Raia wa Kenya walikuwa na masikitiko Jumapili, baada ya taarifa ya ajali hiyo kujulikana, na watu wamekuwa wakizuru nyumba ya kuhifadhi maiti mjini Nairobi kutoa heshima zao.
Makamo wa rais wa Kenya, Kalonzo Musyoka, alipofika kwenye tukio la ajali alitoa rambi-rambi zake na alieleza wale waliokuwamo ndani ya ndege ambao wote wameteketea:
"Ndege hiyo ya aina ya Eurocopter ya police airwing, ambayo ilikuwa inaelekea Yugis, ilikuwa imembeba Waziri George Saitoti, naibu waziri Orwa Ojode na maafisa rubani wa ndege, Nancy Gitwanja na Luke Oyugi, na vilevile askari wawili ambao wanakuwa wanaandamana na Waziri Saitoti, Inspector Tonkei na Thomas Murimi"
Rambi-rambi zimekuwa zikimiminika nchini Kenya, pamoja na za Kofi Annan, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, ambaye alipatanisha baada ya ghasia za uchaguzi uliopita nchini kenya.
Profesa Saitoti alikuwa akizungumza kwa ukali dhidi ya al-Shabaab na inaaminiwa alihusika na uamuzi wa jeshi la Kenya kuingia Somalia mwaka jana.
Bwana Saitoti aliwahi kuwa makamo wa rais na waziri wa fedha katika serikali ya Rais Moi, na akitarajiwa kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka ujao.
Alikuwa na umri wa mika 67.


Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya afariki dunia kwenye ajali ya ndege
Na: Salim Swaleh
Habari za hivi punde kutoka Nairobi, Kenya zinasema kuwa Helkopta ya polisi iliyokuwa imembeba Waziri wa Usalama wa Taifa, Profesa George Saitoti, naibu wake Orwa Ojode pamoja na maafisa wengine wa ngazi za juu serikalini imeanguka na kushika moto. Habari zaidi zinasema maafisa hao wa serikali wamefariki dunia pamoja na walinzi wao na rubani wa helkopta hiyo.  Helkopta hiyo iliyokuwa ikielekea katika eneo la Nthiwa nyumbani kwa Bw. Ojode imeanguka katika milima ya Ngon'g nje kidogo ya Nairobi. Helkopta hiyo ilikuwa na watu saba wakati wa ajali. Inafaa kukumbusha hapa kuwa, tarehe kama ya leo miaka minne iliyopita yaani Juni 10 mwaka 2008, helkopta ingine ilianguka na kumuua Waziri wa Barabara, Kipkalya Kones pamoja na Naibu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais Lona Laboso.

No comments:

Post a Comment