Sunday, June 17, 2012

MWENYEKITI WA CCM MATATANI KWA KUFADHILI KUNDI LA TALBAN

MWENYEKITI wa CCM kata ya Olturument,Thelesia Kitalu anatuhumiwa  kuihujumu bodi ya maji ya kata hiyo,(Meviwasu) kwa kuhamasisha wananchi kungóa mita za maji zinazofungwa kwenye makazi yao, sanjari na kukata mabomba ya maji na kujiunganishia kinyemela akiwaeleza kuwa maji hayo ni ya bure  na haifai kuyalipia .

Pia anadaiwa kufadhili kikundi cha vijana 12 wanaotambulika kwa jina la ‘’Talban’’,ambao wamekuwa na kazi moja ya kungóa mita za mabomba  majira ya usiku na kuendesha vurugu kwa kuwapiga wafanyakazi wa Meviwasu ,wakipinga hatua ya kulipa maji hayo kwa bill huku akiwaeleza wananchi kuwa shirika la Meviwasu linalojihusisha na mradi wa usambazaji wa maji vijijini, halipo kisheria.

Hayo yalibainika  katika mkutano mkuu wa dharura wa bodi ya maji (Meviwasu)uliofanyika katika kijiji cha Ilkishini  wilaya ya Arumeru,uliowahusisha viongozi wa kitongoji ,kijiji na kata,madiwani ,askari polisi pamoja na wazee mashuhuri  kutoka vijiji sita vinavyohudumiwa na shirika la Meviwasu .

Akizungumza katika mkutano huo mwenyekiti wa bodi ya maji ,Lomayani Meshurie alisema kuwa lengo la mkutano huo wa dharura ni kujadili hujuma ya ungóaji wa mabomba na mita za maji unaoendelea,ambapo alielekeza lawama moja kwa moja kwa mwenyekiti huyo wa ccm anayedaiwa kuwashawishi wananchi wasikubali kuwekewa mita ili walipie huduma ya maji safi.

Baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji  waliunga mkono hoja hiyo na kuthibitisha wazi kuwa mwenyekiti huyo wa ccm ndiye amekuwa akitumia mikutano yake ya hadhara  kuwashawishi wananchi waukatae mradi huo wa maji ,akidai shirika hilo la Meviwasu ambalo limetokana na muunganiko wa vijiji viwili vya Muklat na Enaboishu haliko kisheria.

Shirika la Meviwasu limekuwa likiendesha mradi  huo wa  maji  kwa vijiji saba  vilivyomo wilayani Arumeru,chini ya ufadhili wa shirika la ( Ubu) la nchini Denmack linalojihusisha kusaidia miradi endelevu ya maji kwa nchi zinazoendelea.

Mmoja wa wazee mashuhuri mkazi wa kijiji cha Ekenywa, Mzee Logolie Sailevu alisema kuwa mwenyekiti huyo amekuwa akihujumu mradi huo kwa lengo la kujipendekeza kwa wananchili ili kujenga mazingira ya kuchaguliwa katika nafasi ya uongozi ujao hatua ambayo imesababisha kukwama kwa zoezi la usambazaji maji kwa wananchi.

‘’huyo mama achukuliwe hatua  kali hapa tunao  askari polisi ili kushughulika masuala hayo ,amekuwa akiongoza kundi la vijana  wa Talban ili kungóa mita ndio maana vijiji vingi havina maji, huu mradi umeshindwa kufikia malengo kwa sababu yake ‘’alisema Mzee Logolie huku akishangiliwa

Akizungumza  katika mkutano huo,mwenyekiti huyo anayetuhumiwa, alikiri kulifahamu kundi hilo la Talban na kudai kuwa  si kweli kwamba analifadhili ili kungóa mita za maji ila alisisitiza kuwaamekuwa na ukaribu na kundi hilo kwa sababu wamekuwa wakimfuata na kumweleza kero mbalimbali.

‘’ni kweli mwenyekiti hilo nkundi la vijana 12 nalifahamu ila mimi sihusiki kuwatuma wangóe mabomba na kukata mita za maji,mimi naomba sheria ichukue mkondo wake kama kweli kuna watu wanafanya mchezo huo mimi sihusiki’’alisema Mwenyekiti huyo.

Mkutano huo uliadhimia kuwachukulia hatua kali wale wote waliotajwa kuhusika kuhujumu maji akiwemo mwenyekiti huyo ,sambamba na kuwakatia maji wananchi wakorofi waliogoma kulipia huduma hiyo na kuwafikisha mahakamani  kwa kutumia sheria za maji ambazo zinatumika kote nchini.

No comments:

Post a Comment