Monday, September 3, 2012

CHAMA CHA WAANDISHI WA MBEYA PRESS CLUB


HABARI MBEYA
P.O. BOX, 6120 Mbeya Tanzania
S. L. P 6120 Mbeya, Tanzania, TEL:
SIMU: TEL/FAX: 255 25 2500101
TEL/FAX: 255 25 2500101 E-Mail:mbeyapressclub@yahoo.com
E-Mail: mbeyapressclub@yahoo.com
CHAIRPERSON: +255754 301864 SECRETARY GENERAL + 255762246322

3/Sep /2012


TAMKO LA CHAMA CHA WAANDISHI WA HABARI MKOA WA MBEYA (MBPC) DHIDI YA JESHI LA POLISI NCHINI.


Chama cha waandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya (MBPC)kimepokea kwa masikitiko taarifa ya mauaji ya Mwandishi na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa habari Mkoa wa Iringa, Daudi Mwangosi yanayodaiwa kufanywa na Jeshi la Polisi Mkoani Iringa tarehe 2/9/2012.


Kutokana na mauaji hayo na kutoridhishwa na nguvu kubwa kupita kiasi inayotumiwa na polisi dhidi ya raia, Waandishi wa habari Mkoa wa Mbeya wanaungana na waandishi wa habari nchini kusitisha kutoa taarifa za jeshi la polisi hadi hapo jeshi hilo litakapokubali kuchukua hatua kali za kinidhamu kwa polisi waliohusika kufanya mauaji hayo akiwemo, Kamanda wa polisi Mkoa wa Iringa aliyeongoza operesheni hiyo.


Tamko hilo pia limeeleza wazi kuwa muda umefika kuwe na mkataba maalumu wa kazi kati ya waandishi wa habari na jeshi la polisi na kwamba atakayekiuka hatua za kisheria dhidi ya majukumu ya kila chombo zichukuliwe hatua kali za uwajibishaji.


Ili kujenga dhana ya uwazi na uwajibikaji,Waandishi wa habari Mkoa wa Mbeya wanamtaka Waziri wa mambo ya ndani, Mkuu wa jeshi la polisi nchini (IGP) na Kamanda wa mkoa wa Iringa wajiuzulu nyadhifa zao kwa kuwa wameshindwa kusimamia vyema usalama wa raia na mali zao.


Pia Tamko hilo limebainisha mfumo wa uundwaji wa tume ya kuchunguza kifo hicho haupaswi kuongozwa na Jeshi la polisi kwa kuwa ndio waliohusika na mauaji hayo na kwamba tume huru itakayoundwa ipewe muda maalumu ili majibu yapatikane mapema na kwa haraka na hatua za kisheria zichukuliwe kwa wahusika.


Waandishi wa habari Mkoa wa Mbeya, wanaamini kuwa Serikali na jeshi la polisi litachukua hatua stahiki kwa waliohusika na mauaji ya Mwandishi Daudi Mwangosi, na pia Polisi watajitathmini upya katika utendaji wa shughuli zake hasa katika udhibiti wa vurugu na uzuiaji wa maandamano.


………………………………..

Christopher Nyenyembe,
Mwenyekiti MBPC.

Nakala ;


1.Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama.


2.Inspekta wa Jeshi la Polisi(IGP).


3.Vyombo vyote vya Habari.

No comments:

Post a Comment