Waziri Mkuu,Mizengo Pinda
Waandishi Wetu, Dar na Dodoma WAZIRI
Mkuu, Mizengo Pinda amesema kuanzia mwaka huu madiwani wote nchini
wataanza kulipwa viwango vipya vya posho vilivyoboreshwa.
Akisoma
hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu
(Tamisemi), kwa mwaka 2012/13, Pinda alisema tangu mwaka jana Serikali
iliahidi kuwaongezea posho madiwani. “Wakati nahitimisha mjadala wa
hotuba ya bajeti ya ofisi yangu mwaka jana, niliahidi kuwa Serikali
itaangalia upya viwango vya posho za madiwani kwa lengo la kuviongeza,”
alisema Pinda na kuongeza; “Sasa zoezi hilo limekamilika na kuanzia mwaka 2012/2013 madiwani watalipwa viwango vipya vya posho vilivyoboreshwa.”
Alisema
ili kuwawezesha viongozi wa mikoa na wilaya kutekeleza majukumu yao ,
Serikali imetoa mafunzo kwa wakuu wa mikoa na wilaya na kutekeleza ahadi
yake ya kutoa mafunzo kwa madiwani 4,451 nchini.
“Ni imani
yangu kwamba baada ya mafunzo hayo, utendaji kazi wa viongozi hao
utakuwa ni wa ufanisi zaidi,” alieleza matarajio yake Pinda.
Mbali
na kuongezwa kwa posho hizo, aliwaagiza wakurugenzi watendaji wa
Mamlaka za Serikali za Mitaa kubandika kwenye mbao za matangazo katika
vituo vyote vya utoaji huduma, kiasi cha fedha kinachopokelewa kila
mwezi na matumizi yake.
Kwa muda mrefu madiwani nchini wamekuwa
wakilalamikia kiwango cha posho wanachopata sambamba na mishahara, huku
wakishinikiza kulipwa kama wabunge. Mbali na posho hizo, ameonya
kwamba watumishi wa Serikali watakaobainika kutafuna fedha za umma,
watavuliwa madaraka na kufikishwa katika vyombo vya sheria, na hakuna
atakayehamishiwa kituo kipya baada ya kuharibu kituo cha awali.
Alisema
mwaka 2010/11, Serikali ilitangaza nia ya kuanzisha maeneo mapya ya
utawala ya mikoa minne ya Simiyu, Katavi, Njombe na Geita pamoja na
wilaya mpya 19 na Tarafa 34, lengo likiwa ni kusogeza na kurahisisha
utoaji wa huduma kwa wananchi. “Tayari Serikali imeyaanzisha rasmi
maeneo hayo na uteuzi wa viongozi wa kusimamia mikoa na wilaya hizo
umefanywa,” alisema Pinda.
Kuhusu ripoti ya CAG Akizungumzia
viongozi watakaobainika kutafuna mali za umma ambao walitajwa katika
ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Pinda
alisema watachunguzwa na wakibainika watavuliwa madaraka.
“Wakivuliwa madaraka waliyonayo watafikishwa katika vyombo vya sheria,” alisema Pinda na kuongeza; “Serikali
haitawahamisha watumishi wa aina hiyo, bali hatua za kinidhamu na
kisheria zitachukuliwa wakiwa kwenye vituo vyao vya kazi.”
Pinda
aliwataka watendaji wakuu wa Serikali, bodi za wakurugenzi wa mashirika
ya umma na madiwani kuhakikisha wanashiriki ipasavyo katika kusimamia
fedha za umma kwa mujibu wa sheria, taratibu, miongozo na kanuni
zilizopo, na kubandika matumizi hayo kwenye mbao za matangazo. Alisema hatua hiyo itawezesha wananchi kufuatilia matumizi ya fedha zilizopelekwa kwa ajili ya utoaji huduma kwenye maeneo yao.
Ununuzi wa magari Akizungumzia
ununuzi wa magari ya Serikali maarufu kama mashangingi, Pinda alisema
Serikali inaendelea kupunguza matumizi yasiyo na tija hasa ununuzi wa
magari makubwa ya kifahari, ambayo gharama zake ni kubwa.
Alisema
kwa kuanza, magari yatakayonunuliwa yatakuwa ni yale yasiyozidi ukubwa
wa injini wa CC 3,000 kwa viongozi na watendaji wakuu na yasiyozidi CC
2,000 kwa watumishi wengine ambao wanastahili kutumia magari ya
Serikali.
Kambi ya Upinzani Kwa upande wake Kiongozi wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amemlipua Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda kwa kuzuia uchaguzi wa mitaa na vitongoji ili kupisha Chaguzi za
CCM. Mbali na hilo, ameitaka Serikali kutolea ufafanuzi suala la
gharama zilizotumika katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa
Tanzania, kama kweli zilikuwa Sh64 bilioni.
Akisoma maoni yake
kwa Ofisi hiyo ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2012/13, Mbowe alisema
kusimamishwa kwa baadhi ya chaguzi kumeidhinishwa na waziri mkuu
kutokana na chombo kinachosimamia kuwa chini yake. “Chombo cha
kusimamia uchaguzi huo kipo chini ya Waziri Mkuu ambaye ndio amekuwa
akitoa kauli ya kusimamisha ili kupisha uchaguzi wa CCM,” alisema Mbowe
na kuongeza:
"Kambi ya Upinzani, tunamtaka Waziri Mkuu kuwaeleza
wananchi kuwa anachukua hatua gani kwa hili ambalo limetokea kwani
limesababisha baadhi ya mitaa na vitongoji kutokuwa na viongozi kwa
sababu tu chama chake kinafanya chaguzi.”
Mbowe ambaye pia ni
Mbunge wa Hai, alisema Serikali imekuwa ikishindwa kutekeleza majukumu
yake kutokana na kutokuwa na fedha huku ikitumia fedha nyingi katika
sherehe mbalimbali za kitaifa.
“Katika maadhimisho ya miaka 50
(ya uhuru) yaliyofanyika mwaka jana, gazeti la The Citizen
linalochapishwa na Mwananchi Communications Limited lilisema kuwa
Serikali ilitumia Sh64 bilioni na mpaka sasa haijakanusha taarifa hizo,
kitendo kinachoashiria kuwa ni kweli,” alisema Mbowe na kuongeza:
"Serikali
inatakiwa kulitolea ufafanuzi ili wananchi waweze kujua ni kiasi gani
cha fedha kilichotumika kuliko kuendelea kubaki kimya na maswali mengi
yakitanda.” Mbowe alifafanua kuwa umefika wakati kwa Serikali
kuchagua sherehe ambazo ni za muhimu na kuwa zinaadhimishwa, kuliko hivi
sasa, ambapo imekuwa ikifanya hivyo kila sherehe na kuligharimu taifa.
Waliofukuzwa UDOM Mbowe
alikitaka Chuo Kikuu cha Dodoma kuwarejesha wanafunzi waliofukuzwa
mwaka jana kutokana na kupinga kumaliza masomo bila kufanya mazoezi kwa
vitendo.
“Kuwanyima haki zao wanafunzi ni kuendelea kuliweka
taifa katika hali mbaya na kinachotakiwa ni kuwarejesha masomoni mara
moja, ili wamalize masomo yao kuliko kuwaacha wakiendelea kukaa
nyumbani,” alisema Mbowe na kuongeza: “Vitisho na manyanyaso dhidi
yao ni dhambi ambayo itawarudia siku moja, na kinachotakiwa ni
kuwarudisha wanafunzi wote haraka iwezekanavyo.” |
No comments:
Post a Comment