Saturday, June 23, 2012

Ndege ya Uturuki yapotelea kwenye bahari ya Meditteranean

Waziri Mkuu wa Uturuki Tayyip Erdogan amesema kuwa moja kati ya ndege za kivita  za  nchi  hiyo, imepotea katika eneo la bahari ya Meditteranean huku kukiwa na taarifa zisizothibitishwa kuwa Syria imekiri kuitungua.
 Vyombo vya habari vinaarifu kuwa Erdogan alisema hapo awali kuwa Syria imetangaza kuitungua ndege hiyo aina ya F-4 fighter jet, na kuwa imeomba msamaha kwa kitendo hicho.

 Hata hivyo waziri mkuu huyo amesema kuwa hadi sasa hakuna taarifa zozote kuhusu kilichoipata ndege hiyo.
Ndege hiyo ilipoteza mwelekeo baada ya kupaa kutoka kiwanja cha ndege kwenye jimbo la Malatya lililopo kusini mashariki mwa Uturuki.
 Tukio hilo limezusha wasiwasi huenda likasababisha kuzidi kwa mzozo unaoendelea nchini Syria.

Uturuki imekuwa ikiikosoa Syria kuwa inatumia nguvu za kijeshi dhidi ya wapinzani wa utawala nchini humo katika vuguvugu lililodumu kwa miezi 16 sasa.

No comments:

Post a Comment